MKASA WA PILI - Sehemu ya 2
Inaendelea.............
Ndani ya wiki kadhaa baada ya kupata pesa ilitosha kabisa kufanya nauli ya kuelekea Geita kwa ajili ya kumtafuta jamaa yangu yule;Lengo la mimi kwenda Geita ni kuangalia kama naweza kupata fursa yeyote ile ili na mimi nianze kutengeneza pesa maana nilikuwa naona nimechelewa sana katika maisha.Wakati naondoka nyumbani nilimuaga mama,wakati huo wale dada zangu wote wawili walikuwa wameolewa,yule dada yangu mkubwa alikuwa kaolewa hapo hapo Mwanza,na yule mdogo niliyekuwa nikimfuatia yeye alikuwa kaolewa huko Arusha,hivyo mama alikuwa pale nyumbani na watoto wa shangazi yangu ambao walikuwa mabinti wawili;wao walikuwa wakiishi hapo Mwanza tangu zamani hivyo tulivyohamia Mwanza baada ya dada zangu kuolewa ilibidi waje pale nyumbani kukaa na mama,shuleni walikuwa wakienda ila wakitoka wanarudi pale nyumbani.Nilimwambia mama kwamba rafiki yangu tuliyewahi kusoma naye,maisha yake ni mazuri huko Geita,sasa aliniambia nikaonane naye;mama alinikubalia ila mara zote alikuwa akiniambia “niwe muangalifu” ,hayo ndiyo maneno mara zote alikuwa akiniambia mama yangu.
Niliianza safari ya kuelekea mkoani Geita.Baada ya masaa kadhaa nilifika Geita,sasa kwakuwa jamaa aliniambia yeye anakaa Katoro ilibidi niulizie pale Geita gari zinazoelekea Katoro,nilipofanikiwa kuzipata, nililipa nauli nikajipatia tikiti tayari kwa safari.Nilifika katoro muda umeenda na hapo nilikuwa sijala chochote tangu natoka Mwanza,pale stendi ya Katoro kulikuwa na daladala (Hizi ni zile baiskeli walizokuwa wanazitumia watu wa huko maalumu kwa kubeba abiria),kwa wakati huo zilitumika sana hizi baiskeli maana bodaboda zilikuwa chache na kama zilikuwepo basi mimi sikufanikiwa kuziona hayo maeneo.Nilimfuata jamaa mmoja aliyekuwa na baiskeli ambayo ni daladala kumpatia maelezo ya jina la yule jamaa aliloniambia kwamba nikifika niulize mtu yeyote kwani anafahamika na ningepelekwa mpaka kwake,lakini yule jamaa wa daladala pamoja na maelekezo yote niliyompatia alikuwa hamfahamu yule jamaa.
Jamaa wa daladala aliniambia "Unajua hii Katoro ni kubwa vilevile pia ni ndogo,hapa kuna matajiri wengi,pia kumbuka matajiri wa huku ni nadra sana kupanda daladala maana wengi wana magari yao".
Jamaa akaendelea kuniambia "Unajua hawa matajiri wanapendelea kwenda kwenye mahoteli makubwa na mabaa makubwa kwa ajili ya starehe,sasa unaonaje nikupeleke kwenye mahoteli na mabaa maarufu ninayoyafahamu,uenda ukifika hapo na kuulizia itakuwa rahisi kumpata?”.
Kweli,tulifanikiwa kufika kwenye bar ya kwanza kuuliza,kuna jamaa alikuwa akichoma nyama akatuambia kwamba" jamaa mbona anafahamika sana ila anapoishi ndiyo sipafahamu".
Tulijaribu sana kumuomba yule jamaa mchoma nyama atuulizie pale bar uenda kungekuwa na muhudumu yeyote aliyekuwa akipafahamu kwake atupatie muongozo wa namna ya kufika.Baada ya kuona jamaa akiwa anaendelea na shughuli zake,yule jamaa wa daladala alimfuata jamaa mwingine alikuwa amekaa pembeni,ilioneka yale maeneo yeye ni mwenyeji,jamaa wa daladala alimuuliza na kwa bahati nzuri jamaa alimwambia yule jamaa ninayemtafuta mimi kuna sehemu anakaa,akamuelekeza Yule jamaa wa daladala,kwasababu Yule jamaa wa daladala alikuwa mzoefu wa yale maeneo alionyesha kutingisha kichwa ikiwa ni ishara ya kuelewa.
Basi jamaa aliporudi aliniambia "Kaa kwenye baiskeli twende".
Jamaa aliendelea kuniambia "Wewe twende mpaka yale maeneo jamaa aliyonielekeza maana tukifika hapo tunaweza kuuliza".
Tulipofika yale maeneo jamaa aliyoelekezwa tulisimama,jamaa akaniambia “sasa hebu tutafute mtu atuelekeze".
Yale maeneo yalikuwa na nyumba nzuri na kimuonekano,uenda walikaa watu wenye pesa zao.Kuna mama mmoja alikuwa anapita nilimsimamisha nikamsalimia kisha nikajaribu kumuulizia lile jina aliloniambia jamaa tukiwa Mwanza,Yule mama alionekana kumfahamu sana jamaa maana aliniuliza "wewe ni nani yake mwanangu?” .
Nilimueleza mimi ni rafiki yake;Baada ya mazungumzo ya kueleweshana,yule mama alituelekeza mtaa wa pili toka pale tuliposimama na akatuelekeza namna hata nyumba yake ilivyokuwa,nilimshukuru sana yule mama.Nilipanda kwenye baiskeli na kuelekea huo mtaa wa pili ambao yule mama alituelekeza,ile nyumba mama aliyotuelekeza niliiona na kuitambua vizuri!,kiukweli kwa muonekano tu wa ile nyumba,nilijisemea kimoyomoyo ya kwamba jamaa alikuwa na “pesa na wala si mchezo!”.
Yule jamaa wa daladala ilibidi nimwambie “ndiyo hapa,wewe sasa waweza kurudi”.
Nilimuuliza “ni shilingi ngapi?”.
Jamaa akaniambia "ni 600 tu kaka".
Nilimuuliza jamaa “mbona kama tumezunguka sana halafu bei inakuwa ndogo hivyo?”.
Jamaa alinijibu kwamba "Kwa mzunguko huwa tunabeba abiria kwa shilingi 200, kwakuwa tumefanya mizunguko 3 ndiyo unapaswa kulipia hiyo 600".
Mimi kiukweli niliona kama nimemuibia,ndipo ilibidi nimpe shilingi elfu 1000,jamaa alishukuru sana akawa ameondoka zake.Nililisogelea geti na kuanza kugonga,haukupitia muda kuna binti alifungua geti.
"Shikamoo" alinisalimia.
Nilimuitikia "Marhaba".
Sasa ilibidi nitumie jina la shule la jamaa maana nilijua haiwezekani mpaka nyumbani kwake wasilijue jina lake,niliona lile jina maarufu litakuwa ni huko mtaani tu ila kwake nadhani jina lake halisi lilifahamika.Yule binti alitingisha kichwa kuonesha ishara ya kukataa yaani jamaa hayupo.
Nilimuuliza"Nani yupo?"
Alinijibu "Yupo dada".
Nilimwamba aniitie dada yake ambaye nilifahamu ndiyo anaweza akawa mke wa jamaa;Baada ya kwenda kumuita dada yake inaonekana dada mtu alimwambia niingie ndani.Yule binti alikuja kuniambia “dada kasema karibu ndani".
Baada ya kuingia ndani ya geti yule dada aliniambia "karibu kaka,sijui nikusaidie nini tafadhali”.
Ikabidi nianze kujitambulisha "mimi naitwa Lwanda magere ni rafiki yake na.........”.
Ilibidi nimueleze kila kitu tangu tulipokutana Mwanza na yule jamaa,baada ya kuwa nimejitambulisha alinikaribisha ndani kwani aliniambia jamaa hayupo na huwa anarudi usiku,mida hiyo ilikuwa saa 10 jioni,yule dada alimwambia yule binti aniandalie chakula.Ile nyumba ilikuwa inakidhi vigezo vyote vya mwanadamu mwenye shauku ya kuwa na maisha mazuri,jamaa inaonekana aliyapatia sana maisha.Wakati nikiwa pale sebuleni yule dada ambaye alikuwa mke wake alichukua simu akampigia jamaa akamueleza ujio wangu na ndipo jamaa alimwambia “mpe simu niongee naye!”.
