SoC02 Mifumo bora ya elimu inaweza kukabiliana na tatizo la ajira nchini

SoC02 Mifumo bora ya elimu inaweza kukabiliana na tatizo la ajira nchini

Stories of Change - 2022 Competition

RWEZAURAJOHN

Member
Joined
Jul 5, 2011
Posts
24
Reaction score
27
MIFUMO BORA YA ELIMU INAYOWEZA KUKABILIANA NA TATIZO LA AJIRA NCHINI

MWANDISHI: PASCAL MUNYWANYI (03/08/2022)

DIBAJI

Mifumo bora ya elimu inaweza kuwa chombo muhimu sana katika kumwendeleza mwananchi kutoka hali duni kwenda maisha bora. Kuajiriwa limekuwa lengo kuu la wasomi wengi hapa nchini. Pamoja na ukweli huu, zipo juhudi kadhaa za kuwahimiza wahitimu kujiajiri. Juhudi hizi zinaonekana kukutana na changamoto za vigezo vinavyokinzana na pale elimu inapoishia. Vigezo hivi ni pamoja na kukosa uzoefu wa kazi, kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, wanaotaka kujiajiri hawana mitaji. Sababu za ukosefu wa mitaji, ni pamoja na wasomi wengi kutoka katika familia maskini, na masharti magumu yanayowekwa na taasisi za fedha, ili kulinda raslimali hiyo isipotee. Masharti hayo ni pamoja na uzoefu katika shughuli anayoiombea fedha, kuwa na mali isiyohamishika kama dhamana, kuwa shughuli hai inayoombewa fedha, na kutokukopesha hatua za awali za kuanzisha miradi, pamoja na kukataa andiko la mradi kwa kigezo cha kukosa uzoefu. Andiko hili lina lengo la kukabiliana na tatizo la elimu isiyoendana na soko la ajira hapa nchini. Hili linawezekana, katika kukabiliana na kushinda tatizo la ukosefu wa ajira kwa wasomi wetu. Nia ikiwa ni kuondoa mpaka uliopo kati ya elimu na soko la ajira.


UTANGULIZI

Tanzania imebarikiwa kuwa na raslimali nyingi za msingi. Ina watu, maliasili za misitu, ardhi, bahari, na madini. Tuna nguvu kazi ya vijana inayohitimu vyuo vikuu kila mwaka na kuingia soko la ajira (Rejea hotuba ya Mhe Rais, ). Kila mwaka kwa mujibu wa takwimu za wizara ya elimu, tuna wahitimu wasiopungua 900,000 wanaomaliza elimu ya sekondari. Vyuo vikuu vinatoa wahitimu wasiopungua 400,000 kila mwaka. Wakati serikali pekee kwa mwaka 2020 ilitoa ajira ya nafasi 44,096, 2021 ajira 44,800, ambapo mwaka huu wa 2022 ajira zilizotangazwa na serikali ni 32,604. Kwa idadi hii ya wasomi, chini ya asilimia 10 tu inapata ajira ya serikali ambayo ni ya uhakika, wakati asilimia 90 na zaidi wanaingia katika kusaka ajira isiyotabirika. Kwa ukweli huu, andiko hili linaleta mwelekeo wa umuhimu wa kuifanya elimu inayotolewa ilenge kundi hili kubwa ambalo ni nguvu kazi inayoingia mtaani kila mwaka kusaka ajira.


MAENEO YANAYOHITAJIKA KUFANYIWA MAREKEBISHO

A. Mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu

Mitaala ya elimu iandaliwe kimkakati kuendana na hatua za kuhitimu. Katika kila daraja kuwepo na lengo la kumwezesha mtu kujiajiri. Tunaposema kila daraja, tunamwangalia mwanafunzi akiwa na umri wa miaka 18 ambacho ni kigezo cha Tanzania cha mtu mzima anayeweza kuajiriwa au kujiajiri. Kundi hili ni la wahitimu wa Sekondari ambao wamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni wanaoendelea na elimu ya juu. Kundi la pili ni wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu kwa sababu mbalimbali. Hawa wanaoshindwa kuendelea, wanakabiliwa na changamoto nyingine ya kujenga maisha. Inafaa na inatakiwa hiyo elimu waliyoipata iwe na kitovu cha awali (primary hub) cha kuanza maisha. Mfano, Kupitia somo la Kemia vijana hawa wanaweza kutengeneza mafuta, sabuni n.k. Pia kupitia somo Biology wanaweza kuanzisha bustani mbalimbali za mboga, matunda, maua n.k. Inashangaza kuona familia zina wahitimu wa sekondari, Lakini wananunua sabuni, mboga, wanakosa nyama za ndege wafugwao, wakati mazingira yanaruhusu. Vivyo hivyo wasomi wa Elimu ya Juu wawe na mwelekeo, mara tu baada ya kumaliza masomo yao.

