Michezo magazetini leo...

Michezo magazetini leo...

Status
Not open for further replies.
Jamhuri yajiweka kando sakata la ZFA


Na Mwajuma Juma, Zanzibar

KLABU ya soka ya Jamhuri FC ya Pemba imesema, kwamba haihusiki na mvutano wowote unaoendelea, kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).Kauli hiyo ya Jamhuri, imekuja baada ya
klabu hiyo kuhusishwa katika klabu tatu ambazo zimedai kulifikisha mahakamani suala hilo, zikiwemo Zanzibar Ocean View na Miembeni pamoja na taasisi nyengine za soka.

Akizungumzia sakata hilo juzi Katibu Mwenezi wa timu hiyo, Kombo Omar Abdallah alisema timu yake haijashirikiana na mtu yeyote kukaa na kupanga kwenda mahakamani.

"Sisi tusihushishwe na mvutano wowote uliopo huko, hatujashirikiana na mtu wala kupanga kwenda mahakamani, sisi kama uongozi wa timu tutakaa kikao kulijadili hili", alisema.

"Sisi hivi sasa tunajipanga kwa ajili ya ligi na si vinginevyo," aliongeza katibu huyo.Awali timu hizo zilimwagiza wakili wao kutoka Kampuni ya AJM ‘Solicitors& Advocate Chamber, kuzitaka mamlaka tatu za michezo kutoa maelezo ya kina juu ya sababu za kushindwa kutekeleza na kusimamia vizuri majukumu yao.

Taasisi zilizotajwa kushindwa kutekeleza majukumu na timu hizo ni Baraza la Michezo la Taifa Zanzibar (BTMZ), Ofisi ya Mrajisi wa Vyama na Klabu za Michezo na ZFA.Timu hizo zilidai kwamba taasisi hizo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kulisababisha ZFA kuendesha kikao batili cha Uchaguzi Mkuu Desemba 31, mwaka jana.

 
Mtikisiko Jangwani
Wednesday, 19 January 2011 21:36

nchunga%20yanga.jpg
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga

Mwandishi Wetu
HALI inazidi kuwa tete katika klabu ya Yanga baada ya kikao cha jana jioni hadi usiku wa manane kuwa cha moto kutokana na misigano ya masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya klabu hiyo.

Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Hoteli ya Lamada, kilihudhuriwa na wajumbe 15 wakiongozwa na mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga na Makamu wake, davis Mosha.

Wengine waliokuwemo kwenye kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ni pamoja na Mbaraka Igangula, Paschal Kihanga, Charles Mngodo, Mohamed Binda, Sarah Ramadhani, Seif Ahmed, Peter Ossoro, Ally Mayayi, Mzee Yusuf na Salum Rupia.

Pia timu ya sekretarieti ya klabu hiyo inaundwa na Luis Sendeu ambaye ni Afisa Habari wa klabu hiyo na Katibu Mkuu, Lawrance Mwalusako.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zinapasha kuwa kati ya mambo yaliyokuwa yakijadiliwa ni pamoja na ushiriki wa Yanga katika Michuano ya Kombe la Shirikisho la soka Afrika, CAF, Ligi Kuu na hali ilivyo katika benchi la ufundi.

Mengi kati ya mambo yaliyokuwa moto ni misigano iliyopo kati ya mwenyekiti, Nchunga na makamu wake, Davis Mosha na kuelezwa kuwa wanatumia muda mwingi katika malumbano badala ya kushughulikia maendeleo ya timu hiyo.

Chanzo cha habari kilipasha kuwa Kamati ya Utendaji ilipendekeza kumalizika mara moja kwa malumbano hayo ambayo kimsingi hayasaidii zaidi ya kuvunja nguvu wachezaji na kufanya timu kuboronga katika mechi zake.

Kiliendelea kupasha chanzo hicho na kusema kuwa suala la kocha, Kosta Papic lilikuwa ndani ya ajenda kuu, na kwamba kilichokuwa kikielezwa ni kwamba kocha huyo anatakiwa aweke bayana sababu za kumkataa msaidizi wake, Fred Felix Minziro.

"Wewe angalia, Papic anasema hamtaki Minziro, hakuwahi kufanya naye kazi, hakuwahi kumuona sasa ana sababu gani za msingi za kumkataa?," kilipasha chanzo hicho cha habari.

Hata hivyo, chanzo hicho kilisema kuwa waliopewa kazi ya kusaka kocha, Seif Mohamed na Mosha wametakiwa kuongeza kasi kwa kuwa baada ya kumalizika Ligi Kuu, na mkataba wa kocha huyo utakapomalizika Aprili, klabu haitakuwa na mpango wa kuendelea naye.

Habari zaidi zinasema kuwa Kamati imeweka msisitizo kuwa Minziro atakuwa pembeni ya Papic hadi atakampomaliza mkataba wake kabla ya kupewa mikoba rasmi hadi hapo atakapopatikana kocha mwingine.

Juu ya meneja wa timu hiyo, chanzo cha habari kilipasha kuwa Emmanuel Mpangala anaondolewa kwenye nafasi hiyo na mikoba itakabidhiwa kwa Salvatory Edward, kiungo wa zamani wa timu hiyo.

Kuhusu suala la klabu kuwa kampuni, chanzo kilipasha kuwa kwa sasa unatafutwa muundo kamili kabla ya kuifanya klabu kuwa kampuni kamili. Muundo unaotafutwa ni jinsi ya kuiendesha kampuni ndani ya klabu, ugawanwaji wa hisa na aina za viongozi watakaoiendesha pamoja na nafasi ya wanachama.

Suala la Yanga kuwa kampuni kamili, limekuwa likisuasua kutokana na zoezi la kuhesabu wanachama kukwama kwa njia moja ama nyingine pamoja na jinsi gani ya kutengeneza hisa kwa kila mwanachama mwenye sifa.

