Mikasa ya ajabu niliyoishuhudia kwa macho yangu

Mikasa ya ajabu niliyoishuhudia kwa macho yangu

MKASA WA KWANZA - Sehemu ya 3


Inaendelea.............



Basi siku ya kuwapokea wageni wa dada wa kazi iliwadia na kila mtu alikuwa na bashasha siku hiyo,nakumbuka siku hiyo lilipikwa Pilau ambalo sijawahi kulishuhudia mpaka leo hii na ukubwa wote huu,pale nyumbani kulikuwa na ratiba ya vyakula kila siku kuanzia jumatatu hadi jumapili ilikuwa na chakula chake,Kila jumapili tulishazoea ilikuwa ni siku ya kula Pilau,lakini kilichonishangaza sana ni kwamba siku hiyo pilau lilipikwa haikuwa jumapili ila kwasababu ni chakula ambacho nilikuwa nakipenda basi ilibidi nifurahi kimya kimya.Bado sijajua kama lile pilau ndiyo leo linaitwa Biriani ama vipi maana enzi hizo hata Biriani mimi silifahamu nilichokuwa nakifahamu ni Pilau tu,au wengi wetu tuliuita wali mchafu,Pilau lile lilikuwa jekundu na lilikuwa tamu hatari,kama nilivyosema hapo mwanzo sijawahi kula pilau la aina hiyo toka kipindi hicho mpaka leo hii nishakuwa mtu mzima,kumbuka mwaka huo wa 2000 mimi nilikuwa na miaka 14.

Kweli!,siku hiyo tukala vizuri kuanzia mchana mpaka jioni na kila mtu akajiandaa kuwapokea wageni,kumbukeni hapo mwanzo niliwaambia kwamba,moja ya sharti ilikuwa kwamba,ulipokuwa ukitaka kwenda kuoga ilikulazimu yule dada wa kazi akupe ile sabuni aliyokuwa akiitumia yeye ili ukaogee na hivyo ndivyo tulivyofanya!,ilipofika jioni kila mtu alikuwa yupo tayari;Ilipofika mida ya saa 1 usiku,yule dada alituita kama kawaida pale sebuleni na akatueleza namna alivyopenda tulivyoonesha utii,vinginevyo tungemuumiza yeye binafsi hata sisi pia tungeumizwa,akatuambia kwa kuwa tumejianda kikamilifu,kila mtu awe tayari kuwapokea wageni,kiukweli muda ulizidi kuyoyoma sana,mimi kama kawaida nilipata mashaka kidogo,mida ya saa 4 usiku ilipofika wageni sikuwaona na sijawahi kuwashuhudia wageni wakija pale nyumbani usiku,nilishazoea hata kama wageni wangetoka mbali basi walifika pale nyumbani mapema,ila siku hiyo ilikuwa tofauti,kitu kingine kilichonipa mashaka ni kwamba hao wageni wangefika vipi pasipo mwenyeji wao kwenda kuwapokea?,Kumbuka miaka hiyo simu za mikononi zilikuwa kwa matajiri sana,pamoja na wazee wangu kuwa na uwezo lakini hakuna aliyekuwa na simu ya mkononi au tuliita miche ya sabuni,simu iliyokuwepo ni zile simu za mezani za tu.

Yule dada wa kazi chumbani kwake kulikuwa na harufu ya marashi makali na yenye kuvutia sana!, ilipofika saa 6 usiku muda ambao nilishachukuliwa na usingizi kwenye kochi pale sebuleni,ghafla nilishitushwa na kishindo kikubwa juu ya bati!,kiukweli ndugu zangu sijawahi kuexperience hili tukio na halikuwa tukio la kawaida bali liliogopesha sana na kila mtu aliogopa,Kumbuka haya yote yanafanyika hakuna ambaye huko nje kwa majirani aliyesikia wala kuona bali ni sie humo ndani tu!.Baada ya muda yule dada alituita wote tuingie kile chumba alichokuwa akilala yeye na yule dada yangu mwingine,baada ya dakika 10 yule dada wa kazi hakuweza kuongea tena na alikauka akawa kama samaki mkavu!,kiukweli ile hali mpaka leo sitakuja kuisahau,siku hiyo ilikuwa ni mtafutano humo ndani,ndipo ghafla tulisikia sauti ya mwanamke,huyu mwanamke aliongea rafudhi kama ya watu wa pwani hasa huko Zanzibar!.

