Wachezaji Simba wamkuna Phiri
Imeandikwa na Jasmine Shamwepu, Dodoma; Tarehe: 8th February 2011 @ 11:06 Imesomwa na watu: 145; Jumla ya maoni: 0
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri KOCHA Mkuu wa Simba ya Dar es Salaam, Patrick Phiri amesema sasa amepumua na kuwapongeza wachezaji wake kwa ushindi wa mabao 2-0 juzi dhidi ya Polisi Dodoma katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa juzi, Phiri alisema matokeo hayo yamempa faraja kubwa kuweza kujipanga katika kutetea ubingwa wa ligi hiyo pamoja na mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Elan Club de Mitsoudje ya Comoro mwishoni mwa wiki hii.
Phiri alisema mechi hiyo ilikuwa ikimuumiza kichwa kutokana na Polisi Dodoma kuwa na wachezaji wazuri na wenye viwango vya juu.
Hata hivyo alisema kiwango kilichooneshwa na vijana wake kilikuwa cha kuvutia na kwamba sasa anaona kila dalili njema mbele kuhusu timu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Phiri alisema hivi sasa anajipanga vyema kwa mchezo dhidi ya Wacomoro utakaofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambao Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ili isonge mbele baada ya timu hizo kutoka 0-0 katika mchezo wa kwanza mjini Moroni.
Kama Simba ikifanikiwa kuwatoa Wacomoro itakumbana na timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ‘DRC', ambayo ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Amri Said, alisema baada ya kupata ushindi huo na kuongoza ligi wakiwa na pointi 33 mbele ya Yanga yenye pointi 32, ana imani watatangaza ubingwa mapema kabla ya ligi kumalizika.
Alisema Simba ipo nyuma mchezo mmoja, hivyo kama itashinda mchezo huo itakuwa imeizidi Yanga pointi nne, hali inayompa imani kwamba ubingwa utakuwa mapema kuliko wengi wanavyofikiri.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Polisi Dodoma, John Simkoko alisema kufungwa kwa timu yake kwa kiasi fulani kulichangiwa na kuoneshwa kadi nyekundu kwa mchezaji wake Semsue Juma dakika ya 61.
"Simba walitumia makosa yaliyofanywa na wachezaji wangu na ndiyo maana walitufunga kwa urahisi, lakini nakubali kushindwa, " alisema.