Mbali na suala hilo, suala la wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu, ni kati ya mambo yaliyochukua nafasi katika kikao hicho na zaidi ni hatua ya kumpa nafasi katika baraza hilo, Abbas mtemvu, Mbunge wa Temeke.

Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo linaundwa na Mama Fatma Karume, Yusuf Manji, Francis Kifukwe na Mtemvu pamoja na mtu mwingine ambaye anatakiwa kuongezwa ili kukamilisha idadi ya watu watano.

Baada ya kutangazwa Mtemvu kuwemo kwenye baraza la wadhamini, hatua hyo imechukuliwa kwa hisia tofauti huku baadhi wakidai utaratibu haukufuatwa kumopitisha barazani wakitaka jina lake lijadiliwe kwanza na kamati ya Utendaji.

Katika hatua nyingine, Wazee wa klabu ya Yanga walitinga kwenye ofisi za mdhamini wa klabu hiyo na kumweleza kuwa Yanga hakuna mgogoro bali ni watu wachache wasioitakia mema yanga ndiyo wanachocghea mgogoro huo.

Wazee hao walitoa onyo kwa wanaochochea mgogoro ndani ya Yanga kuacha mara moja kwani ni mtu wanamfahamu na aendelea watamtaja na maamuzi mengine yatafanyika.

Katika taarifa yao ya pamoja, wazee hao walisema kuwa wanatoa karipio hilo na endapo mgogoro utaendelea, watakaa mwezi ujao siku kama ya jana kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kuuzima kabisa mgogoro huo.
 
Gerrard ataka Dalglish aendelee kuinoa Liverpool


LONDON, Uingereza

STEVEN Gerrard anamuunga mkono kocha mpya wa muda wa timu hiyo, Kenny Dalglish kupata mkataba wa kudumu wa muda mrefu baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi sita katika msimu huu.Kocha huyo
amechukua mikoba ya kuinoa timu ya Anfield baada ya kumtimua, Roy Hodgson kutokana na matokeo mabaya.

Lakini nahodha wa timu hiyo, Gerrard anataka kuona King Kenny anakuwa kocha kamili kwa mara ya pili kwa Liverpool.

Alisema anatamani wamalize msimu wakiwa na matokeo mazuri, ili aweze kupata mkataba wa muda mrefu na kuongeza kuwa yuko tayari kujituma kwa ajili ya matokeo mazuri ya kocha huyo.

"Mimi siwezi kuongopa, wakati Kenny aliposema alikuwa anakuja nyuma, ilikuwa ni kuinua ari kubwa. Ninampenda binafsi na nimefurahia siku chache za kufanya kazi naye pamoja.

Alisema siku chache tangu kuanza kwake kazi, ameona tayari timu imeanza kuwa na mwelekeo mzuri kwa wachezaji kuwa na ari uwanjani.

Licha ya matokeo ya kufungwa mechi mbili na sare moja tangu
Dalglish kuanza kazi, timu imeboreka kiuchezaji na Gerrard anaamini kocha huyo aliwahi kuichezea timu hiyo anaweza kuendelea kuinoa baada ya msimu huu kuisha.

Gerrard alisema kocha huyo ana uwezo wa kuwaunganisha wachezaji na ni wakati wao kuungana naye kwa ajili ya kuleta matokeo mazuri. Alisema matokeo mabaya ni kitu ambacho kila mmoja kwenye klabu hiyo kinamsikitisha, lakini kunapokuwa na matokeo mabaya si vyema kumlaumu mtu mmoja.

Kutokana na ufundishaji wake, wachezaji wamekuwa wakijituma katika mazoezi kutokana na kuwa na mahusiano mazuri na wachezaji.Wakati huohuo, Liverpool imetangaza kumuuza winga wake Ryan Babel na timu ya Ujerumani, Hoffenheim itamchukua.

Hatua hiyo imekuja wiki moja tangu Dalglish, kuanza kukisuka kikosi chake na inadaiwa kuwa atauzwa kwa pauni milioni saba.Mchezaji huyo anakubaliana kuhusu maslahi yake na miamba hao wa Ujerumani.

 
Aliyempiga risasi Cabanas atiwa mbaroni Wednesday, 19 January 2011 21:23 MEXICO CITY, Mexico
MTU mmoja ametiwa nguvuni kwenye mji mkuu wa Mexico, Mexico City kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kufanya shambulio kwa kumpiga risasi mchezaji wa timu ya taifa ya Paraguay, Salvador Cabanas.

Jose Jorge Balderas, maarufu "J.J." amekamatwa na askari wa Mexico wanaopambana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya alitiwa nguvuni katikati ya mji wa Mexico City, msemaji wa Shirikisho la Kupambana na Dawa za kulevya, Ramon Eduardo Pequeno aliwaambia waandishji wa habari.

Balderas alionyeshwa kwa waandishi wa habari huku nywele zake akiwa amezitia dawa na kuwa nyeusi. alisimama akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Pequeno alisema Balderas alikanusha kuhusika na tuhuma za kumpiga risasi Cabanas na badala yake akamtuhumu Francisco Jose Barreto Garcia, ambaye anye alikamatwa mwaka jana kwa tuhuma hizo.

Balderas alisema tukio lilitokea wakati huo akiingia bafuni na alikutana na Salvador Cabanas na kumuuliza nani alkimruhusu kutumia choo.

Alisema, mtuhumiwa alimwambia mpepelezi kuwa mwanasoka huyo alijibu kwa kutumia hali zote, kwa maneno na vitendo. Baadaye Garcia, ambaye alimuona Balderas' akiingia na kumpiga risasi Cabanas kichwani akiwa karibu naye, Balderas alidai.