B. Mfumo wa elimu ya juu umwandae msomi kukidhi vigezo vya soko la ajira
Vigezo vya soko la ajira vinapatikana katika maeneo mawili; Kuajiriwa na Kujiajiri. Vikwazo vya kuajiriwa vinatakiwa viangaziwe na elimu yenyewe wakati mwanafunzi akiwa chuoni. Vivyo hivyo, vikwazo vya kujiajiri vinatakiwa viangaziwe na elimu yenyewe wakati mwanafunzi akiwa chuoni. Vigezo hivi ni pamoja na kuwa na uzoefu kama kigezo cha kupata ajira, na kwa upande mwingine, kuwa na shughuli hai, mali isiyohamishika na uzoefu katika mradi unaotafutiwa mtaji, kwa wanaojiajiri. Maeneo mawili yanaweza kuboreshwa katika mchakato huu;

i. Kuwapa wasomi uzoefu wa kazi bila kuongeza muda wa masomo ili kukidhi kigezo cha uzoefu kinachotakiwa na mwajiri. Kwa mujibu wa sera ya elimu (2014), Elimu ya Juu inayoratibiwa na serikali ni hadi shahada ya kwanza ambayo ni miaka mitatu. Bila kuathiri sera hii, Mwanafunzi atakaa darasani miaka miwili chini ya walimu kwa nadharia na vitendo. Mwaka wa mwisho utumike kwa mafunzo kazini (Internship) vyuo vikishirikiana na mashirika yanayohitaji nguvu kazi ili kumtengenezea uzoefu. Kwa njia hiyo kuwepo uwajibikaji mdogo wa shirika linalopokea wasomi hawa kwa ajili ya kuwapa uzoefu. Ili linawezekana kwa kutumia vigezo vya uwezo wa kitaaluma wa mwanafunzi na vigezo vya mashirika yanayohitaji wafanyakazi.

ii. Kwa kuwa asilimia 90 ya wasomi ambao kwa sehemu kubwa wanatoka familia maskini zisizokuwa na uwezo wa kuwapa mtaji, hawapati ajira serikalini. Elimu iwe na nyenzo ya kumwezesha asiyepata ajira, aweze kujiajiri kwa kupata mitaji. Vikwazo hivi ni pamoja na; kutokuwa na biashara/mradi hai, kutokuwa na uzoefu katika mradi anaoombea fedha, kuwasilisha andiko zuri la mradi ambalo ni mawazo zaidi ya uhalisia, na ukosefu wa mali isiyohamishika kama dhamana. Elimu inayotolewa, iwezeshe kuwa na majibu ya kukidhi vigezo hivi. Kwa maana kwamba, mwaka wa mwisho utumike kuandaa mazingira ya kuwa na biashara/mradi hai, kumpa uzoefu katika mradi huo, au kuwa na ardhi ambayo ni raslimali ya awali ya kila mtanzania.


HITIMISHO

Kwa kuwa tatizo la ajira lipo na linazidi kuongezeka, pamoja na juhudi nyingi zinazofanywa na serikali yetu tukufu ya Tanzania, kuna haja ya kujipanua na kuangalia ni kwa namna ipi nzuri na yenye tija, isiyoongeza gharama na mzigo kwa serikali na vyuo vyetu. Kutumia fedha ileile na sera zilizopo, kumwandaa msomi wa Tanzania kukabiliana na changamoto za soko la ajira. Mimi naamini kwamba endapo kuna utashi wa kisiasa Kama alivyosema Waziri wa elimu Prof. A. F. Mkenda () kwamba elimu lazima ilenge kumwezesha mwanafunzi kupata ajira katika mitazamo yote miwili; Kuajiriwa na kujiajiri. Katika kuboresha mitaala hiyo, itasaidia kumwandaa msomi ili kukidhi vigezo vya soko la ajira kitaifa na kimataifa. Zipo sababu nyingi za kumwandaa msomi kukidhi vigezo kama tulivyosema awali, mwajiri anaangalia ufanisi, ndiyo maana anahitaji wazoefu. Vivyo hivyo taasisi za fedha zinaangalia usalama wa fedha zake. Kwa hiyo, tatizo linabaki kwenye mifumo ya elimu kumwandaa msomi kukabiliana na changamoto hizi.
 
Upvote 3
Share, Recommend, and write your comments. (Shirikisha wazo hili kwa wengine, andika maoni yako, pendekeza kama linafaa).
 
Back
Top Bottom