Kumbuka sauti tunaisikia ila anaye zungumza hatumuoni,hiyo sauti ilituambia tusiwe na hofu kwani wao wamekuja kumuona binti yao na anashukuru sana kwa sisi kuwa watiifu kwa mtoto wao na akatuambia hajaja peke yake bali kaja na baba yake,basi baada ya ile sauti ya kike kuzungumza ghafla ilianza kusikika sauti ya kiume iliyokuwa nzito,ndugu zangu kumbukeni mpaka huo muda huyo dada wa kazi kakauka,alikuwa hajitingishi wala haoengei,yaani alikuwa kakaushwa kama samaki mkavu!,ile sauti ya kiume ilimuita kila mtu kwa jina lake na nakumbuka aliye kuwa wa mwisho kuitwa na kutajwa jina lake alikuwa dada yangu mkubwa,kiukweli hapa labda niseme kidogo,sijawahi kuona mtu anaongea na haonekani bali mnasikia sauti tu,nilizoea kuona ni maigizo lakini siku hiyo nilishuhudia laivu(Mubashara).Dada yetu mkubwa aliitwa na akaambiwa asogee asimame katikati ya kile chumba,kumbuka tulikuwa kwenye kile chumba alichokuwa akilala dada wa kazi na yule dada yangu mwingine!,basi dada yangu alitii akasogea,ile sauti iliianza kumwambia mambo yafuatayo ambayo bado nayakumbuka,mambo hayo ni haya :-

1.Ahakikishe itakapofika ijumaa ya wiki hiyo ambayo hili tukio limetokea asifanye kama anavyofanyaga,kwani akifanya atapoteza maisha yake,dada aliitikia kwa sauti ya kwamba ameelewa.

Hapo hatukuelewa huwa anafanyaga nini,kila mtu alibaki na swali kichwani mwake.

2.Ile sauti ilimwambia kwakuwa yeye ndiye mkubwa pale nyumbani ahakikishe anamhimiza kila mtu kuwa msafi wa kila kitu kuanzia mwili,mavazi mpaka vyumba tunavyolala vinginevyo tusipofanya hayo mahimizo tutapotea na kuangamia.

3.Jambo la mwisho hiyo sauti ilisistiza ya kwamba wao hawana shida yeyote na sisi na ndiyo maana wametupenda sana kwa kuwa watiifu.

Baada ya hiyo sauti kusema na dada na kila mtu kusikia,ghafla mle ndani ya chumba kulikuwa na mtikisiko mkubwa na vicheko vya kejeli!,ndani ya dakika kama 5 kulikuwa na ukimya wa ajabu huku tukitazamana,ndipo yule dada wa kazi akajitingisha,alilejea kwenye hali yake ya kawaida,hayo yaliyoendelea humo ndani hakutaka tumsimulie kwani alisema alikuwa anayaelewa yote!.Baada ya hapo kila mtu alitaka kufahamu ile hali iliyomkuta,alituambia kuna jambo halikwenda sawa na alipaswa kufa ila kupitia sisi tuliokoa maisha yake!,nadhani hapo mwanzo mnakumbuka niliwaambia kuhusu yule mlinzi wetu mzee Mniko,yule mlinzi siku hiyo ya tukio alikuwa amekunywa pombe ili akili yake ikae sawa,sasa kwa kuwa alisha tahadharishwa na hakusikia kumbe ile adhabu ilipaswa ailipe yule dada wa kazi na ndiyo maana alikaushwa kama samaki,pona pona yake anasema ni sisi mle ndani kutii yale aliyotuambia!.

Hiyo ilikuwa mida ya saa 8 za usiku na baada ya hapo tulitaka kufahamu yule mlinzi kule nje atakuwa na hali gani,basi dada yetu mkubwa alifungua mlango akatoka nje na kumuita yule mzee Mniko lakini hakuitikia,aliendelea kuita sana lakini hakukuwa na ishara yoyote ya mwitikio kutoka kwa yule mlinzi,basi sote tuliingia ndani kulala,dada akasema uenda atakuwa katoka nje ya geti anazunguka huko nje.Kweli!,siku hiyo tulilala kwa wasiwasi sana na kwa kuwa mimi nilikuwa bado dogo dada yangu mkubwa aliniambia nikalale naye chumbani kwake.



Itaendelea ...............
 
MKASA WA KWANZA - Sehemu ya 4.


Inaendelea.............



Kiukweli mimi nilipitiwa na usingizi na hata kulipokucha sikujua kama kumekucha ila nilikuja kuamshwa na dada yangu mkubwa niende nikapige mswaki kwa ajili ya kunywa chai,mambo hayo yote ya huu mkasa yalitokea mwezi wa 12 na vurumai hili liliendelea mpaka mwaka uliofuatia yaani mwaka 2001.Asubuhi hiyo dada zangu waliendelea kumtafuta yule mlinzi wetu mzee Mniko bila mafanikio,walimtafuta kila pembe ya nyumba,huyu mzee haikuwa kawaida yake kuondoka bila kuaga,ilikuwa ni lazima aage kila anapoondoka ili kila mtu ajiridhishe kwamba kuko salama,lakini siku hiyo ilikuwa tofauti,basi kila mtu aliendelea na shughuli zake baada ya kuona mzee hapatikani.Pale nyumbani kulikuwa na migomba, vilevile kulikuwa na maua ya kutosha,hivyo kila siku ilikuwa lazima niimwagilie ile migomba pamoja na maua,nilipokuwa nahitaji kumwagilia ilibidi nichukue mpira mrefu nikaunganishe kwenye bomba,bomba lilikuwa pembeni mwa nyumba yetu,ulikuwa ukiingia pale nyumbani mkono wa kulia mwa geti ndipo lilipokuwa bomba pamoja na tenki la maji lililokuwa limejengewa vizuri na cement,pembeni ya hilo tenki la maji kulikuwa na mti mkubwa wa mchungwa.

Sasa wakati nimefika hapo bombani kwa ajili ya kuchomeka mpira nikamwagilie migomba na maua, ghafla namwona mzee Mniko akiwa amelala chini ya ule mchungwa, kwa mazingira yale yalivyokuwa ilikuwa si rahisi yeye kuonekana!,basi nikakimbia kwenda kuwaita dada zangu pamoja na yule dada Ashura aliyekuwa mfanyakazi wetu,walipofika lile eneo yule dada wa kazi alisema mtu asimguse kwanza,alirudi ndani akavaa nguo flani hivi ndefu na ushungi kisha akaja,kuna maneno aliyatamka lakini sikuyaelwa na ndipo alipomgusa yule mzee Mniko akaamka!.Yule mzee alipoamka aligonganisha macho na dada Ashura akashituka lakini cha ajabu yule mzee alikuwa haongei,yaani alikuwa bubu,kila mtu aliingiwa na wasiwasi,mzee Mniko alilia kama mtoto mdogo maana alianza kuonyesha kwa ishara lakini hakuna aliyemuelewa.

Yule dada Ashura akaanza kumwambia "Siunaona sasa ulivyokuwa,nilikwambia lakini hukutaka kusikia,mdomo wako huo mchafu umekuponza ushukuru umepatikana mzima lakini wasingekuwa hawa ulikuwa uende na maji".

Dada yetu mkubwa ilibidi amuulize dada wa kazi huyo mzee amekuwaje na nini hatma yake?.

Dada Ashura alisema "siku ile nilikuambia uje umwambie huyu mzee siku watakapokuja wageni asinywe pombe na yeye akawa kichwa ngumu hiki ndicho kimempata"

Akaendelea kusema "simnakumbuka jana mimi nilivyokuwa nimekaushwa kama samaki mkavu?,basi ni kwasababu ya ukaidi wa huyu mzee,ila mlioniponya nafsi yangu na yake ni nyinyi kwa kutii yale niliyowaambia!"

Basi dada yangu mkubwa alimsihi sana yule dada wa kazi amuhurumie yule mzee maana alitia huruma kwani alikuwa akilia kama mtoto na sauti haitoki,alikuwa anapiga yowe tu kama mwendawazimu!.

Yule dada wa kazi alisema "mbebeni mpelekeni chumbani kwangu".

Kabla ya hapo niliambiwa mimi kwasababu ni mtoto wa kiume kwamba,kabla hajaingizwa mle chumbani kwa dada Ashura, inabidi akaoge kwanza na hilo zoezi nilisimamie mimi kule bafuni,basi tulimwingiza ndani na tukawa tunamuelekeza kwa ishara lakini aelewi ilibidi dada yetu mkubwa ajiongeze,akachukua daftari na karatasi akawa anamwandikia anasoma na hatimaye akaelewa kilicho maanishwa!,wakati huo mzee Mniko alikuwa aongei wala kusikia chochote!.Hivyo yule dada wa kazi alinipatia ile sabuni yake nikampa yule mzee na mzee akagoma kabisa mimi kumpeleka bafuni kwa kuwa nilikuwa mdogo!Yule dada wa kazi alimwambia dada yangu amwandikie kwenye karatasi na kumsihi kama amekataa kwenda na mimi basi ahakikishe anaiogea hiyo sabuni ili apone vinginevyo ingekula kwake,mzee aliposoma aliitikia kwa kutingisha kichwa kuonyesha ameelewa,dhumuni la mimi kutaka kumpeleka bafuni ilikuwa ni kwamba nikamsimamie na nihakikishe anaogea ile sabuni asije akaoga maji makavu maana mzee alikuwa mbishi sana na alikuwa hapatani na yule dada ashura.

Baada ya kumaliza kuoga alivaa nguo zake na yule dada akasema tumpeleke kule chumbani kwake,wote tukaingia mle chumbani kwa dada wa kazi.

Dada wa kazi akamwambia "vua shati na ukae hapo katikati ya chumba uangalie mashariki!.

Yule mzee aliandikiwa hayo maelekezo kwenye karatasi na dada akasoma na akafanya kama alivyoambiwa, yule dada alianza kutamka maneno ambayo sikuyaelewa kabisa maana yalikuwa ya lugha ngeni!.Mle chumbani ghafla kukaanza kusikika harufu za marashi makali na vicheko vya watu wakicheka,ndipo yule mzee alipoteza fahamu na sisi tukaanza kuogopa maana hali ilikuwa inatisha!,hiyo ilikuwa mida ya saa 3 asubuhi,Yule dada wa kazi akaendelea kutamka yale maneno mpaka kukawa kimya kabisa!,baada ya kupita kimya kila mtu akiwa anashangaa ghafla yule mzee akazinduka akaanza kushangaa kama vile haelewi kitu,ndipo alipoanza kuzungumza kwa kuuliza "Hapa ninafanya nini?".

Dada yetu mkubwa akamwambia "twende unywe chai".

Baada ya kunywa chai yule mzee kumbukumbu zilikaa sawa akaanza kubwata kwa kikurya kama kawaida yake.

Mzee alisema "Yaani wewe umeuletea huu mji shida na matatizo,sasa nakwambia leo nakuua kwa mshale,sasa nakuomba uchague uondoke hapa leo hii au ufe kwa mshale wa sumu".

Hayo maneno yule mzee Mniko aliyatamka kwa lugha ya kikurya.Yaani hii hali ilitufanya watu hapo ndani kuwa kama mazezeta, kana kwamba tumefungwa,wazo hata la kuwapigia wazazi simu halikuwepo na cha ajabu hata wao hawakupiga simu kwa muda huo na wakati haikuwa kawaida yao.Basi baada ya kumaliza kunywa chai yule mzee alimuaga dada yetu na akasema jioni nikirudi nisije kumkuta huyu "Msaghane".

Kwa watu wa Tarime hili neno "Msaghane" anapoambiwa mwanamke lilikuwa tusi kubwa sana na linalomdharirisha!,Yule mzee aliondoka na wengine pale nyumbani tuliendelea na shughuli zetu kama kawaida.kabla ya kufika jioni alikuja pale nyumbani kijana wa yule mzee alikuwa akiitwa Ezekiel,huyu kijana alikuwa akija pale nyumbani mara chache sana endapo labda kuna kazi ambazo zilimuhitaji,alizifanya na mama akawa anampa hela.Sasa jioni ile hakuja kwa ajili ya kufanya kazi ila alikuja kwa taarifa ambayo ilitushangaza kidogo!.




Itaendelea....................
 
Back
Top Bottom