Walioshuhudia walisema, Cabanas na Balderas walikuwa wakizozana na Balderas ambaye alimuuliza mchezaji huyo wa Paraguay juu ya uwezo wa soka yake katika klabu yake. Cabanas aliamua kumtwanga risasi.

Mchezaji huyo alipigwa risasi ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya Fainali za Kombe la Dunia 2010 wakati huo Paraguay ikiwa imefuzu na yeye alitarajiwa kucheza.

Balderas alikamatwa akiwa na watu wengine sita walioko katika mtandao wa dawa za kulevya na J.J. alikimbia kujificha baada ya kumpiga risasi Cabanas.

Mtandao huo unaouza dawa za kulevya na bunduki unaoishi katikati ya Mexico City katika kitongoji cha Huixquilucan, Pequeno alisema. Kati ya watu waliokamatwa, yumo mwanamke anayejihusisha na amsuala ya mitiondo ambaye ni 'bibi' wa Balderas.

Watu hao walikamatwa walipokuwa wakionyesha hati 'feki' za kusafiria pamoja na vitambulisho katika mabegi yao yaliyokuwa yamejaa cocaine, bunduki, alisema Pequeno.

Msemaji huyo alisema kuwa Balderas alikiri na kusema anamtambua ni kati ya wahusika wa Beltran Leyva na waliwahi kufika kwenye hafla zao mbalimbali.

 
Wachezaji Stars wadai walizidiwa
Wednesday, 19 January 2011 21:26

Doris Maliyaga
TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars' imewasili jana alfajiri ikitokea Cairo Misri ilikokuwa ikishiriki Michuano ya Bonde la Mto Nile huku wachezaji wakidai kuwa walizidiwa kimchezo na ndiyo sababu ya wao kuboronga na kushika nafasi ya tano.

Taifa Stars na wenyeji Misri ndiyo timu zilizokuwa zimebeba mastaa mbalimbali katika mashindano hayo tofauti na ilivyokuwa kwa timu zingine zilizoshiriki katika mashindano hayo.

Mara baada ya kuwasili nchini, wachezaji wa Taifa Stars waliiambia Mwananchi kwa nyakati tofauti kuwa lililowasababisha kufanya vibaya ni kuzidiwa uwezo wa kutandaza soka.

Beki wa kati wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro' alisema: "Wenzetu walituzidi kila kitu ndiyo maana tumefanya vibaya, hakuna sababu yoyote nyingine, kama maandalizi yalikuwa mazuri na yalikuwa ya kuridhisha ila uwezo ndiyo tatizo.''

Said Maulid, mshambuliaji anayecheza soka la kulipwa nchini Angola alisema: "Wenzetu walituzidi na sisi hatukuwa na jinsi tulijaribu kadri ya uwezo wetu, lakini ndiyo hivyo ikashindikana.''

Naye Ally Shiboli anayeichezea Simba na Zanzibar Heroes alisema mashindano yalikuwa mazuri, lakini walizidiwa na kwa ujumla wenzao waliwazidi kila kitu na kusema pia kuwa maandalizi hayakuwa makubwa kwani walishtukizwa.

Salum Machaku anayeichezea Mtibwa Sugar hakuwa tofauti na kauli za hao waliotangulia isipokuwa Stephano Mwasika alisema,"Mashindano yalikuwa magumu na kila timu ilikuja ikiwa imejiandaa vema, sisi tulivuna tulichopanda.''

Kipa wa Majimaji, Said Mohamed alisema,"Kiujumla mashindano yalikuwa magumu na wenzetu walituzidi.''
 
Simba kusaka tiketi ya Brazil leo Wednesday, 19 January 2011 21:27

Clara Alphonce
SIMBA inashuka dimbani leo kucheza mchezo wa kirafiki na Atletico Paranaense ya Brazil, mchezio utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa huku ikimjaribu mchezaji wake raia wa Cameroon, Eke Cosmas.

Mchezaji huyo ambaye ni kiungo amekuja katika klabu hiyo kwa ajili ya kujaribiwa na katika mechi ya leo atakuwa ni mmoja wa wachezaji wanaotaraji kuongoza Simba kwenye mchezo huo.

Afisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema jana kuwa mchezaji huyo yuko katika majaribio kwani alitua nchini wiki iliyopita na endapo atafaulu majaribio hayo watabaki naye mpaka kwenye usajili wa msimu ujao.

Endapo Cosmas atafuzu majaribio yake, atawaweka mashakani wachezaji viungo wawili wa kimataifa ambao ni Hilal Echessa, Jerry Santo pamoja na mkongwe, Mohamed Banka.

Simba inaingia dimbani leo ikiwa na mawazo ya kwenda Brazil kwa ajili ya kuweka kambi baada ya Mkurungezi wa timu ya African Lyon, Rahma Kharoos ambaye ndio aliyeileta timu hiyo kutoka Brazil kuiahidi Simba kuipeleka nchini humo lakini endapo tu, itashinda mchezo wa leo.

Hata hivyo, mechi ya leo itakuwa na hamasa kubwa baada ya mkurugenzi huyo kuruhusu mashabiki kuingie bure baada ya kuona viti vikiwa tupu katika mchezo dhidi ya Yanga juzi kutokana viingilio walivyoweka kuwa vikubwa.

Meneja wa Simba, Innocent Njovu alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na mpaka sasa wachezaji majeruhi katika timu ya Simba ni Uhuru Seleman na Emmanuel Okwi.

Alisema huenda kocha wao Patrick Phiri akawatumia wachezaji waliokuwepo katika timu ya taifa nchini Misri waliojiunga na wenzao jana au asiwatumie na kuwachezesha wale waliokuwepo.

