Hongera Simba SC kuwavua gamba mafisadi wa jengo
MWENYEKITI wa klabu ya Simba Alhaj Ismail Aden Rage juzi alitangaza klabu yake kusitisha mikataba ya wapangaji wote wa jengo lao la makao makuu lililo mtaa wa Msimbazi kwa kutoa notisi hadi Aprili 30.
Rage, alisema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya wajanja ambao waliingia mkataba kinyemela kwa kusaini mkataba mpya ambao ulikuwa unakwisha mwaka 2014 badala ya ule wa awali unaomalizika Aprili 30 mwaka huu.
Kupitia mikataba hiyo hewa baadhi ya wajanja wamekuwa wakivuna mamilioni kwa mgongo wa vitega uchumi hivyo huku klabu ikiendelea kuwa ombaomba na kujikusanyia kiasi cha shilingi bil.17.
Tanzania Daima tunachukua fursa hii kuwapongeza viongozi wa klabu ya Simba kwa kuvaa ujasiri huo kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitembeza bakuli kwa akili ya masuala mbalimbali ya kuendesha timu wakati fedha zinazopatikana katika vitega uchumi hivyo zingewawezesha kutatua shida zao.
Inasikitisha sana kwani wazee wa zamani wa klabu hiyo kwa uchungu waliokuwa nao walijikusanya na kujenga jengo hilo kwalo leo hii baadhi ya wajanja wananenepa matumbo na kuacha klabu ikiaibika.
Pamoja na hatua hiyo, tunapenda kuwashauri viongozi wa Simba wasiishie kuvunja mikataba bali wawasiliane na wanasheria wao kuona uwezekano wa kuwashtaki wale walioamua kuingia mikataba kinyemela na kuvuna mamilioni ya shilingi.
Sisi Tanzania Daima tunaamini huo ni wizi wa kuaminika ambao unapaswa kulaaniwa na kupigwa vita kwa nguvu zote katika medani ya michezo kwani unarudisha maendeleo ya klabu nyuma.
Ni vema uongozi wa Simba ukaanzisha utaratibu utakaokuwa wazi na ambao utajulikana na viongozi watakaoingia madarakani wakati wowote tofauti na hii siri iliyokuwepo kwenye mikataba hii ambayo ilisababisha viongozi waliopita wasibaini kuibiwa huko.
Sisi Tanzania Daima tumelazimika kutoa pongezi hizi kutokana na kuridhishwa kwetu na ushupavu uliofanywa na viongozi wa sasa wa Simba chini Al hajj Ismail Aden Rage ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya timu hiyo.
Hii ni kutokana na kwamba walioingia mikataba hii kinyemela ni wana Simba wenzao na huenda ndio maana viongozi waliopita walishindwa kuchukua hatua stahiki kwa sababu ya kulindana au kuoneana haya.
Kwa waliokuwa wapangaji kwenye klabu hiyo ni vema kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Simba na wakubali kuingia nao mikataba mipya kama bado wanataka kuendelea kufanya kazi hapo ili kodi zao zisaidie kuijenga Simba.
Pia tuchukue fursa hii kuwakumbusha wanachama wa Simba kuwa jukumu la kulinda na kutetea mali za klabu hiyo liko mikononi mwao, hivyo kila wanapoona hujuma inafanyika ni vyema wakaufahamisha uongozi wao kungali na mapema kuliko kusubiri mambo yaharibike.
Kama alivyosema Rage ‘kuanzia sasa kuibiwa basi' Tanzania Daima tunaamini mapambano hayo na mafisadi wa mali za Simba yaliyoanzishwa na uongozi wake yataendelea kwa nguvu zote, huku tukiwashauri viongozi wa timu nyingine kuiga mfano huo kwa maendeleo ya michezo nchini.