Simba yatuma salamu Mazembe Sunday, 13 February 2011 21:22
Mshambuliaji wa timu ya Simba, Mussa Hassan Mgosi akijaribu kuwatoka mabeki wa timu ya Elan, Yousouf Ali Mohamed na Mohamoud Mohamed wakati wa mechi ya marudiano ya Kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana/Picha na Jackson Odoyo.
Sostenes Nyoni
WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, Simba jana waliichapa Elan de Mitsoudje ya Comoro mabao 4-2 katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo Simba itakutana na TP Mazembe ambao ni mabingwa DR Congo na mabingwa wa Afrika katika raundi ya pili ya mashindano hayo kati ya tarehe 18,19,20 mwezi Machi na kurudiana kati ya tarehe 01,02,03 mwezi Aprili 2011.Katika mechi ya jana mpira ulianza kwa kasi huku safu ya ulinzi ya Simba ikiwa chini ya Kelvin Yondani, Juma Nyoso, Haruna Shamte na Juma Jabu, ambapo katika dakika ya sita Simba ilipata faulo baada ya mshambuliaji wake Mbwana Samata kuchezewa rafu nje kidogo ya 18, lakini Mussa Hassan Mgosi alipiga mkwaju dhaifu ulioenda nje.
Mgosi katika dakika ya nane pia aliwalamba chenga mabeki wa Elan de Mitsoudje ya Comoro pembeni ya uwanja na kupiga krosi nzuri, lakini Mbwana Samata akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga aliukosa mpira.
Winga wa kushoto wa Elan, Mohamed Mouien nae alikuwa akiwasumbua mabeki wa Simba, lakini krosi zake nyingi zilikuwa hazitumiwi vizuri na washambuliaji wa timu yake ambao ni Moustackina na mwenzake Madaha Mohamed.
Katika dakika ya 30 Madaha Mohamed wa Elan alikosa bao akiwa yeye na Kaseja baada ya kupiga mpira uliotua mikononi mwa Kaseja.
Madaha Mohamed alirekebisha makosa yake na kuipatia timu yake bao la kuongoza dakika ya 41 baada ya kuchomoka na mpira winga ya kulia na kumchambua kipa Juma Kaseja kwa kupiga shuti kali upande wa kushoto huku mabeki wa Simba wakidhani Madaha alikuwa ameotea.
Kabla ya kwenda mapumziko Mbwana Samata aliisawazishia Simba bao katika dakika ya 44 baada ya kupiga krosi ambayo ilimshinda kipa wa Elan, Youssouf Ahamada ambaye katika jitihada za kuuokoa mpira ule alijikuta akiutumbikiza wavuni.
Mpaka mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.
Simba katika kipindi cha kwanza walikosa mabao mengi kutokana na washambuliaji wake Mbwana Samata, Musa Mgosi na Ally Mohamed Shiboli kutokuwa makini.
Kipindi cha pili kilianza huku Simba wakipeleka mashambulizi katika lango la Elan, ambapo katika dakika ya 48 Simba walipata bao la pili ambalo lililofungwa na Patrick Ochan baada ya Mbwana Samata kupiga krosi iliyomgonga Ochan tumboni na katika jitihada za walinzi na kipa wa Elan kutaka kuokoa mpira huo walijikuta wakijichanganya na kuuacha mpira ukitinga wavuni.
Katika dakika ya 53 kocha wa Simba, Patrick Phiri alimtoa Mohamed Banka na kumuingiza Jerry Santo mabadiliko ambayo yalisaidia kuimarisha safu ya kiungo.
Kama haitoshi mshambuliaji Mbwana Samata aliiongezea Simba bao la tatu katika dakika ya 56 kwa shuti kali la umbali kama mita 30, bao hilo lilitokana na faulo aliyokuwa amefanyiwa Patrick Ochan.
Kocha wa Elan, Youssof Bachiro alifanya mabadiliko katika kikosi chake dakika ya 58 baada ya kumtoa kipa wake Youssouf Ahamada na kumuingiza Mohamed Hassan.
Baada ya mabadiliko hayo, Elan ilipata bao la pili katika dakika ya 63 ambalo lilifungwa na Abdoulhouda Abdouleafor.
Pia timu zote mbili zilifanya tena mabadiliko kwa wachezaji wao, ambapo Elan ilimtoa Madaha Mohamed na kumuingiza Zaidou Soilihi wakati Simba ilimtoa Ally Shiboli na nafasi yake ilichukuliwa na Amri Kiemba.
Mabadiliko hayo yalionekana kuinufaisha Simba kwa sababu katika dakika ya 72 Amri Kiemba ambaye alitokea benchi aliipatia Simba bao la nne akipokea pasi kutoka kwa Haruna Shamte.
Katika dakika ya 88 kocha Phiri alimtoa Rashid Gumbo na kumuingiza Salum Aziz.
Pambano hilo lilichelewa kuanza baada ya mwamuzi Issa Kagabo kutoka Rwanda kugoma kwenda kuanzisha pambano hilo kwa sababu wachezaji wanne wa Simba walikuwa hawana hati za kusafiria.
Baada ya suala hilo kupatiwa ufumbuzi kwa makubaliano ya wachezaji hao kupigwa picha, timu ziliingia uwanjani na muamuzi alianzisha pambano hilo.
Akizungumza mara baada ya mechi kumalizika kocha wa Simba, Patrick Phiri aliwashukuru mashabiki kwa ushangiliaji wao mkubwa katika dakika 90 za mchezo, pia aliwatetea wachezaji wake kwa kukosa mabao akisema ilitokana na umuhimu wa mechi yenyewe.
Mashabiki ni wengi waliojitokeza kushuhudia pambano hilo, suala lingine ni kwamba ilibidi gari litumike kunyonya maji yaliyokuwa yametuama uwanjani kutokana na mvua zilizonyesha jana mchana.
Katika pambano hilo la jana rais wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF, Leodeger Tenga alihudhuria, pia alikuwepo kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Polsen pamoja na Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Profesa Juma Kapuya.
MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Simba, jana walifanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwang'oa Elan Club ya mjini Mitsoudje, Comoro, kwa jumla ya mabao 4-2. Ushindi huo wa jumla kwa Simba unatokana na timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Mitsoudje, Comoro. Kwetu Tanzania Daima, tukiwa sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo, tunawapongeza wachezaji, benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Phiri na viongozi kwa mafanikio hayo ambayo kwa hakika hayakupatika kirahisi. Tofauti na ilivyotarajiwa, licha ya kung'olewa katika michuano hiyo, timu ya Elan Club imeweza kuonyesha uwezo mkubwa kiuchezaji kuanzia mechi ya kwanza wakiwa kwao hadi ya jana hata kuwalazimu Simba kufanya kazi ya ziada hadi kupata ushindi. Tunaipongeza Simba kwa mafanikio haya hasa tukizingatia ni siku moja tu tangu wawakilishi wengine katika michuano ya kimataifa kutoka bara, Yanga imetupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Africa (Caf). Yanga ambayo ilianza kutoka sare ya mabao 4-4 katika mechi ya nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita, juzi ikicheza mechi ya marudiano mjini Addis Ababa, ilikubali kipigo cha mabao 2-0, hivyo kuaga kwa jumla ya mabao 6-4. Pamoja na pongezi zetu kwa Simba, pia tunatoa wito kwa viongozi, makocha na wachezaji wa timu hiyo kutobweteka na ushindi huo kwani kibarua kigumu kinakuja mbele ya safari ambapo watakwaana na mabingwa mara mbili mfululizo wa michuano hiyo, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. TP Mazembe walio chini ya kocha wake Lamine N'Diaye, wao wataanzia raundi hiyo ya kwanza wakitaka kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mara mbili: 2009 na 2010. Kwa vile Rais wa TP Mazembe, Moses Katumbi Chapwe, ametamka kuwa lengo ni kutwaa taji la tatu kisha kucheza na kubeba taji la Klabu Bingwa ya Dunia, Simba hawana budi kufanya maandalizi ya uhakika kabla ya kukutana na wakali hao. Kwa mujibu wa ratiba ya mechi hizo za kimataifa, mechi ya kwanza kati ya Simba na TP Mazembe, itapigwa kati ya Machi 18 na 20 kabla ya kurudiana kati ya April 1 na 3, hivyo kabla ya mechi hiyo ya kwanza, Simba wafanye maandalizi ya uhakika. Tunaamini, licha ya ubora wa kikosi na mipango ya uongozi wa TP Mazembe katika kuelekea kampeni hizo, kama Simba watafanya maandalizi ya uhakika wanayo nafasi ya kufanya maajabu kama ya mwaka 2003, walipowang'oa waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Zamalek. Kama Simba chini ya Kocha James Siang'a iliweza kuwang'oa Zamalek, kwa nini ishindwe kufanya hivyo kwa TP Mazembe kama kweli kutakuwa na juhudi za pamoja katika kupigania mafanikio ya timu? Maandalizi ambayo tunamaanisha hapa, ni timu kwenda kambini mapema huku ikijifua kwa mechi za kirafiki na timu kubwa ikiwezekana kutoka nje ya nchi ili kuwajengea wachezaji hali ya kujiamini kabla ya kukutana na TP Mazembe. Jukumu ambalo linamkabili Kocha Phiri na benchi lake la ufundi na viongozi wa Simba kwa ujumla, ni kuhakikisha wachezaji wanapata mechi za kirafiki za kimataifa za kutosha kabla ya kuwafuata TP Mazembe kwa mechi ya kwanza ambayo itachezwa mjini Lubumbashi. Kama Simba watafanikiwa kuwabana TP Mazembe kwa kutoka nao sare ya aina yoyote katika mechi hiyo ya ugenini, watakuwa wamejiweka katika nafasi nzuri kuelekea mechi ya marudiano ambayo itapigwa jijini Dar es Salaam kati ya Aprili 1 na 3. Tunamaliza maoni haya kwa kuwapongeza wachezaji, makocha na viongozi wa Simba kwa kufanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mafanikio haya yawe chachu ya kujipanga zaidi kabla ya kuwakabili TP Mazembe.
KWA yakini, faida ya kipato na maslahi mazuri kwa ujumla katika mchezo wowote ule hapa duniani, ndio tarajio kuu na la kwanza kabisa kwa mchezaji wa mchezo husika. Hii ni kwa sababu, pamoja na kuwa michezo ni burudani, lakini pia ni kazi inayotegemewa na wachezaji wetu katika kujikimu kimaisha wao pamoja na wawategemeao. Kwenye michezo mingi hapa nchini, wachezaji wamekuwa wakipongeza jitihada na hatua za makusudi za wadau katika kuhakikisha michezo hiyo inapiga hatua. Wanafahamu kama wengi tunavyofahamu kuwa kukua kwa michezo hiyo, kimsingi ndiyo pia kukwamuka kimaisha na ndio kupanuka kwa wigo wa pato lao. Lakini, hali imeonekana ni tofauti kwa upande wa mchezo wa ngumi, masumbwi ama vyovyote unavyoweza kuuita, licha ya kuwa ni kati ya michezo yenye mashabiki, wapenzi pamoja na wadau wengi zaidi nchini. Kelele nyingi zilishapigwa na wachezaji wa ndondi juu ya uduni wa maslahi yao ukilinganisha na ugumu wa mchezo huo na mazingira yake yanayouzunguka. Wanaotupiwa zaidi zigo zito na kubwa la lawama ya kufanya hali ya maisha kwa mabondia kuendelea kuwa ngumu na tatanishi ni mapromota wao. Inadaiwa kuwa mapromota wamekuwa wakiwabana zaidi mabondia kwa kuwalipa pesa kiduchu katika mapambano wanayoyaandaa. Aidha, hutokea wakati mwingine kuwadhulumu kwa ama kuwakata bila sababu malipo waliyoahidiana, au kutowalipa kabisa na kuwakimbia. Katika hili, binafsi naungana na mabondia katika kulitupa zigo la lawama kwa baadhi ya mapromota wanaokosa uungwana na kulitia doa jina hili. Kwa sababu, nilishashuhudia pambano likiandaliwa huku promota akiahidi kuwalipa vema mabondia anaowapiganisha, lakini mwisho wa siku akatokomea kizani bila kutekeleza makubaliano. Najiuliza sipati jibu, nini sababu kubwa ya mapromota kuamua kuwafanyia hivi mabondia wetu wanaopigana kwa maslahi yao, jamii na taifa kwa ujumla? Ni uroho na tamaa ya pesa? Kutokuwajali na kuthamini ipasavyo mchango wao? Ama udhaifu wao wa kutosimamia na kufuatilia haki zao za msingi? Kwa sababu hata pale inapotokea mabondia kulipwa bila utata kwenye mapambano wanayopiganishwa, basi malipo huwa ni tofauti na kazi yenyewe. Hivi kweli kwa mchakato huu, mchezo wa ngumi unaweza kupiga hatua, kufika mbali na mabondia kuneemeka kama ilivyo kwa nchi za wenzetu? Kingine ambacho kiukweli kinanipasua kichwa kwa kadri ninavyofikiria, ni hali ya ukimya iliotawala kwa upande wa vyama husika vya mchezo huo. Hata serikali kupitia wizara yenye dhamana, imeonekana ni kama vile imelala usingizi wa pono na kuwapa mwanya mapromota uchwara, kuzidi kuwanyonya mabondia watakavyo. Kwani kilio hiki cha mabondia kuhusiana na kudhulumiwa na kutotekelezwa kwa mikataba wanayoingia na mapromota, kimekuwa ni kama wimbo wa taifa hivi sasa. Sisi wapenzi na mashabiki wa mchezo huo tulipenda kuona maslahi ya wachezaji wetu yakiboreshwa ili kuwatia moyo na kuwajaza ari ya kufanya vema zaidi. Suala la kuboreshwa kwa haki na maslahi ya mabondia ni jambo linaloweza kuwafanya wengi wavutike kuingia katika ndondi na kuongeza idadi ya wawakilishi wa mchezo huo ngazi ya kimataifa. Kwa sababu, kama nilivyotangulia kusema hapo juu, pamoja na kuwa michezo ni burudani, lakini pia ni kazi hivyo hakuna atakayekuwa tayari kufanya kazi isiyo na tija stahiki. Kwa kumalizia niwasihi mabondia wa mchezo huu nchini, kutokatishwa tamaa na ugumu wanaokumbana nao katika mchezo huo waliojitoa kuutumikia, badala yake wasimame imara katika kuziba mianya inayowaacha na kilio cha kudhulumiwa kila uchao. Wajipange kuvibana vyama na mapromota wasiowajibika ipasavyo, wahakikishe wanatumia kichache wanachokipata katika kufanya maandalizi sahihi kila wanapokabiliwa na pambano, huku wakifanyia uchunguzi afya zao ili kutojiweka kwenye mazingira hatarishi wawapo ulingoni. Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki mabondia wentu Mungu wabariki wanamichezo wote kwa ujumla. Amin.