Katika hatua nyingine, klabu ya Yanga imelalamikia maamuzi ya mratibu wa ziara ya Wabrazil hao, Rahma kuwa haikuwatendea haki kwa kuruhusu mashabiki kuingia bure kwenye mechi ya Simba wakati wao walicheza viti vikiwa wazi.

Yanga ilipambana na Wabrazil hao na kufungwa mabao 3-2 kwenye uwanja huo, katika mechi iliyokuwa na mashabiki kiduchu kabla ya mratibu huyo kutoa ofa kwa Simba kwa mashabiki wake kuingia bure na endapo itashinda, Simba itakwenda Brazil.

 
Mwape: Subirini ligi ianze
Wednesday, 19 January 2011 21:25

Jessca Nangawe
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Davis Mwape amewaonya wanaomkashifu kuwa hana uwezo wa kuifungia timu yake na amewaambia wasubiri kwani wataona mambo yake mara atakapoanza kucheza katika mzunguko huu wa lala salama.

Mwape ambaye amesajiliwa katika dirisha dogo akitokea Zambia, alisema amekuja kuonyesha makali yake na kuhakikisha anaisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa na si vingine hivyo kwa wale wanaomkejelli amewataka kusubiri mambo yake.

Mwape aliiambia Mwananchi juzi mara baada ya mchezo wao dhidi ya Atletico ya Brazil kuwa Yanga bado ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na nafasi iliyopo na yeye amekuja kuhakikisha anaifikisha mbali hivyo wajibu wake ni kuifungia magoli kadri ya uwezo wake.

Alisema hajacheza mchezo wowote wa ligi hivyo ana matarajio makubwa ya kuonyesha kiwango chake hivyo mashabiki wake watarajie mazuri kutoka kwake.

"Nimekuwa nikikutana na changamoto mbalimbali najua hii ni kutokana na ushindani uliopo, naamini timu zote zimejiandaa vizuri kila moja anataka kuwa bingwa lakini mimi lengo langu ni moja kuipeleka Yanga kutwaa ubingwa," alisema Mwape.

Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na itakuwa na kibarua dhidi ya AFC katika kufungua pazia la mzunguko huu wa lala salama.

 
Saba za Bonanza la Angetile zatajwa Send to a friend Wednesday, 19 January 2011 21:25

Mwandishi Wetu
TIMU saba zitashiriki bonanza la kumpongeza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, Angetile Osiah linaloandaliwa na timu ya soka ya Pugu Kigogo Fresh Veterans, zimetajwa.

Mratibu wa bonanza hilo, Bonaventura Mphuru aliliambia Mwananchi jana kuwa timu hizo zitapelekewa barua rasmi za mwaliko kushiriki bonanza hilo.

Osiah aliyeteuliwa Katibu Mkuu wa TFF hivi karibuni, ni mshambuliaji wa Pugu Kigogo Fresh Veterans.

Mphuru alizitaja timu hizo kuwa ni pamoja na timu ya soka ya waandishi wa Habari za Michezo, TASWA FC na timu za maveterani za Ukonga, Kitunda, Stakishari, Vituka, Pugu Kajiungeni na timu ya soka ya Radio Times.

"Tunaandaa bonanza kubwa la aina yake na hizo ndizo timu zitakazoshiriki, kwa sasa tunakamilisha suala la burudani na tutatoa taarifa rasmi karibuni," alisema Mphuru.

 
Henry: Arsenal itaifunga Barcelona UEFA Wednesday, 19 January 2011 21:22

LONDON, England

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Arsenal na baadaye Barcelona, Thierry Henry amesema wachezaji waliopo katika kikosi cha sasa wanaweza kumaliza ukame wa mabao pamoja na kutwaa ubingwa wanaoutafuta kwa kipindi kirefu.

Arsenal ambayo jana usiku ilikuwa ikicheza na Leeds United mchezo wa marudiano wa Kombe la FA bado inapigana katika mashindano ya aina nne na Henry anasema kuwa timu hiyo itatwaa ubingwa mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanz atangu kuhamia Uwanja wa Emirates mwaka 2006.

Mchezaji huyo bado anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi akiwa Arsenal, na anasema kuwa anataka kuona klabu hiyo inatwaa ubingwa msimu huu.

"Vijana wa sasa walioko Arsenal wanacheza kwa kujiamini sana," aliliambia The Sun. "Kila mmoja anamtegemea mwenzake – Arsenal inacheza soka ya kuvutia sana.

"Nimekuwa shabiki wa Arsenal na naipenda nataka kuona inatwaa ubingwa na kuleta furaha kw wachezaji, viongozi na mashabiki.

"Wachezaji hawa wana kipaji cha aina yake, lakini kuna kitu wanakikosa, kutwaa ubingwa."

Henry, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya New York Red Bulls, amekuwa akijifua na Arsenal alipokuwa akijiandaa na msimu mwingine wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS).

Mfaransa huyo alisema kuwa kila mara anakuwa na hamu ya kuiona Arsenal na hasa katika mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa ULaya dhidi ya Barcelona mwezi ujao na kuwa timu hiyo inaweza kuifunga, mechi yao itachezwa mapema mwezi ujao.

Henry, aliondoka Arsenal na kujiunga na Barcelona in 2007na akiwa na miaka 33, alisema kuwa hana wasiwasi kuwa Gunners itaihofia timu hiyo na kuwa mwaka huu utakuwa wa Arsenal.

"Hizo ni timu kubwa duniani na zenye uchu wa kupata ushindi kila mwaka," alisema.

 
Yanga, Simba msipuuze wapinzani Monday, 17 January 2011 12:48

KLABU za Simba na Yanga ndizo zitaiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika na kombe la washindi mwishoni mwa mwezi huu.

