Saidi Maulidi ataka ushirikiano Stars
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 26th December 2010 @ 11:18
MSHAMBULIAJI Saidi Maulidi ‘SMG' amesema amefurahishwa kuitwa kwenye timu ya Taifa, Taifa Stars na kuahidi ataitumikia kwa moyo wake wote.
Aidha mshambuliaji huyo ameomba ushirikiano kwa mashabiki na wachezaji wenzake, kwani yeye peke yake hawezi kuipatia ushindi Stars.
Kocha Msaidizi wa Stars Silvestre Marsh juzi alitangaza kikosi cha wachezaji 23 wa timu hiyo kitakachokwenda Misri kwa ajili ya michuano ya Mto Nile.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, SMG ambaye anacheza soka ya kulipwa Angola alisema amefurahi na alikuwa akitamani kuichezea timu hiyo kwa muda mrefu.
"Mara ya mwisho mimi kuichezea Stars ilikuwa katika mechi dhidi ya Msumbiji ya kuwania
fainali za Kombe la Mataifa Afrika zilizofanyika Ghana mwaka 2008, tulifungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, tangu wakati huo sijagusa tena mpira kwenye ardhi ya Tanzania," alisema.
"Kwa hiyo Saidi kama Saidi peke yangu si kwamba ndio naweza sana, hapana ushirikiano
unahitajika kwa mashabiki wote na wachezaji wenyewe kwa wenyewe pia, tupeane ushirikiano tufanye vizuri kwenye mashindano hayo,"alisema.
Mbali na SMG, Marsh pia amemwita Athumani Machuppa anayecheza soka ya kulipwa Sweden.
Pia amewaita Jerryson Tegete wa Yanga mchezaji mpya wa Simba Ally Ahmed ‘Shiboli' na
mchezaji wa Kagera Sugar Godfrey Taita.
Tegete aliachwa takribani mara mbili na Kocha Mkuu wa Stars Jan Poulsen. Michuano ya
Mto Nile inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Cairo, Misri Januari 5 na Stars itaingia kambini kesho kabla ya kuondoka Januari 2.
Timu hiyo itakuwa kambini chini ya Marsh na kocha wa makipa Juma Pondamali na Kocha Mkuu Poulsen ambaye yuko nyumbani kwao Denmark kwa mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka ataungana nayo Cairo, Januari 3.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki katika michuano hiyo inayoshirikisha nchi zilizo Ukanda wa Ziwa Victoria na Mto Nile ni Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Ethiopia, Sudan na wenyeji Misri.
Lengo la michuano hiyo ni kuhamasisha kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kwa mujibu wa ratiba, Stars itaanza kufungua dimba la michuano hiyo dhidi ya wenyeji Misri Januari 5 saa moja jioni, kabla ya mechi hiyo Kenya itacheza na Sudan saa kumi jioni.