‘Manji kama huna unachopoteza okoa damu isimwagike Jangwani'
Mwandishi wetu
NI Jumatatu nyingine tena tunakutana wadau wa safu hii ya Uwanja wa Kuchonga , ili kupena changamoto lengo likiwa kuleta ufanisi katika kusukuma mbele gurudumu hili la maendeleo katika sekta nyeti ya michezo. Kabla hatujapeana dondoo za wiki iliyopita, kwa nawatakia maadhimisho mema ya siku hii ya Wapendao, ‘Valentine Day', nawapenda nyote. Bila shaka mu wazima wa afya na mnaendelea vema na majukumu ya ujenzi wa Taifa, ila kwa wale ambao hali zao ni tete, tunawaombea nafuu. Baada ya kujuliana hali, wapenzo wasomaji wa safu hii, kama tulikuwa pamoja mtakumbuka wiki iliyopita tulijadili mada isemayo, ‘Katika hili Wana Yanga mweleweni Davis Mosha. Katika mada hiyo tuliiangalia hali ya mtafaruku ambayo imeiguka klabu kongwe ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kwa takribani mwezi mmoja na nusu sasa, ambako umezidi kuchukua sura mpya kila kukicha. Yameshuhudiwa mengi katika klabu hiyo ndani ya muda huo mfupi wa misigano, ikiwamo baadhi ya viongozi kuachia ngazi na sasa kinachotwala ni vurugu za kuwapiga viongozi na wachezaji pale matokeo ya uwanjani yanapokuwa sio mazuri. Tulieleza kuwa, kimsingi mitafaruku hii ndani ya Yanga ilianza na kugawanyika katika makundi makuu mawili, moja likiwa la Mfadhili na mjumbe wa bodi ya wadhamini, Yussuf Manji akiwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga huku mwingine ukiwa wa viongozi wengine wa Kamati ya Utendaji wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Davis Mosha. Wakati hali ya mtafaruku huo ikizidi kuchukua sura mpya, ndipo lilipotokea sakata la kupigwa kwa wachezaji na viongozi ambako Makamu Mwenyekiti Mosha siku ya mechi dhidi ya Mtibwa ambako Yanga ililala 1-0. Kutokana na hali hiyo, Mosha alifungua jalada kituo cha Polisi Chang'ombe kuhusiana na tukio hilo, akiwatuhumu watu kadhaa kuhusiana na tukio hilo, ambako baadhi yao walokamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi. Lakini wakati hali ikiwa hivyo, Mosha kwa moyo wa kiungwana na kiuna michezo na kwa maslahi ya klabu ya Yanga, alifikia uamuzi wa kumsamehe kijana aliyeongoza uharibifu wa gari lake, baada ya mtuhumiwa kukiri na kuomba msamaha. Pili Mosha alifanya kazi ya ziada, lengo likiwa ni kuiona Yanga moja yenye amani, kwenda kukutana na kundi hilo la Wanachama ambalo limekuwa likiendesha kampeni za kumchafua na kumpinga, kuzungumza nao kwa kina kuhusiana na hayo wanayomtuhumu. Kutokana na hatua hiyo ya Mosha, kwa yeyote mwelewa na mpenda michezo, tulihimiza anapaswa kumuelewa kiongozi huyo na kumuunga mkono kwa lengo la kuleta amani, umoja na mshikamano ndani ya klabu, jambo ambalo ni nguzo kuu ya maendeleo katika klabu hiyo kongwe hapa nchini. Baada ya dondoo hizo za wiki iliyopita, turejee katika mada yetu ya leo, ambako kimsingi bado tuko Jangwani ambako bado hali ni tete. Jangwani mambo bado hayajatulia na jambo la kunyong'onyeza ni mwenendo usioridhisha ndani ya klabu na timu, ambako mbali ya kusua sua katika mechi zake za Ligi Kuu bara, Jumamosi iliyopita imeshuhudiwa ikiiaga michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), kwa kuondolewa kwa jumla ya mabao 6-4 na Dedebit ya Ethiopia. Lengo si kuzungumzia matokeo hayo ya Kombe la Shirikisho, bali leo ni kuwataka Wana Yanga wakae chini na kujiuliza nini chanzo cha matatizo haya na nini mwisho wake. Kimsingi kuna wanachama wa Yanga ambao wako mstari wa mbele kuanzisha vurugu kwa madai ya uchungu na klabu yao, lakini kimsingi hawakijui hata hicho wanachojidai kukipigania na nini faida zake. Hivyo Wana Yanga badilikeni na mjiulize, tangu kufanikiwa kuzikwa kwa makundi yale yaliyoiandama kwa miaka kadhaa, yakiwemo yale ya Asili, Kampuni, Academia na mengineyo. Kuzimika kwa makundi hayo kama sio kusinzia, kuliwezeshwa kwa mchango mkubwa wa mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Yussif Manji ambaye leo hii ni mdhamini na mfadhili wa klabu hiyo. Bila shaka, pamoja na hayo aliyoyafanikisha Manji na mengineyo ndani ya klabu hiyo, ndiko kulikosukuma apendekezwe kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo. Lakini Wana Yanga wanapaswa kujiuliza, inakuwaje leo hii baada ya kazi kubwa ya kuyazimisha makundi yale, kumekuwa na moshi ukifukuta chini kwa chini mara kwa mara. Ukianza na uongozi mpya uliongia madarakani baada ya muafaka ule, chini ya Mwenyekiti Imani Madega, ndani ya muda mchache ulizuka mtafaruku na hata kutishia kufanyika mapinduzi ya kumng'oa Mwenyekiti huyo madarakani. Chanzo cha kutaka kumng'oa Madega madarakani ilikuwa ni kupishana na mfadhili Manji, lakini Mwenyekiti huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria alipigana kufa na kupona na kuzuia harakati hizo na hatimaye kubaki madarakani. Lakini hivi karibuni tangu kuingia kwa uongozi mpya chini ya Lloyd Nchunga Julai 18 mwaka jana, hivi sasa nao umegubikwa na hali ya mitafaruku na Manji ni mhusika mkuu tena katika hali hii. Kama ambavyo tumewahi kuhoji katika moja ya mada zetu hapa Uwanjani; Wana Yanga jiulizeni kwa nini Manji? Leo kwa heshima na taadhimima tunapenda kumwambia mfadhili huyo; Kama hana anachopoteza Yanga aokoe damu isimwagike Jangwani. Kimsingi hali hii iliyoko Yanga hivi sasa, Manji ni mhusika mkuu, hivyo