Simba itakayoshiriki katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika itaanza kwa kucheza dhidi ya Elan Club Mitsoudje ya Comoro kati ya tarehe 28,29 au 30 mwezi huu na kurudiana kati ya tarehe 11,12 au 13 mwezi wa pili.

Yanga itakayoshiriki kombe la washindi barani Afrika yenyewe itaanza kwa kucheza na Dedebit ya Ethiopia pia kati ya kati ya tarehe 28,29 au 30 mwezi huu na kurudiana kati ya tarehe 11,12 au 13 mwezi wa pili.

Tunasikitika kuona maandalizi duni yanayofanywa na klabu hizi huku tukishuhudia wachezaji na viongozi wao wakiwapuuza wapinzani wao Wacomoro na Waethiopia.

Tunashangazwa kuona viongozi wa klabu ya Yanga wakirumbana hali inayosababisha viongozi hao kushindwa kuisaidia timu na wachezaji kufanya vibaya uwanjani.

Tunaamini lengo la kushindana ni kupata ushindi lakini kuna kushinda, kushindwa na kutoka sare ila kitendo cha wachezaji na viongozi wa Simba na Yanga kuzipuuzia timu za Elan na Dedebit tunaona siyo sawa kwa sababu tulitegemea kuona timu hizo zikichukulia kila mechi kwao ni sawa na fainali.
 
TFF iandae mapema timu Michezo ya Afrika Monday, 17 January 2011 12:51

MICHEZO ya 10 ya Afrika 2011 inatarajiwa kufanyika mjini Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3 mpaka 18, ambapo wanamichezo watashindana katika michezo 23 tofauti.

Katika michezo hiyo 23 tofauti mchezo mmoja wapo ni mchezo wa soka ambao utashirikisha timu za vijana chini ya miaka 23 kwa wanaume na wanawake.

Hivi sasa mechi za awali za kufuzu kushiriki mashindano hayo kwa upande wa soka ambapo kwa baadhi ya timu zimeshaanza na zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi huu kabla ya kuanza raundi ya kwanza mwezi April.

Ni timu nane tu kwa wanaume na nane kwa wanawake zinatakiwa kufuzu kushiriki katika mashindano ya Afrika mjini Maputo Septemba 3 ili kuungana na mwenyeji Msumbiji ambao wamefuzu moja kwa moja.

Kwa upande wa wanaume Tanzania itaanza harakati zake katika raundi ya kwanza kati ya Aprili 15-17 kwa kucheza na Uganda na kurudiana nao kati ya April 29 na Mei 1.

Kama Tanzania itaifunga Uganda itaingia raundi ya pili na kucheza na mshindi wa mechi ya Kenya na Eritrea kati ya Juni 24-26 na kurudiana Julai 8 mpaka 10 na kama ikishinda itapata tiketi ya kucheza michezo ya Afrika mwezi Septemba huko Maputo.

Hata kwa wanawake Tanzania itaanza harakati za kufuzu katika raundi ya kwanza April 29 mpaka Mei 1 na kurudiana kati ya Mei 13-15 kwa kucheza na mshindi wa mechi kati ya Sudan na Kenya.

Nchi mbalimbali za Afrika katika kipindi hiki zipo katika maandalizi ya michezo tofauti kwa ajili ya kuhakikisha zinatwaa medali nyingi katika mashindano hayo, na zingine zinashiriki hivi sasa mashindano ya awali,lakini katika hali inayoshangaza Tanzania bado haijaingiza timu kambini kwa ajili ya maandalizi na wala hakuna dalili ya kufanya hivyo katika siku za hivi karibuni.

Mara kwa mara tumekuwa tukishuhudia maandalizi ya zimamoto wanayofanyiwa wanamichezo wetu kila mwaka inapobaki mwezi mmoja au wiki mbili kabla ya mashindano kuanza wakati tulikuwa na muda mrefu wa kuwafanyia maandalizi mazuri vijana wetu wanaoenda kuiwakilisha Tanzania.

Tunaamini Shirikisho la soka Tanzania TFF, lisipoiingiza timu yetu ya vijana kambini kwa ajili ya maandalizi na kuipatia mechi za kirafiki za kutosha itashindwa kufanya vizuri katika mechi za kufuzu na hivyo kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika katika upande wa soka.
 
Fomu ushiriki Big Brother 2011 zaanza kutolewa


na Andrew Chale


amka2.gif
KAMPUNI ya MultiChoice Tanzania kwa kushirikiana na M NET Africa, imeanza kutoa fomu za kushiriki shindano la Big Brother Africa msimu wa sita 2011, litakaloanza kufanyika Mei mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhusiano Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Barbra Kambogi, nchi 14 zitashiriki katika kinyang'anyiro cha kuwania dola 200,000 za Marekani katika shindano ambalo washiriki wake hukaa siku 91 ndani ya jumba hilo la BBA.
Watanzania wenye sifa za kushiriki shindano hilo wametakiwa kuwa na uwezo wa kujua lugha ya Kiingereza kwa ufasaha, kuanzia miaka 21 na kuendelea, sambamba na kuwa na hati ya kusafiria.
Sifa nyingine ni kuwa na kipaji binafsi, pamoja na kuweza kuishi na watu wa mataifa mengine ndani ya jumba hilo.
Taratibu za kuchukua fomu hizo tayari zimeanza kutolewa na mwisho wa kurejesha ni Februari 27 mwaka huu, makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 
k. Bilal kubariki tamasha la Wanyambo Dar


