Viingilio poa Mapinduzi
Tuesday, 28 December 2010 21:36
Vicky Kimaro
MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi imepangwa kuanza kutimua vumbi Jumapili ijayo,ambapo mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Chuoni dhidi ya Azam Fc, huku viingilio vikiwa ni shilingi 1,000 na 3,000.
Akizungumza na Mwananchi, msemaji wa kamati ya maandalizi ya mashindano hayo Maulid Ahmed Maulid alisema tayari timu ya Simba imeshawasili na kuweka kambi kwenye nyumba za Zakaria zilizopo Chukwani visiwani humo.
Simba imeenda Zanzibar kwa mafungu, fungu la kwanza liliondoka juzi likiwa na wachezaji 13 na viongozi watano wakati fungu la pili lilitarajiwa kuondoka jana likiwa na wachezaji tisa.
"Simba wamewahi kuja watajigharamia wenyewe mpaka Januari Mosi ndio sisi tutaanza kuwalipia gharama za kambi, Yanga, Azam na Jamhuri Pemba zitawasili Januari Mosi," alisema Maulid.
"Mtibwa itawasili visiwani humu Januari 2 na timu za Zanzibar ambazo ni Chuoni, KMKM na Zanzibar Ocean View zitajitegemea kambi na waandaaji wa michuano hiyo watawapa posho pekee,"alisema Maulid.
Alisema,"Mashindano yanaanza mwishoni mwa wiki hii na kufikia kilele siku ya Mapinduzi Januari 12 na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein."
Siku kabla ya fainali za michuano hiyo ambayo Mtibwa ndio bingwa mtetezi kutakuwa na mechi kati ya wachezaji soka Maveterani wa Bara na wale wa Zanzibar.
"Na katika fainali kutakuwa na mechi ya utangulizi ambapo timu ya soka ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) itacheza na timu ya Baraza la wawakilishi," alisema.