kama kweli ana nia njema na Yanga na hana anachopoteza, basi akae pembeni awaachie wanachama waweke sawa mambo yao kwa mujibu wa katiba yao, hasa pale ambako wanaona kuna dosari na mfadhili huyo ndio chanzo. Kimsingi Manji kama akiamua, anaweza kuisaidia Yanga hata bila kuwa kiongozi, lakini vinginevyo kwa hali hii inayoendelea hata viongozi wabadilishwe kila siku, lakini Manji akiendelea kuwepo kama ambavyo yuko hivi sasa katika klabu hiyo, hawataendana. Ni wazi wanachama wanaohoji juu ya uwepo na utendaji wa Manji ndani ya Yanga wana hoja na ndio chanzo cha mgogoro, kwani wale waamini wa mfadhili huyo ni vigumu kuiva chungu kimoja. Hapa wahusika wanapaswa kupaelewa, si lengo la kumuondoa Manji Yanga, bali lengo ni kusaka suluhu ya kudumu ndani ya klabu hiyo kuliko hali ilivyo hivi sasa. Mfano, hivi Manji asingefanya uteuzi wa Mbunge Abbas Mtemvu kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini, mamlaka ambayo hana kabisa kikatiba, hoja ya wanachama wa Yanga kumpinga kwa hilo ingetoka wapi. Sidhani kama Manji angekuwa amesimama kama mfadhili bola kuingilia masuala ya utendaji ya klabu, hao wanaohoji mambo anayoyaamua ndani ya Yanga wangetoka wapi? Kutokana na hali hiyo ndio maana wadau wa uwanja wa kuchonga tumesukumwa kulisemea hili; ‘Manji kama huna unachopoteza okoa damu isimwagike Jangwani'. Lakini hili likipuuzwa, tukae mjkao wa kula kukinga damu za Wana Yanga ambazo hivi sasa ‘zinabib' kumwagika. Mungu ibariki Yanga Afrika, Mungu libariki soka la Bongo. Kila la heri, tukutane wiki ijayo.
KAMATI ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka la Aprili 24 chini ya Mwenyekiti wake, Alex Msama, imepanga kutumia sehemu ya fedha itakayopatikana katika siku hiyo, kuwasomesha watoto yatima na kuwapa mitaji ya biashara kina mama wajane. Wengi wamejitokeza kusifu hatua ya kamati hiyo kwa kusema inaonyesha kwa jinsi gani Msama na kamati yake inavyojali makundi yenye mahitaji maalumu kama hayo katika jamii. Kwa upande wake Waziri wa Afrika Mashariki na Mbunge wa Urambo kwa tiketi ya CCM, Samuel Sitta, amempongeza na kuongeza anaamini kamati hiyo itatimiza ahadi yake kwa maslahi ya walengwa. Kauli ya Sitta, inatokana na maudhui ya tamasha hilo la Pasaka litakalofanyika siku hiyo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, kutumia sehemu ya fedha, kusaidia yatima na wajane. Kwa mujibu wa Msama, mbali ya kusomesha watoto yatima kwa lengo la kuwapatia elimu ambao ni urithi bora kwao, fedha hizo pia zitawasaidia wanawake wajane kwa kuwapa fedha za kuanzisha biashara. Waziri Sitta ambaye amekuwa akishirikiana kwa karibu na Msama katika kusaidia makundi hayo yenye mahitaji maalumu, amesema jitihada zinazofanywa na Msama ni mfano wa kuigwa. "Nimeguswa na kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na Msama, zimekuwa msaada kweli kwa vijana wengi hapa nchini, kwani anaisaidia jamii
kwa mapenzi kutoka moyoni," alisema Sitta aliyewahi kuwa mgeni rasmi katika tamasha la mwaka 2009 na kuongeza: "Kama wangejitokeza vijana wengine kama Msama, naamini kabisa jamii yetu ingekuwa inapata misaada mingi kwani ni huduma ambayo imekuwa faraja na msaada kwa wengi, nampongeza sana." Alisema amewahi kushuhudia walemavu wakinunuliwa baiskeli, watoto yatima wakisomeshwa achilia wajane kusaidiwa mitaji ya biashara kupitia kile kilichopatikana kupitia matamasha ya Pasaka yaliyotangulia. Sitta anaongeza kuwa kwa kiasi kikubwa tamasha hilo pia litasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kwani wengi hivi sasa wameamua kujikita katika muziki wa Injili kwa ajili ya kumuimbia Mungu na kujipatia kipato. Alisema, mbali ya matamasha hayo kuwezesha wananchi kupata mafunzo ya neno la Mungu kupitia ujumbe wa nyimbo mbalimbali ambazo huimbwa na waimbaji, pia uimbaji ni moja ya ajira kwa vijana. "Unapokuwa na watu wenye uzalendo kama Msama Promotion kwa hakika kabisa vijana wengi watajitokeza na watahamasika kujiingiza katika muziki huu, kwani watakuwa na uhakika wa kujipatia kipato," alisema Sitta. Wakati huo huo mbunge wa viti maalumu kupitia chama cha Mapinduzi mkoani Mbeya, Mary Mwanjela, naye amejitokeza kumpongeza Msama kwa kuandaa tamasha hilo kwa kusema ni lenye manufaa makubwa kwa jamii. Pongezi za viongozi hao zimeungana na nyingine ambazo zilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Sera na Uratibu katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, Phillip Marmo. Marmo aliyewahi kuwa mgeni rasmi katika tamasha la 2008, alisema tamasha la Pasaka, ni kielelezo cha upendo wa dhati kwa wenye mahitaji maalumu. Kwa upande wake, Msama ameshukuru kwa pongezi hizo na kusema atajitahidi kumwomba Mungu amjalie uzima, afya na moyo wa kutimiza ahadi na malengo aliyojiwekea katika kusaidia wengi kwa kidogo anachojaaliwa na Mungu. Mwenyezi Mungu wa ajabu kabisa, unaweza kuwa na uwezo mdogo, lakini kama utaguswa kutoa, fanya hivyo kwa sababu Mungu atakurudishia mara dufu, hivyo nitazidi kusaidia wengi kwa njia hii kwa kadiri nitakavyojaaliwa," alisema Msama. Msama ambaye ni mwasisi wa matamasha ya Injili nchini hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki huo, amesisitiza tamasha la mwaka huu litakuwa na utofauti mkubwa ikilinganishwa na yaliyopita. Mbali ya Sitta na Marmo, viongozi