na Samia Mussa


amka2.gif
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal, kesho anatarajiwa kufungua tamasha la utamaduni wa Mtanzania linalowakilishwa na jamii ya Wanyambo kwa mwaka huu, ambalo limepangwa kufanyika kwa siku tatu mfululizo ndani ya Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tamasha la Wanyambo, Revelians Tuluhungwa, aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam jana.
Alisema, tamasha hilo litahusisha wasanii wa aina mbalimbali kutoka wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera, mabalozi, wasomi na viongozi wa serikali, sekta binafsi na wadau wa mambo ya utamaduni.
Alisema kuwa ili tamasha hilo liweze kufanikiwa, juhudi za Wanyambo wote waishio jijini Dar es Salaam zinahitajika, ambako wataungana na Wanyambo zaidi ya 200 waliowasili juzi na jana kutoka Karagwe na Kyerwa ambao wamekuja kuhudhuria tamasha hilo.
Tuluhungwa alisema ni mara ya kwanza kufanyika kwa tamasha hilo hapa jijini, ambako litategemewa kuwa kiungo muhimu kati ya Wanyambo washio Dar es Salaam na wilaya hizo.
Alitaja mambo mbalimbali yanayotarajiwa kufanyika siku hiyo kuwa ni pamoja na maonyesho ya ngoma za asili, vyakula vya asili vya kabila hilo, vinywaji, zana za asili, mila na desturi, nyumba za asili, kazi za mikono za Wanyambo, maandishi na methali za Kinyambo.
 
Mabalozi wa malaria watakiwa kubuni mbinu mpya


na Khadija Kalili


amka2.gif
WAZIRI wa Afya, Dk. Haji Mponda, ametoa rai kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao pia ni mabalozi wa mradi wa kupambana na ugonjwa wa malaria wa Zinduka, ‘Malaria No More' kutunga nyimbo zitakazoleta hamasa ya kubadili tabia iliyojengeka miongoni mwa jamii ya kuudharau ugonjwa huo.
Mponda alisema kwamba wasanii hao watafute njia mpya ya kusambaza ujumbe kutokana na tabia iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kudharau kujitibu malaria, ugonjwa ambao unaua kwa haraka zaidi hasa wanawake na watoto.
"Utaona mama anaona mtoto ana dalili zote za malaria, lakini atakachofanya ni kumpatia dawa za kutuliza maumivu na kuendelea na shughuli zake, kadhalika kwa vijana wenzenu, nao wanaoongoza kwa kudharau, utakuta mtu akijisikia ana dalili zote za malaria atapata kinywaji chake na kwenda zake, tofauti akiwa anasumbuliwa na magonjwa kama kaswende, hapo atajitibu kwa haraka zaidi," alisema waziri.
Wakati huo huo, Profesa Jay akizungumza kwa niaba ya wasanii wengine, alimwomba waziri kufanya nao kazi pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao, ombi lililokubaliwa.
Kundi hilo la mabalozi wa malaria ambalo lilikwenda kumtembelea waziri ofisini kwake jana, linaundwa na Profesa Jay, Lady Jaydee, Fid Q, Barnaba, Marlow, Mwasiti, Diamond, Amini, Banana na B Twelve.
 
Watanzania wapigwa changa la macho - Atletico kumbe magarasa


na alum Mkandemba


amka2.gif
ZIARA ya klabu ya soka ya Clube Atletico Paranaense ya Brazil kwa mechi za kirafiki dhidi ya klabu za Yanga na Simba za Dar es Salaam, imegubikwa na utata kutokana na waratibu wake kutotoa maelezo yanayotosheleza kuhusiana na kikosi kilichopo hapa nchini.
Tangu kuanza kutangazwa ziara ya timu hiyo hapa nchini iliyoratibiwa na Kampuni ya RBP Oil Industries, imekuwa ikielezwa kuwa ni mabingwa wa zamani wa nchi hiyo, huku ikidaiwa inashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi nchini kwao.
Lakini wakati timu hiyo ikiwa hapa nchini, ratiba ya Ligi Kuu nchini Brazil inaonyesha timu hiyo inaendelea na mechi zake za ligi huko Brazil ‘Serie A'.
Utafiti uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, siku ambayo klabu hiyo ya Paranaense ilipowasili nchini, kulikuwa na mechi dhidi ya Arapongas iliyochezwa kwenye uwanja wa nyumbani (wa Paranaense), wa Estádio Joaquim Américo Guimares na kuhudhuriwa na watazamaji 9,985 na kumalizika kwa Paranaense kulala 2-1.
Kama hiyo haitoshi, ratiba ya ligi hiyo ya ngazi ya juu zaidi nchini humo, inaonyesha kuwa jana Jumatano Januari 19, klabu hiyo ilikuwa ikichuana na Corinthians PR kwenye dimba la Estádio Janguito Malucelli, kabla ya Jumamosi Januari 22, kuwakaribisha Iraty kwenye dimba la nyumbani kwao katika mechi ya Serie A.
Utata zaidi juu ya ziara ya Atletico Paranaense, unatokana na waratibu wake kutoeleza kwa usahihi wakati wa ujio wa Wabrazil hao, juu ya kikosi kilichokuja nchini na kile kilichobaki Brazil, huku kikiorodhesha mataji yaliyotwaliwa na klabu ya wakubwa, kama sehemu ya mafanikio yake katika soka.
Waratibu hao wakayataja mafanikio ya timu ya wakubwa ya Paranaense, iliyotwaa ubingwa wa Serie A Brazil mara moja, Serie B Brazil mara moja na ubingwa wa Jimbo la Parana inakotoka mara 22, badala ya mataji yaliyobebwa na Vijana ya Dallas Cup mara mbili (2004 na 2005), na Winterthur Tournament mara mbili (1991 na 1992).
Katika kuthibitisha mkanganyiko huo, waratibu hao baada ya kuulizwa juu ya sakata hili, walikiri kuleta kikosi cha pili cha vijana (U-20), huku cha wakubwa kikiwajibika katika ligi ya nyumbani inayojumuisha timu 12, huku Paranaense wakishika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa ligi.
Lakini licha ya maelezo hayo, uchunguzi umebaini nyota wengi wanaounda kikosi kilichopo hapa nchini wana miaka zaidi ya 20, ambapo ni nyota wanane tu kati ya 19 waliotua nchini ndio walio chini ya umri huo.
Wachezaji 11 waliosalia, wanajumuisha nyota tisa waliofikisha na wanaokaribia kufikisha miaka 21, huku wawili wakiwa wanavuka miaka 20.
Kati ya walio na umri mkubwa katika kikosi hicho ni pamoja na mshambuliaji Jonatas Oliveira miaka 27 (amezaliwa Machi 30, 1983), huku kiungo Andres akiwa na miaka 22 (Amezaliwa Februari 7, 1989).
Waratibu wa ziara hiyo, pia wameongeza mkanganyiko zaidi baada ya kupanga kiingilio kikubwa, kinachofanana na kile ambacho Watanzania walikilalamikia katikati ya mwaka jana walipotakiwa kulipa kima cha juu cha shilingi 200,000 kuiona timu ya taifa ya Brazil ilipoumana kirafiki na Taifa Stars.
 
