SoC04 Mifumo bora ya uongozi suluhu ya ‘uchawa’ na kujipendekeza kwa viongozi wa Serikalini

SoC04 Mifumo bora ya uongozi suluhu ya ‘uchawa’ na kujipendekeza kwa viongozi wa Serikalini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Jobstata

New Member
Joined
May 29, 2024
Posts
2
Reaction score
1
Tanzania ni taifa linalopatikana Afrika ya mashariki na ni mwanachama wa jumuiya ya nchi za Afrika mashariki (EAC), katika jumuiya hiyo kila taifa linaongozwa na siasa ambazo hazifanani kabisa na taifa lingine. Hii ni kutokana na historia tangu mataifa haya yaliopoundwa, kwa mfano Kenya ni taifa ambalo bado linatafunwa na ukabila, hali hii ni tofauti kwa Tanzania ambapo tunajivunia kuwa na tunu za taifa ambazo ni lugha ya taifa ambayo ni Kiswahili, amani, mshikamano na upendo vitu hivi vinawafanya watu wake ‘Watanzania’ kusahau kabisa neno kabila kwasababu wote wanazungumza lugha moja.

Tangu taifa lipate uhuru mwaka 1961 hakujawahi kuwa na machafuko ya kisiasa, awamu zote sita za marais wamebadilishana madaraka kwa amani tofauti na baadhi ya mataifa jirani na Afrika kwa ujumla. Licha ya sifa nzuri katika nyanja hiyo Tanzania inasumbuliwa na mambo mawili ‘Uchawa’ na ‘kujipendekeza’ ambapo yakifanyiwa kazi mambo haya naamini taifa litapiga hatua katika ngazi ya uwajibikaji na utawala bora.

Kujipendekeza na uchawa. Neno kujipendekeza lilikuwa maarufu sana katika utawala wa awamu ya tano chini ya Dokta John Pombe Magufuli (Mwenyezi Mungu amrehemu) ambapo baadhi ya viongozi hata wa ngazi za juu za kimaamuzi walishuhudiwa wakimpa sifa hata asizo stahili ilimradi tu kulinda nafasi walizonazo. Wapo baadhi walienda mbali zaidi na kusema ‘Mungu amshukuru rais (Magufuli), Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Tabora Agrey Mwanri mwaka 2019, ingawa baadaye aliikana kauli hiyo kwa kufafanua kuwa haikuwa tafsiri yake kama ambavyo wengi waliitafsiri. Chanzo EATV.

Kujipendekeza ni zao la uoga, ambapo matokeo yake huligharimu taifa kwa sababu Rais ni taasisi inayozungukwa na watu wabobevu katika masuala mbalimbali, watu hawa tunategemea wamshauri vizuri Rais kuhusu mwenendo bora wa taifa badala yake wanageuka kuwa hatari kwa afya ya taifa ‘kujipendekeza’. Kwa mfano Rais Samia Suluhu Hassan wakati anapokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Dr. John Pombe Magufuli mwezi Machi 2021, taifa lilikuwa katika mkwamo wa kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia hii yote ni matokeo ya uoga wa washauri wa rais aliyekuwa madarakani.

Taifa lilishuhudia kudorora kwa mahusiano ya Tanzania na Kenya, kufilisika kwa mitaji kwa baadhi wafanyabiashara na yote hii ilitokana na washauri kusahau majukumu yao na kugeuka wasifiaji tu, hata kama taifa linakwenda mrama.

Uchawa ni neno ambalo limekuwa maarufu sana katika kipindi cha Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan aidha lilipata umaarufu zaidi kuanzia Januari 2023 baada ya kuzinduliwa kwa kile walichokiita taasisi ya chawa wa mama, inayoongozwa na mwenyekiti taifa bi. Lydia Mgaya katika uzinduzi wake ilibainisha kuwa lengo la chawa wa mama ni kujibu hoja za watu wenye mtazamo tofauti kuhusu uongozi wa Rais Samia, chanzo Times Majira TV Januari 15, 2023.

Kabla na baada ya uzinduzi kumekuwa na mwendelezo wa watu binafsi na vikundi kujiita chawa wa mama (Rais Samia). Watu hawa wamekuwa wakitumia muda mwingi kuandaa mikutano ya uchawa na kujadili/kutetea hoja mabazo kimsingi zilitakiwa kujibiwa na watu wenye weledi na jambo husika. Jambo hili ni kupoteza muda, fedha, pia tunajenga utamaduni mbaya wa watu wasio na fikra chanya kwa taifa lao.

Chawa ni mdudu anayekaa katika mwili wa mwanadamu na baadhi ya wanyama kama mbwa, mdudu huyu hupenda mazingira machafu hivyo kwa tafsiri hiyo si neno zuri sana mtu kujiita chawa wa mtu.

Wakati tukitafakari kuhusu chawa wa mama ni vema kutambua kuwa baada ya Rais Samia kuchukua madaraka ya kuliongoza taifa la Tanzania akiwa mwanamke wa kwanza tangu taifa lizaliwe, katika siku 100 za mwanzo madarakani, alijizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya chama chake (Chama Cha Mapinduzi). Hakuna aliyebeza utawala wake hata waliokuwa wapinzani wakubwa wa serikali ya CCM awamu iliyopita wakati Rais Samia akiwa makamu wa Rais.

Umaarufu wa Rais Samia ulitokana na kufanya mageuzi katika mambo yaliyopigiwa kelele na wanaharakati na vyama vya upinzani, miongoni mwayo ni uminywaji wa demokrasia, kufungia vyombo vya habari, kufifia kwa mahusiano kati ya Tanzania na mataifa jirani, kuua sekta binafsi, ukiukwaji wa kanuni za kitaalamu kuhusu COVID-19 nk. Yote hayo yalifanywa na mtangulizi wake hivyo kufanya mabadiliko katika baadhi ya maeneo ilikuwa ni karata mhimu kwake, katika siasa na kufanikiwa kuwafanya wote waongee lugha moja ndipo likazaliwa neno ‘mama anaupiga mwingi’.

Hali hiyo ilidumu kwa muda mfupi sana tunaweza kusema ilikuwa ni nguvu ya soda tu, mambo yakabadilika CCM ikawa ya Samia na Samia ni CCM, watu husema CCM ni ile ile hata akija mtu wa aina gani, pengine ni kwasababu amezungukwa na watu walewale, waliomsifia mtangulizi wake hata alipofanya mambo yasiyofaa kwa ustawi wa taifa ndiyo haohao wanaomshauri Rais Samia leo.

Baadhi ya mambo yaliyompotezea umaarufu Rais Samia.
Pengine kwa kushauriwa vibaya Rais Samia amejikuta akikumbana na upinzani mkali kutoka nje ya chama chake mambo hayo ni pamoja na kushindwa kukubali mabadiliko ya katiba mpya, sakata la DP World, tozo, sakata la Ngorongoro, mikopo kutoka mataifa ya nje na taasisi za kifedha za kimataifa na kupaa kwa gharama za maisha.

Hatuwezi kupiga hatua kama watu wanaomshauri Rais kila siku wanamjaza hofu ya uchaguzi wa 2025, hofu ya uchaguzi imeibua miradi mbalimbali ambayo kimsingi inaligharimu taifa kwa mfano, hivi karibuni umeibuka mradi unaitwa ‘TK Movement’ ambapo uzinduzi wake ulifanyika Mei 25, 2024. Mradi huu uliwakusanya mamia ya vijana kutoka mikoa yote Tanzania, wasanii, viongozi wa ngazi ya juu katika serikali, waandishi wa habari wakiwemo. Lengo la mradi huu ni kuwaleta vijana pamoja katika maendeleo ya taifa hususani kuunga mkono kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita, ambapo baada ya uzinduzi huo itakwenda katika ngazi ya mikoa. Chanzo: Ukurasa rasmi wa TK movement katika mtandao wa Instagram. Huku ni kupoteza muda na kuchezea akili za vijana na kuwafanya wawe tegemezi kifikra na chanzo cha umasikini.

Swali la kujiuliza ni nani mfadhili wa miradi hii? Je ni kodi zetu? Je ni pesa ya mtu mfukoni?

Nini kifanyike

Tunahitaji mifumo imara na siyo mtu imara, kama tungelikuwa na mifumo imara tusingelikuwa na machawa na watu wanaojipendekeza. Mifumo imara itachochea uwajibikaji, watu (wateule wa Rais) hawatafanya kazi ili kumfurahisha aliyewateua bali watawajibika kwa wananchi na taifa litakuwa na furaha.

Mwisho
Yote yanawezekana endapo tutapata katiba mpya.

Picha uzinduzi wa TK Movement taifa
Chanzo: Ukurasa wa TK Movement Instagram.

Screenshot_20240612_112535_Instagram.jpg
 
Upvote 2
Back
Top Bottom