wengine ambao wamewahi kuwa wageni rasmi katika matamasha ya Injili ambao Msama anawaweka kwenye kundi la watu maalumu waliosaidia kukua kwa muziki wa Injili ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi (2000). Katika tamasha la mwaka 2001, mgeni rasmi alikuwa ni Mchungaji wa Kanisa la Mikocheni Assemblies of God, Dk. Getrude Rwakatare. Mwaka 2002, alikuwa Makamu wa Rais wa Awamu ya Tatu, Dk. Omari Ali Juma, na mwaka 2003, alikuwa mzee Wiso. Mwaka 2004, akawa mwakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN) nchini na mwaka 2005, alimwalika Rais Benjamini Mkapa, ambaye hata hivyo aliwakilishwa na Waziri Jumanne Maghembe. Mwaka 2006, mgeni alikuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Abraham Mengi na mwaka 2007, akawa Mama Salma Kikwete. Katika tamasha la mwaka 2008, mgeni rasmi alikuwa ni Philipo Marmo, wakati huo akiwa Waziri Ofisi ya Rais-Sera na Uratibu wa Bunge. Mwaka 2009, mgeni akawa aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, ambaye sasa ni Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mwaka 2010, kamati yake ilichukua maamuzi magumu ya kupeleka tamasha hilo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa: Shinyanga, Mwanza na Mara. Anasema kwa mwaka huu, baada ya tamasha hilo la Diamond Jubilee hapo Aprili 24, siku itakayofuata yaani Aprili 25, mashambulizi yatahamia Shinyanga kabla ya kwenda CCM Kirumba, jijini Mwanza hapo Aprili 26.
SAFARI ya timu ya Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imeishia mikononi mwa Dedebit ya Ethiopia, timu iliyoasisiwa Oktoba 31, mwaka 1998 kwenye viunga vya Jiji la Addis Ababa kama timu ya vijana wadogo. Wakiwa na msimu wa kwanza katika Ligi Kuu ya Ethiopia, mwaka 2010 walifanikiwa kumaliza ligi wakiwa nafasi ya pili nyuma ya wakongwe St. George, hivyo kujitwalia tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho. Mbali ya kumaliza nafasi ya pili, Dedebit chini ya rais wake Kanali Awel Abdurahim, ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa kuwafunga St. George. Ikicheza mechi yao ya kwanza ya kimataifa tangu kuanzishwa kwake, Januari 29 timu ya Dedebit walifanikiwa kutoka sare ya mabao 4-4 na Yanga. Kwa wenyeji Yanga, sare hiyo ulikuwa mwanzo mbaya kwao kwani kutokana na kucheza nyumbani, walipaswa kucheza kufa au kupona ili kushinda kujiweka kwenye nafasi nzuri kabla ya kwenda mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa mechi ya marudiano. Kiwango ambacho kilionyeshwa na Dedebit katika mechi ya kwanza, kilitosha kuwa onyo kwa Yanga ambayo siku hiyo walionekana kucheza chini ya kiwango na wengi wenye kuijua vizuri soka, walisubiri kushuhudia maajabu ya soka kwa Yanga. Kiwango ambacho kilionyeshwa na Yanga katika mechi ile, kilitosha kusema Yanga walikuwa na mtihani mgumu kwa Dedebit katika mechi ya marudiano kwani mbali ya umahiri wa Waethiopia hao, pia mcheza kwao hutuzwa. Wakati Yanga wakipaswa kujilaumu wenyewe kwa kuruhusu mabao manne kwenye uwanja wa nyumbani, Dedebit kwao ikawa furaha kwani ulikuwa mtaji mzuri kuelekea mechi ya marudiano pale katika viunga vya Addis Ababa. Kama ilivyotarajiwa na wenye kujua mazingira ya soka, wakiwa na akiba ya mabao manne ya ugenini kibindoni, Dedebit walipambana na kufanikiwa kushinda mabao 2-0, hivyo kuwangoa Yanga kwa jumla ya mabao 6-4. Yanga imeaga michuano hiyo katika hatua hiyo ya awali huku Dedebit wakisonga mbele ambapo watakutana na Haras El Hadoud ya Misri ambapo mechi ya kwanza itapigwa kati ya Machi 18 hadi 20 na kurudiana Aprili Mosi hadi 3. Ingawa kufungwa ni sehemu ya mchezo, lakini kwa Yanga, kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na mparaganyiko uliopo ndani ya klabu hiyo kuanzia kwa viongozi hadi kwa benchi la ufundi. Kwa upande wa uongozi, ndani ya Yanga kumekuwa na msigano ambao umekuwa na sura tatu tofauti, lakini zote zikiwa na athari kubwa kwa mustakabali wa timu hiyo. Sura ya kwanza, ni msigano kati ya mfadhili na Mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa klabu hiyo Yusuf Manji na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo. Kielelezo cha msigano huo, ni pale Manji alipowataka wachezaji kupiga kura dhidi ya viongozi ambao wanadhani ni kikwazo cha maendeleo ndani ya klabu hiyo. Hili lilileta mpasuko mkubwa kati ya viongozi na mfadhili huyo, akionekana amevuka mipaka yake huku naye akisisitiza kuwa yu sahihi kwa mujibu wa nafasi zake ndani ya Yanga. Kukiwa na hali hiyo, Manji akaibua hoja nyingine ya kutaka kufanyike kwa hesabu za siku 100 za uongozi wa Lloyd Nchunga aliyeingia madarakani Julai 18, mwaka jana. Wengi walipohoji hili, hoja ya mfadhili ikawa ni kutaka klabu hiyo iendeshwe kisasa zaidi huku kile kinachoingia na kutumika, kikijulikana kama kweli klabu hiyo inataka kupiga hatua. Katika hilo, Manji akasitisha misaada yake kwa Yanga kama mfadhili isipokuwa kutoa fedha kwa sharti la kurejeshewa, kwa mfano sh mil. 100 za usajili wa dirisha dogo. Kuna wakati wachezaji nao waligoma wakitaka kupewa chao wakijenga hoja kuwa kwa ujumla wao wanadai zaidi ya sh milioni 700, lakini wakarejea dimbani baada ya viongozi kuahidi kushughulikia tatizo hilo. Zaidi ya hapo, viongozi wa matawi ya Mkoa wa Dar es Salaam, wakaitisha mkutano na kuitaka Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, kuangalia hatua ya kuchukua dhidi ya mwenyekiti Nchunga kwa kufanya maaamuzi pasipo ridhaa ya Kamati ya Utendaji. Mojawapo ni Nchunga kuridhia uteuzi wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, kuwa Mjumbe wa Bodi ya Udhamini bila Kamati ya Utendaji bila ridhaa ya Kamati ya Utendaji na wanachama. Viongozi hao wa matawi, walihoji pia uteuzi wa Francis Kifukwe kuhusika na ufufuaji wa mfumo wa kampuni kwani suala hilo. Kukiwa na hali hiyo, Fred Felix Minziro akateuliwa kuwa Msaidizi wa Kocha Kostadin Papic ambaye aligoma akijenga hoja kuwa iweje atafutiwe msadizi pasipo ridhaa yake. Hali hii ilimfanya Papic asiwepo katika benchi siku Yanga inacheza na Dedebit kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kuamua kuondoka rasmi, hivyo nafasi yake kutwalia na Mganda, Sam Timbe. Mtiririko huu unaonyesha wazi, mazingira ya Yanga kushindwa kufika mbali katika michuano ya kimataifa, yalikuwa wazi kwani katika hali kama hii, ni miujiza timu kufanya vizuri. Kwa mantiki hiyo, hiki kilichotokea kwa Yanga, ni mavuna ya kile kilichopo ndani ya klabu hiyo kuanzia kwa wanachama, viongozi, wachezaji hadi mfadhili wao. Kitu muhimu kwa pande zote, si kuanza kunyoosheana kidole kwamba nani amekuwa chanzo cha tatizo kwani kwa kufanya hivyo, Yanga itazidi kupoteza mwelekeo, hivyo ni kusahihisha makosa. Utimilifu wa mwanadamu, ni pamoja na kutambua kosa na kupata ufumbuzi ili kosa kama hilo lisitokee tena kwa maslahi ya Yanga na soka la Tanzania. Ni wakati wa Nchunga na Kamati ya Utendaji kuketi chini na kumaliza tofauti miongoni mwao kwa upande mmoja na mdahili wao kwa upande mwingine ili Yanga uwe moja katika kupigania maendeleo ya soka na kiuchumi. Wito kwa viongozi na wanachama wa Yanga, hakuna mwingine wa kuibomoa au kuijenga klabu hiyo, isipokuwa wao wenyewe, hivyo wasahau yaliyopita, wakae chini na kufikiria nini wafanye.
KILICHOFANYWA na sehemu kubwa ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya soka Tanzania, ‘Taifa Stars', katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Palestina Jumatano iliyopita kwenye dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam, kimenisikitisha. Wengi wa wachezaji wetu, walicheza mechi ile kama vile hawajui wanachopaswa kukifanya uwanjani ama kama vile wamelazimishwa, kwa kifupi, hawakujituma kabisa. Ni wachezaji wachache waliojituma kwa nia ya kusaka ushindi, ambao ni kipa Shaban Kado, Juma Jabu, Haruna Shamte, Nadir Haroub ‘Cannavaro', Aggrey Mourice, Mrisho Ngasa, Mussa Hassan Mgosi na watokea benchi, Mohammed Banka, Julius Mrope, Godfrey Bonny na Mbwana Samata. Waliobaki, walikuwa wakicheza kama vile wanatimiza wajibu, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kukosa mabao ya kutosha kama wengi walivyotarajia kutokana na timu tuliyocheza nayo. Bila ya kuficha, lakini ni ukweli kwamba, kutojituma kwao, kutokuwa makini wawapo uwanjani, ni jambo kubwa linalowafanya Watanzania kutojitokeza kushangilia timu zetu mbalimbali za taifa, pamoja na klabu. Nipo tayari kuapa kwamba Watanzania wanapenda mno soka na wako tayari kupoteza muda na fedha zao kushuhudia na kugharamia soka, lakini wachezaji wanawaangusha na kuwakatisha tamaa. Uzembe unaofanywa na wachezaji wetu, ndio kwa kiasi kikubwa unaosababisha viwanja vingi vikose mashabiki wa kutosha katika mechi mbalimbali, ziwe za ligi au mashindano mengine. Wengi wa mashabiki wanapofikiria hali itakavyokuwa baada ya mchezo kumalizika, huku timu yao ikiwa imefungwa kutokana na wachezaji kutojituma, wanaamua kutokwenda uwanjani. Matokeo yake mapato yanakuwa kidogo, hivyo hata posho za wachezaji nazo kuwa kidogo vilevile, kitu ambacho kisingetokea kama wangejituma na kupata ushindi wa kishindo katika kila mchezo ambao wanaweza kushinda. Iwapo wachezaji watacheza kwa kujituma, mashabiki hawatajali, kwa sababu wanafahamu fika kwamba hiyo ni bahati mbaya na soka lina matokeo matatu mojawapo ikiwa ni kushindwa. Ni ukweli usiopingika kwamba wachezaji wetu wasipobadilika, kuweka umakini, kujituma kwa moyo na nguvu zao zote wawapo dimbani, tuendako mashabiki watakauka viwanjani. Aidha timu zitabadili na kuajiri makocha wa kila aina, lakini mafanikio hayatapatikana, hivyo tutabaki kuwashangilia wenzetu wa nje daima. Kila nikijaribu kutafakari na kuuchambua mchezo ule wa Stars na Palestina, napata wasiwasi kama kutakuwa na tofauti yoyote kati ya wachezaji wetu wa Stars na wale wanaoshiriki mashindano ya shule. Ninaungana na shabiki mmoja wa soka aliyesema ni afadhali mtu aende uwanjani kutizama mechi za bonanza la maveterani, atafaidi soka kuliko kuja taifa kushangilia timu ambayo inakupa presha muda wote. Sijajua kama wachezaji wetu wanakutana na maneno ya aina hii kutoka kwa mashabiki au laa na kama wanakutana nayo, wao wanayachukuliaje? Ninawashauri wanasoka wetu wa sasa, pale wanapoingia uwanjani kucheza, iwe mechi ya mashindano au kirafiki, wawe wanaichezea Stars au klabu zao, wacheze kwa juhudi na kujituma. Wanapaswa kufahamu kuwa, mashabiki wanakwenda uwanjani kwa nia ya kushangilia ushindi baada ya mechi, hivyo wanapofungwa wanawatesa na kuwasononesha mno mashabiki wao. Kwa kweli kwa staili hii hatufiki, niwaulize wachezaji wetu, hivi ni mpaka mchapwe bakora ndio msake ushindi?.
KARIBUNI sana wapenzi wa kona hii ya kila Jumatatu ya mtiririko wa michezo na hususan soka na hasa soka la Bongo ambalo mi' ni muumini wake mkubwa sana. Kama nilivyowagusia wiki iliyopita, baada ya ile makala iliyowahusu Simba na Yanga ya kutaka kuumana na Hadood na TP Mazembe, huku sisimizi wa Comoro na Ethiopia wakiwatoa jasho, leo nina habari nyingine kabisa juu ya timu iliyofundishwa na makocha 11 kwa miaka 10. Kama kuna mambo yaliyozungumzwa sana katika vyombo vya habari mwezi huu, hususan kuhusu soka ni sakata la timu kongwe nchini yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani, Yanga Afrika, la kocha mkuu Kostatin Papic, kumkataa msaidizi wake aliyeletwa na uongozi, Fred Felix Minziro, na hatimaye kubwaga manyanga na nafasi yake kushikiliwa kwa muda na Baba Isaya au Majeshi na baadaye kuwasili kwa kocha Sam Timbe raia wa Uganda na kuhitimisha mlolongo wa makocha waliopata kutua katika timu hiyo kongwe kabisa hapa nchini. Unaweza usiamini au ukakataa, lakini ukweli ndio huo kuwa timu hiyo kongwe, kwa miaka 10 kuanzia 2001 hadi leo, imefundishwa na makocha wasiopungua 10; ni ajabu kwelikweli. Ni jambo la ajabu na ninadhani klabu hiyo kongwe kabisa hapa nchini, inabidi iingie katika vile vitabu vya maajabu dunia yaani ‘Guinness'. Miaka 10 makocha 10! Kwa taarifa yako, makocha waliopita katika kipindi hicho ni wazawa Charles Boniface Mkwasa, Syllersaid Mziray, Kennedy Mwaisabula (mimi), Juma Matokeo na Fred Felix Minziro, huku makocha toka nje ya nchi ni Jean Pierre Bonganya raia wa Rwanda, Jack Chamangwana wa Malawi, Milutin Micho wa Serbia, Dusan Kondic na Kostatic Papic wote toka Serbia na sasa Sam Timbe wa Uganda! Hivi ni kweli Yanga tatizo lenu ni kocha? Hivi ni kweli mmeshindwa kuwa wavumilivu kiasi hicho? Hivi ni kweli wanachama na wapenzi hamjishangai? Kabla ya watu wa nje kuwajashangaa? Mtawatimua makocha wenu mpaka lini? Ni kocha gani atakayekubali kufanya kazi na nyie na kupanga mipango yake ya muda mrefu kama atakuta historia yenu mbaya kiasi hicho? Na dunia leo ni kama kijiji habari ziko wazi duniani kote. Leo Sam Timbe, ameripoti Yanga na kauli mbiu yake, anasema anataka Yanga icheze soka, sio ipige mpira mbele. Namuonea huruma sana Timbe, kocha leo ataingiza kitu ambacho sidhani kama wapenzi wanataka, kuna rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia, tatizo la Yanga wenyewe wanashangilia vitu viwili tu, navyo ni kufunga bao na filimbi ya mpira kwisha na si vinginevyo. Sasa mashabiki wa aina hiyo hawataki burudani, Timbe anataka kuleta burudani, namwonea huruma sana, ni bora apate matokeo mazuri nje ya hapo na yeye safari mapema tu itamuwakia. Bahati nzuri mwandishi wa makala hii, ni mmoja kati ya hao makocha waliopata bahati ya kupita pale Jangwani, ni ukweli usiopingika na bila kumung'unya, baadhi ya wanachama wa Yanga hawawezi kusomesha watoto wao, kula chakula cha siku, kujenga nyumba na hata kuwa na maisha ya unafuu, bila kuwa na migogoro pale Jangwani, maisha yao yote wanategemea migogoro tu. Migogoro inapotokea, ndipo wanapokula, ndipo wanapata nafasi ya kwenda kuchukua fedha katika pande hizo mbili zenye mvutano na bahati nzuri, sio wengi ni kakikundi ka watu wachache, lakini wanaonekana wana nguvu kubwa ndani ya klabu na bahati nzuri binafsi nawajua wote mmoja baada ya mwingine. Ukiwaona kwa macho unaweza ukadhani kuwa wana mapenzi makubwa mno na Yanga na wako mbele kwa kila jambo, lakini mwisho wa yote hawakubali hali ya utulivu iwepo klabuni kwa kujua watakula wapi! Uongozi ulioko madarakani, ukiongozwa na mwanasheria Lloyd Nchunga ulipoingia tu, ukaanzisha utaratibu mpya wa kila tawi liwe linakaa milangoni, hapo ndipo balaa lilipoanza, kwani lile kundi dogo linalopenda vurugu, moja wapo ya kazi zake kubwa ni kudhibiti fedha za milangoni ili ziende vizuri kwenye matumbo yao, sasa unalinyang'anya tonge mdomoni, vurugu zinaanza, sasa viongozi wanapoona vurugu ambazo zinaletwa na wanachama wachache sana kwa kile wanachodai kiwango kibovu cha timu hata kama inaongoza ligi, dawa yao wanaona ni rahisi tu, kutimua kocha na kumleta mwingine, lakini gonjwa lipo pale pale ni njaa ya watu wachache ndiyo inasababisha hayo
na timu inaingia katika zoezi lake lile lile la kubadili makocha kama nguo leo. Sam Timbe wa 11 ndani ya miaka 10, duuh! ni hatari lakini ndiyo hivyo. Duniani kote, kocha anafukuzwa kutokana na kazi ya timu uwanjani na si vinginevyo, lakini Yanga sio hivyo, ni ajabu na kweli hao ndio Gongo wazi, watoto wa mitaa ya Twiga na Jangwani. Kama kweli Yanga inataka ijitoe katika janga hili, ni lazima iwatoe au iwaweke kando wale wenye njaa ambao wenyewe kwa macho ndio wanajifanya wana uchungu sana na Yanga kuliko wale kina Tabu Mangara na Kondo Kipwata Mzee sio hao watoto wao. Lakini suala la kuwatoa hao, linahitaji nguvu kubwa sana, tena kutoka nje ya Yanga na si ndani, mfano kuna sababu gani mwandishi wa habari, akaenda kumhoji mtu habari za Yanga, hata katika uongozi wa tawi la Yanga hayupo? Huo nao kwa kiasi kikubwa ni chanzo cha migogoro katika timu. Hivi kuna uhalali gani kwa mwanachama kuvunja kioo cha gari la kiongozi wa timu aliyechaguliwa kwa kura nyingi tu na wanachama, halafu bado vyombo vya dola vimwachie tu akizurula mitaani? Dola nayo isaidie na mbaya zaidi kiongozi huyo alikuwa anawazuia mashabiki wasiwadhuru wachezaji wao. Kuna uhalali gani shabiki ampige Nsa Job na kujifanya yeye ana uchungu sana na timu kumbe wapi, katumwa tu kuharibu hali ya hewa. Kuna sababu gani ya viongozi wanaoingia madarakani kuwakumbatia watu hao hata katika zoezi zima linalohusu usajili, ilhali wakijua kabisa kuwa hao ni watu ambao hawana hata uwezo wa kumnunulia mchezaji togwa! Unategemea nini hapo, zaidi ya kusajili mchezaji bomu ili tu avute asilimia 10 na mwisho wa siku, kocha hafai, leo tunaye wa 11 ndani ya miaka 10! Kuna sababu gani mfadhili kama Yusuf Manji aliogope sana kundi hilo dogo kabisa na kila wakati kuliita na kulipa fedha zisizopungua laki mbili kwa kila mtu? Lazima hapo kuna matatizo na yatazidi kuendelea kwa sababu huyo anayewapa hela ana uwezo wa kuwaambia chochote ili mradi kila kukicha pale ni vurugu tupu. Ushauri wangu wa bure Yanga, ni kwamba nyie kundi dogo mnaojifanya ni Yanga damu, watu wenye akili wamewachoka, piganeni kukaa milangoni sawa lakini msiliingilie benchi la ufundi, wapeni muda makocha wafanye kazi yao kwa utulivu, waacheni sasa Sam Timbe na Fred Minziro miaka mitano tuone kazi yao. Kweli, Yanga leo inasikitisha kweli kweli, miaka 10, makocha 11? Duuh!
Mwandishi wa makala hii ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi Bandari na sasa anasoma Chuo cha Bandari, Diploma of Maintenance. Anapatikana kwa Email: kennymwaisabula@yahoo.com.
BENDI ya African Stars ‘Twanga Pepeta' leo usiku itanarajiwa kufanya onyesho la kupamba usiku wa wapendanao ‘Valentine Day', katika ukumbi wa Da' West Park , Tabata jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa waratibu wa onyesho hilo lililopewa jina la Dodoma Wine Valentine Show, Bob Entertainment na Keen Arts kwa udhamini wa Dodoma Wine na Fredito Entertainment, litatumika kuwatambulisha wanamuziki wapya wa bendi hiyo. Bendi hiyo inayotamba na mtindo wa Sugua Kisigino, inatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo ikitokea Zanzibar kutumbuiza katika tamasha la kimataifa la Sauti za Busara. Twanga Pepeta kwa sasa inatamba na nyimbo zake ilizorekodi na gwiji wa muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Bozi Boziana, ambazo ni ‘Mwana Dar es Salaam', ‘Shida ni Darasa', ‘Rafiki Adui', ‘Mwisho wa Ubaya ni Aibu', ‘Nazi Haivunji Jiwe' na ‘Sitaku Tena'. Wanamuziki wapya wa bendi hiyo watakaotambulishwa ni Greyson Semsekwa, Khadija Mnoga ‘Kimobitel' na chipukizi aliyetamba katika mashindano ya BSS, Haji ambao wataungana na wenzao kama Charles Baba, Dogo Rama, Msafiri Diouf, Amigolas, Vena, Saleh Kupaza, Luiza Mbutu na Janet Isinika katika safu ya uimbaji. Kwa upande wa upigaji vyombo wapo Jojo Jumanne, Adolph Mbinga, Thabiti Abdul, Miraji Shakashia, Gody Kanuti, Victor Mkambi, James Kibosho, huku safu ya unenguaji ikiwa na kina ‘Super K', Saidi, Mandela, Abdilayi Zingu, Asha Sharapova, Lilian Tungaraza ‘Enternet', Aisha Madinda, Maria Soloma na wengineo.
KAMPUNI ya filamu ya Arafat Smart Game ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii imepanga kuziingiza sokoni filamu zake mbili za ‘OCD' pamoja na ‘Blandina'. Mkurugenzi wa Arafat, Omary Mbega ‘Director Ommy' alimweleza mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana kuwa, filamu hizo zitasambazwa nchi nzima na Kampuni ya Fumos iliyo chini ya Ajay Chavda. Aidha, Director Ommy alisema kuwa, filamu hizo zitakapotoka zitapatikana kwenye maduka yote, hapa jijini Dar es Salaam pamoja na mikoani, ambako zitakuwa kwenye mikanda ya kawaida VHS, VCD na DVD. Alisema kuwa, filamu hizo alizozisifu kuwa zitakuwa moto wa kuotea mbali zitawashika vilivyo mashabiki wengi wa soka na kwmaba kazi zote zibebeba ujumbe mzuri kwa jamii. "Wahusika katika OCD ni kama Bambucha, Zungu na Mateso, na kwenye ‘Blandina' ni Blandina, Penina na Bambucha," alisema Director Ommy. Alisema kuwa pamoja na kwamba yeye mwenyewe amecheza katika filamu zote hizo lakini kuna wasanii wengi waliofunika hivyo akawataka wapenzi kutoikosa.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.