Wanachama Yanga wamvimbia Nchunga


na Juma Kasesa


amka2.gif
KATIKA hali inayoashiria kunukia kwa mgogoro mpya ndani ya klabu ya Yanga, wanachama wa klabu hiyo walioandaa mkutano wao leo na kupigwa ‘stop' na Mwenyekiti wake, Llyod Nchunga, wamesisitiza uko pale pale na bosi huyo hana mamlaka ya kuuzuia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga, Mohamedi Msumi, alisema wao kama wanachama wanayo haki kikatiba kuitisha mkutano huo na Nchunga hawezi kuwazuia kukutana kujadili masuala yanayohusu maslahi ya klabu hiyo.
Kauli ya Msumi inakuja siku moja, baada ya Nchunga kupinga kufanyika kwa mkutano huo, kwa madai ya uongozi wake upo katika maandalizi ya ushiriki wa timu hiyo katika Ligi Kuu na michuano ya kimataifa, hivyo uahirishwe mpaka utakapopangwa baadaye.
"Hawezi kutuzuia sisi tusikutane kwa masilahi ya Yanga, sisi tumemualika yeye na Kamati ya Utendaji waje wasikilize kile ambacho tumepanga kama ajenda ili wakakifanyie kazi, hivyo wakija wasije mkutano utafanyika," alisema Msumi.
Alisema moja ya agenda ambazo wamepanga kujadili ni vigezo vilivyotumika kumteua Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, kuwa miongoni mwa wadhamini na uhalali wa uanachama wake katika klabu hiyo na ushiriki wa Yanga katika mashindano mbalimbali.
Msumi alisema yeye kama Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga anawafahamu wanachama wote wa Yanga na matawi waliyotoka na suala la Mtemvu kuteuliwa katika nafasi hiyo wao hawalitambui, kwa kuwa si mwanachama wa Yanga wanayemfahamu.
"Tumewataka viongozi waje kwenye mkutano wa leo, kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya klabu lakini pia watueleze Mtemvu uanachama wa Yanga ameupata lini kwa kuwa sisi hatumtambui," alisema Msumi.
Alisema wadhamini wanaofahamika kikatiba ni mfadhili wao, Yusuf Manji, mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Fatma Karume na Francis Kifukwe, hivyo viongozi hao wanapaswa kuwaeleza wanachama kwa undani suala hilo, ili kuepusha miguno ambayo imeanza kujitokeza tangu mbunge huyo kuteuliwa.
Alisema mkutano huo pia utajadili kwa kina msuguano uliopo baina ya Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha, ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakilumbana kuhusiana na uendeshwaji wa klabu hiyo.
"Hatupendi kuona Yanga inarudi katika zama za migogoro na ndiyo maana tumepanga kukutana ili kujadili masuala mbalimbali ya klabu hiyo kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi ili kuhakikisha Yanga inainyang'anya Simba ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vema katika michuano ya kimataifa," alisema Msumi na kuongeza:
"Wanachama waje kwa wingi, mkutano upo na waachane na kauli ya Nchunga kwani Katiba ya Yanga ni halali na tumekuwa tukiuitisha miaka yote."



h.sep3.gif

 
Simba kuwafuata Wacomoro Jan. 26


na Dina Ismail


amka2.gif
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ya jijini Dar es Salaam wanatarajiwa kuondoka nchini Januari 26 kwenda nchini Comoro kwa ajili ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Elan de ya huko.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, kikosi cha Simba kilitarajiwa kuingia kambini rasmi jana jioni katika Hoteli ya Lamada iliyopo jijini Dar es Salaam tayari kujiweka sawa na michuano hiyo na ile ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.
Simba imekuwa katika maandalizi ya michuano hiyo tangu mwishoni mwa mwaka jana, ilipokwenda kuweka kambi visiwani Zanzibar, sambamba na kucheza mechi kadhaa za kirafiki na timu za ndani na nje ya nchi.
Aidha, katika maandalizi yake, Simba ilishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani humo iliyofikia tamati Januari 12 na kufanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga kwa mabao 2-0.
Mabingwa hao wa Bara, iwapo watawatoa Wacomoro hao watakutana na vigogo vya soka barani Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika hatua nyingine, Simba leo inatarajiwa kushuka katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu inayodaiwa kuchakachuliwa ya vijana wanaodaiwa kuwa ni U-20 wa Atletico Paranaense ya nchini Brazil.