Yule dada alinipa simu nikaanza kuongea na jamaa,jamaa alionesha kufurahi sana,aliniambia nisiwe na wasiwasi kwani hapo ni kama kwangu tu!,alisema angerudi muda si mrefu maana yupo Geita kazini kwake.Basi baada ya kuwa nimemaliza kuongea na jamaa niliendelea kuwa mtulivu nikimsubiria.Chakula kilipokuwa tayari kilitengwa kwenye chumba maalumu cha kulia chakula(dinning room)ndipo nilisogea kuelekea kula,yule dada yeye muda wote alikuwa chumbani kwake,huku yule binti alikuwa akiendelea na shughuli zake, hivyo nilibaki mwenyewe pale sebuleni nikijiachia kama kwangu.Baada ya kumaliza kula nilielekea sebuleni kukaa kuangalia luninga.
Itaendelea...........................
............................................................
MKASA WA PILI - Sehemu 3.
Inaendelea.............
Ilipofika mida ya saa 1 usiku nilisikia honi ya gari ikipiga kwa nje ya nyumba hivyo nilifahamu atakuwa ni jamaa karudi.Kweli!,alikuwa ni jamaa ndiye kafika,alionekana kunichangamkia sana na bila kupoteza muda alinitambulisha kwamba yule mwanamke niliyemkuta hapo kwake ndiye mke wake na yule binti alikuwa ni mdogo wa huyo mkewe.Aliniambia pia anao watoto wawili mabinti na kwa wakati ule mimi sikuwaona pale sebuleni kumbe baada ya kutoka shule walikuwa wamelala.Basi mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea na jamaa akawa ananielezea namna yeye baada ya maisha kule Tarime kuwa magumu aliamua kutokomea huko Geita ambako aliitwa na rafiki yake,Kwahiyo baada ya mapambano ndiyo kama ninavyomuona alivyo.Mkewe baada ya kumwambia mimi ni msukuma aliniambia "Kumbe wewe niwa kwetu kabisa" .Jamaa yeye alikuwa mkurya wa Tarime.
Baada ya kupiga msosi wa usiku niliona kama ile nyumba imechangamka tofauti na mwanzo maana jamaa kama kawaida yake akaanza kupiga huang'unywa na mimi kama kawa nikakamata soda!,basi yule mke wake akawa ananishangaa mimi kunywa soda wakati wao wakipombeka!,nilimwambia sikuwahi kunywa pombe katika maisha yangu yote, alikuwa akinishangaa sana!,baada ya kuburudika sana usiku ule na stori za hapa na pale jamaa alimwambia mkewe aende akaniandalie chumba cha kulala,ndipo mkewe alimuita yule mdogo wake akamwambia "nenda kaandae chumba cha mgeni"
Yule dogo alisema "Kipo tayari dada"
Baada ya muda nilimwambia jamaa inabidi nikapumzike,ndipo jamaa aliniambia kesho asubuhi tutaondoka wote kuelekea geita akanionyeshe kazi zake zinavyofanyika,nilimkubalia ukizingatia nilienda kule ili kama ingepatikana kazi yeyote nianze kuifanya ili kujipatia kipato maana maisha ya jamaa tayari yalishanichanganya akili!.Basi niliingia chumba cha wageni ambacho kilikuwa kilikuwa na kila kitu ndani,kabla ya kulala nikaona kwanza nikaoge ili kuuweka mwili katika hali ya usafi.Asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa jamaa alinichukua na safari ya Geita ikaanza,jamaa alikuwa akimiliki enzi hizo gari aina ya Harrier old model na hiyo ilikuwa miaka ya 2012,Kiukweli jamaa niliona kama kayapatia sana maisha!,tukiwa ndani ya gari mastori ya hapa na pale yaliendelea,alikuwa akinisimulia namna alivyompata huyo mkewe mpaka wakaoana!.
Tulivyofika pale Geita jamaa alipaki gari mahala fulani hivi akaniambia "nisubiri kidogo nakuja"
Aliingia kwenye duka moja la vifaa vya ujenzi na ilimchukua kama dakika 10 akawa amerejea,jamaa akawa ananiambia lile duka la vifaa vya ujenzi nilakwake na mara nyingi huwa anashinda hapo kama akiwahi kutoka huko kazini kwake tulipokuwa tukielekea.Tulikuwa tukielekea nje ya mji wa Geita,ilikuwa kama tunarudi Mwanza,baada ya kusonga kwa umbali mrefu hatimaye tuliikamata barabara ya vumbi kuelekea kwa ndani ndani huko!,Baada ya muda wa dakika 45 tulifika hapo kazini kwake.Kiukweli lile eneo lilikuwa kubwa na kulikuwa na watu wengi wakifanya kazi,palikuwa pamechangamka sana,jamaa aliniambia lile ndilo lilikuwa eneo analo miliki kunapofanyika kazi zake za kila siku,akaanza kunitembeza na kunionyesha namna watu walivyokuwa wakifanya kazi.Kumbe lile eneo lilikuwa linahusika na mambo ya uchenjuaji wa udongo wa dhahabu,wao kule walikuwa wanaita "Marudio",haya marudio ni ule udongo ambao migodi mbalimbali huwa wameshauondoa dhahabu,sasa yeye kumbe alikuwa akiununua anafanya kazi ya kuuozesha kwenye mashimo kisha anaufanyia process unatoa dhahabu,na pale tulipofika kumbe ndiyo ilikuwa kambi ya huo udongo maana ulikuwa umerundikwa mwingi sana,ulikuwa umetengeneza kama mlima!,Kiukweli niliamini jamaa alikuwa vizuri maana hapo kambini alikuwa kajenga nyumba fulani hivi za mabati ambazo hao wafanyakazi wake walikuwa wakiishi hapo.
Basi baada ya jamaa kuwa amenizungusha hapo nilimwambia aniajiri nami nianze kupiga kazi maana niliona kama nimechelewa sana katika maisha,jamaa aliniambia kama naweza kweli kufanya kazi,turudi kwanza nyumbani kwake tukapumzike kwa siku hiyo halafu kesho yake tungerudi wote hapo kazini.Tulirudi Geita nakumbuka tuliingia kwenye moja walilokuwa wakiuza nguo na viatu,jamaa akaninunulia jinsi mbili,mashati mawili,akaninunulia na viatu aina ya wanchoma(four angle),Kiukweli nilijiona kama mtu niliyeyapatia maisha kwa wakati huo kumbe nilikuwa msindikizaji tu!.
Tuliingia duka jingine walikuwa wakiuza simu fulani hivi zilikuwa za promosheni ya zain (Airtel),na mbele ya kioo kwa juu vilikuwa vimendikwa Zain,basi jamaa alininunulia nikasajili na laini ya Zain maana ile simu ilikuwa inatumia laini ya Zain tu!,kiukweli nilimshukuru sana Jamaa.Kweli kesho yake ilibidi nimuage yule mke wake nikamwambia ngoja nikapambane na siku si nyingi tungeonana.Tulielekea huko porini kama kawaida na baada ya kufika jamaa aliniambia kwa kuwa sina uzoefu ataniweka niwe kama kibarua ili niendelee kujifunza,ndani ya hiyo kambi kulikuwa na watu walioajiriwa rasmi na kulikuwa na vibarua,walioajiliwa wao walikuwa wakifanya shughuli zilizohitaji uzoefu lakini vibarua wengine ikiwemo mimi kazi yetu ilikuwa ni kupiga chepe kwenye udongo na kupangiwa shifti ya kuzungukia kwenye maduara ya kuozeshea udongo ili kuhakikisha mambo yanaenda sawa!,Wale jamaa walioajiliwa walikuwa wakilipwa mishahara rasmi na sisi vibarua ilitegemea kama dhahabu ingepatikana ndipo tulikuwa tunalipwa posho tu!.
Basi baada ya jamaa kuwa ameondoka alinikabidhi kwa jamaa mmoja tulikuwa tukimuita bonge ambaye alikuwa mmoja wa wale jamaa walioajiliwa,ilipofika mida ya saa 10 jioni,yule bonge aliniambia twende tukale maana ugali wa pale ni kama wa gerezani,ukiukosa muda huo wa jioni ndiyo ilikuwa inatoka,labda mpaka kesho yake tena ndiyo kulikwa na mlo mwingine.Japo nilienda kutafuta maisha lakini kiukweli hali ya pale ilianza kunitisha!,maana ugali wenyewe uliyokuwa umepikwa ulikuwa na sura mbaya sana,siunajua tena ugali wa masela unavyoga kuwa!,walikuwa wamepika na dagaa bila kuungwa nyanya,mchuzi ndiyo ulikuwa mwingi kuliko hata dagaa wenyewe!,Yaani kiukweli nilikula tu ili isije ikaonekana niilikuwa nina dharau!.Ilibidi nizoee ile hali maana sikuwa na namna,nakumbuka kila baada ya siku 7 walikuwa wanafanya kazi ya uchenjuaji kwa baadhi ya mashimo na dhahabu ilikuwa inapatikana,kwa wakati huo aliyekuwa akitulipa ni yule bonge,Pesa yangu ya kwanza kupata kwa kipindi kile ilikuwa laki moja na themanini(180000),nilifurahi sana maana ndiyo ilikuwa hela kubwa kuanza kuikamata hiyo miaka ya 2012,baada ya siku kupita nilikuwa mzoefu wa ile kazi na kuanza kupata marafiki.
Siku moja nakumbuka kuna jamaa miongoni mwa wale vibarua tuliokuwa pale alikuwa rafiki yangu sana,tulikuwa tushazoena alikuwa akipiga stori na mimi akawa anaieleza kwamba yule jamaa yangu aliyenipeleka pale ile kambi si ya kwake bali kuna mtu alikuwa akimuangalizia tu!,ilibidi nimuulize tena jamaa mara mbilimbili!,yule rafiki yangu hapo kambini akawa anasisitiza kwamba yule jamaa ile kambi si yake,yeye pale alikuwa anazuga tu.Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na kumuelewesha ya kwamba mimi sikuwa ndugu yake bali nilikuwa rafiki yake ambaye nilikuwa nimesoma naye tu,huyo rafiki yangu wa hapo kazini aliniambia yule jamaa hakuwa mmiliki wa lile eneo,bali alikuwa ni Jambazi mkubwa sana!.Kiukweli mimi mara ya Kwanza nilikataa sana na sikukubali ila huyo rafiki yangu akanisihi nisimwambie mtu maana watu wengi hapo kazini walikuwa hawafahamu ila aliyekuwa akifahamu ni yule Bonge,wengine wote walikuwa hawafahamu chochote!,rafiki yangu huyo akawa ananiambia kwamba,mwenye lile eneo alikuwa akiishi Mwanza na huwa anakuja mara moja moja kuangalia namna kazi ilivyokuwa inaendelea,huyo rafiki yangu aliendelea kuniambia kwamba,huyo mmiliki wa hilo eneo,anamiliki sehemu kama hizo za kutosha hapo Geita!.Nilirejesha mawazo nyuma maana kuna maswali kadhaa niliwahi kumuuliza jamaa akawa anaishia tu nisiwe na wasiwasi!.
Basi kweli kwakuwa nilikuwa nimezoeana na yule bonge siku moja tukiwa maeneo ya jirani mimi nikipata soda na bonge akipiga Pombe,baada ya Pombe kumkolea ndipo nilimuuliza kuhusiana na yule jamaa yangu aliyenipeleka huko kazini,bonge ndiyo aliponieleza ukweli kwamba "Yule jamaa ni Jambazi na mara nyingi ishu zake yeye na wenzie wanaenda kupigia huko Mutukula kwenye mpaka wa Uganda na Tanzania, kwa kuwa yeye aliniambia toka mwanzo kwamba wewe ni ndugu yake nikajua utakuwa unaelewa!"
Bonge akaendelea kuniambia "watu wote hapo kazini wanafahamu wewe ni ndugu yake!"
Kiukweli baada kusikia vile niliishiwa nguvu maana sasa nikaona linaweza kutokea suala lolote lile nikajumlisha na mimi wakati ndiyo hata sikuelewa chochote!.Siku hiyo ilibidi niweke vocha kwenye kile ki simu changu alichoninunulia jamaa nikawapigia nyumbani,kuna nyumba ya jirani nilikuwa nawapigia halafu wanaenda kumuita mama naongea naye!,basi walipomuita mama niliongea naye nikamueleza kazi namna zilivyokuwa ngumu,akaniambia kuna mtoto wa mama mdogo kutoka Bunda alikuwa amekuja kuniulizia pale nyumbani,alitaka kuna kazi tukaifanye huko Bunda,hivyo alipokuta sipo akawa ameondoka.
Ile taarifa ya mama ni kama ilinichanganya akili yangu,nikamwambia ngoja niweke mambo sawa kesho yake ningeanza safari ya kurudi Mwanza.
Kesho yake asubuhi nilichukua mkoba wangu nikaweka nguo zangu ambazo nyingine zilikuwa chafu,nilimuaga bonge na yule aliyekuwa rafiki yangu nikaondoka zangu kupanda gari nielekee Mwanza,japo bonge alinisihi sana nibaki ili niendelee kukomaa na ile kazi kwakuwa ilikuwa na hela lakini mimi niligoma kabisa;siku zote nilizokuwa hapo kazini,yulee jamaa yangu niliyeambiwa ni Jambazi sikuwahi kumuona tena toka aliponipeleka hapo kambini,alikuwaga akinipigia simu tu na kunijulia hali.
Itaendelea..................