SoC04 Mila, desturi na maadili yanayo tutambulisha kama taifa ili kufikia ustaarabu wa kimaendeleo

SoC04 Mila, desturi na maadili yanayo tutambulisha kama taifa ili kufikia ustaarabu wa kimaendeleo

Tanzania Tuitakayo competition threads

Muharram wa Pili

New Member
Joined
Jun 2, 2024
Posts
3
Reaction score
0
Yawezekana yapo machapisho mengi yahusuyo mila,desturi na maadili lakini yakawa tofauti na wazo langu. Ndio Tanzania nchi yangu ina takribani makabila mia na ushee ambayo yanatofautiana katika tamaduni,lakini yanashabihiana kwenye lugha na asili. Makabila yote hayo kwa wingi wake yametuunganisha katika utaifa na lugha adhwim ya kiswahili ,Muungano wa Tanganyika na visiwa vya Zanzibar vimetupa utambulisho ulimwenguni kama Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dunia inatutambua kama nchi katika ukanda wa Afrika ya Mashariki ,tukizunguza lugha ya umoja ya kiswahili kama Taifa. Hoja yangu katika chapisho hili Ni namna gani kama Taifa ambalo tunatajwa kukua kiuchumi na hata kufikia nchi ya uchumi wa juu wa kati. Je tumejiandaa kukilea kizazi cha taifa hili kutambulika kwa Mila ,desturi na maadili ili kuendana na ustaarabu wa hatua za maendeleo tunazofikia?

Mataifa yaliyo endelea duniani kama China,Japan,Uingereza,Marekani,Urusi na mengineyo mengi tunaona ni namna gani kuendelea kwao kunaenda sambamba na ustaarabu wa aidha miundombinu yao,siasa zao,elimu zao,teknolojia bila ya kuathiri mila,desturi na maadili ya vizazi vyao ili kulinda utambulisho wao kama Taifa.

Kimsingi Taifa ni watu na utaifa ni namna ya kufuata utaratibu wa haki na wajibu wa kuishi kwa miongozo ya katiba na mamlaka za kitaifa zilizokubaliwa na watu wa Taifa lenyewe. Ulimwengu unakuwa kwa kasi kubwa hususan katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Ni lazima kama taifa wakati tunafikiri na kutenda kuwendana na kasi ya kukua kwa maajabu ya sayansi na teknolojia duani.Tuwe tayari kuunda mpango wa kulinda kizazi cha Taifa letu kubaki kwenye asili ya mila zao,desturi na maadili ya Taifa lao.

Elimu isimamiwe ipaswavyo ,kuweko na mitaala yenye kuwaelimisha watoto wa taifa hili asili ya mila ,desturi na maadili ya utaifa wao kutoka kwa babu zao.Elimu lazima iwaandae watoto kuishi katika ustaarabu wa maendeleo yanayofikiwa na nchi yetu ili kulinda miundombinu hiyo.Yawezekana kuna vitu vingi tunaona ni sawa katika jamii kwasababu hatujui asili mila na desturi zetu ,na hazikulindwa hadi kufikia kuathiriwa na propaganda za kilimwengu.

Serikali inalo jukumu la kulinda asili ya mila ,desturi na maadili ya watu wake ili kuunda taifa hai lenye utambulisho kwa watu wake. Wizara ya utamaduni na Wizara ya mambo ya ndani ya nchi iunde kanuni ambazo zitasimamiwa madhubuti kuimarisha maadili kwa kizazi hadi kizazi. Kwa mfano kuwe na kanuni ya kuvaa mavazi ya sehemu za umma na sehemu za starehe. Kuzuia nyimbo zenye matusi bila kutazama watu fulani fulani ama maslahi ya kibiashara ilhali kizazi cha Taifa kina haribikiwa. Kanuni ziwe nyingi zitakazo simamiwa kuleta ustaarabu na kulinda maadili.

Kuundwe tume ambayo itakusanya maoni kwa wananchi kuona ni mila, tamaduni na desturi zipi zilikuwa zina tija kwa kizazi ili ikibidi zifundishwe mashuleni.Mtakao soma andiko langu mtakubaliana nami kuwa kuna tofauti kubwa ya maadili baina ya kizazi cha miaka fualani hadi kizazi fulani na utofauti huo upo kwenye maadili na desturi. Maana yake kadili miaka inavyosogea ndivyo kizazi kinavyo momonyoka kimaadili kwenye mavazi,michezo,starehe, na hata kuheshimiana baina rika na rika.Hii ni hatari kwa Taifa linaloendelea kama tahadhari za kulinda kizazi chetu kama taifa hazitachukuliwa hatua kwa uzito stahiki.

Ifike mahala tutafakari na kuona maendeleo bila kuwa na kizazi kilicho staharabika ni sawa na kufuga Mbwa kichaa ambaye atakung'ata mwenyewe.Zipo jitihada za kupongeza ambozo Serikali imezifanyia kazi kama kuzuia mitandao ya picha za ngono Pongezi kwao.Lakini bado ndani zipo changamoto nyingi hususan kwa vijana na wengi wao wameathiriwa na kukua kwa teknolojia.Yamekuwepo matukio ya kujirekodi picha za utupu,mitandao ya ukahaba,magenge ya uhalifu amboyo ni hatari kwa uhai wa kizazi cha taifa letu.

Mila,desturi na maadili mema hufundisha utiifu. Viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali ni vema mkashabihisha matendo mema ya kimila na mafunzo ya kiimani ili msipingane na asili za watu. Utiifu huanza na kutambua rehema za Mungu naye hutujaalia neema.Kuwaheshimu wazazi na kuwatendea mema kunatupa baraka.Kuheshimu serikali na mamlaka zake hutupa manufaa.Kuheshimu watu wa rika zote kuwa wasilikizana zaidi na kuliko wazungumzaji tunavuna maarifa.Haya yote tukiandaa kizazi chenye kujitambua kiasili yanawezekana.

Mwisho nasisitiza kuchukuliwe hatua za dhati na madhubuti kwa serikali kushirikisha wadau wa amaendeleo na jamii kwenye kukusanya na kupokea maoni ya kukabiliana na wimbi hili la mmomonyoko wa maadili na kulinda mila na desturi za watu wa Taifa lake.Wajumbe wa nyumba kumi kumi wapewe uwezo wa kimalaka kutoa taarifa kwenye makazi yao.Serikali isiwaachie jukumu la malezi wazazi bali wao Walee kizazi cha Taifa hili.


Ndimi wenu Muharram wa Pili.
instagram @amit_antar_sangali.jr
 
Upvote 1
Back
Top Bottom