h.sep3.gif


juu
 
Masumbuko, Kavina kukimbia Mali


na Samia Mussa


amka2.gif
WANARIADHA wawili wa Tanzania wanatarajiwa kushiriki mbio za kimataifa za Bank of Africa (BOA), zitakazorindima Bamako nchini Mali Januari 23 mwaka huu.
Wanariadha hao Masumbuko Paul na Sarah Kavina, jana walikabidhiwa bendera na tiketi tayari kwa safari hiyo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Katika mashindano hayo, Masumbuko atakimbia marathoni kamili kilomita 42 huku Kavina akikimbia mbio za kilomita 10.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa BOA Tanzania, Kobby Andah, alisema anaamini kupitia ushiriki wa wanariadha hao katika mashindano hayo, Tanzania itaweza kujitangaza kimataifa.
Wanariadha hao wanatarajiwa kuondoka nchini kesho wakiwa na kocha wao Shaaban Hiki na watarejea Januari 26 mwaka huu.
Mashindano hayo yameanza miaka mitatu iliyopita na kudhaminiwa na benki hiyo na yameweza kuvutia wanariadha 20 kutoka nchi zipatazo 10 za Afrika, huku Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza mwaka huu.
 
Mbunge Ilemela aahidi ligi ya soka


na Sitta Tumma, Mwanza


amka2.gif
KATIKA kuinua michezo, Mbunge wa Ilemela, jijini Mwanza Highness Kiwia (CHADEMA), ameahidi kuanzisha ligi ya soka jimboni humo, lengo likiwa ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana na hatimaye kuwa wachezaji wa kimataifa.
Akiwahutubia mamia ya wananchi katika mkutano wake wa kuwashukuru, uliofanyika Igombe Kata ya Bugogwa juzi, Kiwia alisema, katika mikakati yake ndani ya miaka mitano ijayo, atahakikisha vijana wa Wilaya na jimbo lake hilo, wanashiriki michezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwashindanisha na wenzao wa majimbo mengine likiwemo la Nyamagana.
"Nipo kwenye mpango wa kuanzisha ligi ya Ilemela, ili kutoa fursa kwa vijana wetu kushiriki michezo na hatimaye kuwa wachezaji tegemeo wa kimataifa," aliahidi mbunge huyo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, sekta ya michezo inapaswa kuboreshwa na kwamba, moja ya dira na mipango yake ndani ya miaka mitano ijayo ni kuona jimbo lake hilo linang'ara kwa michezo na kuwa tishio kwa timu za jiji, mkoa na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, aliwaahidi vijana na wanachi hao wa Ilemela kwamba, kamwe hawezi kurudi nyuma katika kutekeleza ahadi zake hizo za uboreshaji wa michezo na kuhoji: "Nikianzisha hii ligi mtaifunga timu ya Nyamagana kwa Wenje? Msiniangushe vijana wenzangu."
 
Yanga hapakaliki

Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 20th January 2011 @ 09:16

YANGA bado hapakaliki na wala hakunogi baada ya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo na wazee kuja juu na kuhoji mahali inapopelekwa timu yao wakidai kuwa wanaingizwa kwenye siasa.

Kwa muda mrefu sasa, ndani ya Yanga mambo yamekuwa hayaeleweki kutokana na sababu mbalimbali ndani ya uongozi wa klabu hiyo kongwe yenye maskani yake mtaa wa Twiga na Jangwani Kariakoo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini baadhi ya wanachama hao na wazee wa Yanga walisema kuwa klabu yao sasa inaingizwa kwenye masuala ya siasa kitu ambacho wao hawakitaki kwa vile si malengo ya klabu hiyo.

"Klabu yetu inaenda wapi, tumesikia kwamba mfadhili (Yusuf Manji) amemteua Mtemvu (Abbas) kuwa mmoja wa wadhamini, hilo limepitishwa na nani?"

"Mbali na hilo, lakini pia tunasikia kwamba kuna wanasiasa wengine anataka kuwaingiza kwenye safu ya udhamini ya Yanga, jamani tumefikia hatua hiyo kweli,"alisema mwanachama mmoja ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa Yanga.

Alisema kwa anavyofahamu, suala la mdhamini wa Yanga ni lazima achaguliwe na Kamati ya Utendaji na pia mkutano mkuu ulipitishe jina lake lakini mambo si kama yanavyokwenda sasa Yanga.

"Huyo Manji mwenyewe mpaka sasa mkutano mkuu haujampitisha bado, halafu yeye analeta watu wengine, tena bila Kamati ya Utendaji kuamua wala mkutano mkuu, hapana hili sasa halikubaliki,"alisema.

Akizungumza na gazeti hili jana, mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji ya Yanga alikiri kuwa uamuzi wa kumpatia Mtemvu udhamini haukufikishwa katika Kamati yao na wao pia wanashangaa kitendo cha mdhamini wao huyo.

"Ni kweli wanavyosema hao wanachama wala si uongo, tunatakiwa tuamue Kamati ya Utendaji, kisha tupeleke jina hilo kwenye mkutano mkuu wa wanachama nao walipitishe, hivi ninavyokwambia hata wenyewe hatuelewi hali inakuwa vipi".

"Kwanza hata yeye mwenyewe, ( Manji) uteuzi wake haukupitishwa kwenye mkutano wa wanachama bali kiongozi mmoja tu katika uongozi uliopita (anamtaja jina) alimteua basi,"alisema.

Habari zaidi zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilidai kuwa jana kulikuwa na kikao kati ya wazee na Manji kikao ambacho kilichukua muda mrefu na kilikuwa na mabishano ya hapa na pale.

"Lakini sisi Kamati ya Utendaji tutakutana leo jioni (jana), hapo ndipo zitakapojulikana mbichi na mbivu, tunataka tujue mustakabali wa klabu, haiwezekani watu wengine waingie watuendeshe wanavyotaka wao, kama ni hivyo kusiwe na uongozi basi, kama kila kitu anafanya mdhamini,"alisema.
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom