John Mrema aliwahi kuwa mwanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA kabla ya
kuvuliwa uanachama kupitia tawi lake la Bonyokwa mkoani Dar es Salaam, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu, dharau kwa mamlaka halali za chama, na kukaidi misingi na maadili ya chama.
Kadhalika aliwahi kuhudumu kama mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA ambapo baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025 alikoma kutumikia nafasi hiyo. Aidha baadaye Mrema aliibuka kuwa miongoni mwa waliotofautiana (G55) na uongozi mpya chini ya Tundu Lissu uliosimamia ajenda ya 'No reforms No election' akisema ajenda hiyo haitekelezeki na inazuia haki ya wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu.
Madai
Ipo taarifa inayosambazwa katika mtandao wa Facebook inayodaiwa kuchapishwa na Millard Ayo pamoja na Wasafi Media akinukuliwa John Mrema kuhusu madai ya kuwekewa sumu akitajwa Godbless Lema kuhusika na mpango huo.
Je, ni upi uhalisia wa machapisho hayo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia maneno muhimu (Key Word Search) ulibaini kuwa taarifa hiyo haikuchapishwa na
Wasafi Media wala
Millard Ayo kwenye kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii bali machapisho hayo ni ya kutengenezwa na wapotoshaji waliotumia utambulisho wa vyombo hivyo.
Aidha Chapisho linaloonekana kuchapishwa na Mrema, si la kweli kwani halikuchapishwa kupitia
ukurasa wake kwenye mtandao wa 'X' bali
akilikanusha. Kumbuka Wapotoshaji wanaweza kutengeneza ujumbe kuonesha ulichapishwa na mtu fulani katika mitandao ya kijamii ili kupotosha uhalisia, hivyo ni muhimu kuthibitisha kabla ya kuamini na kuwasambazia wengine.