MAMBO YA KUKUBALIANA MKATABA WA BANDARI TANZANIA NA DUBAI
JE, Mkataba una matatizo? Ndio, matatizo yapo.
Je, mkataba hauna faida? Faida zipo.
Je, Mkataba ni wa milele au wa miaka 100? Hapana, una kikomo. Na sio miaka 100.
Nianze na kikomo; ibara ya 5, kipengele cha tatu, inasema baada ya Mkataba huu kusainiwa, kampuni ya DPW ya Dubai, itaandika proposal kwenda TPA. Kisha TPA na DPW watakubaliana na kusaini makubaliano.
Tafsiri, Mkataba huu wa ushirikiano baina ya Tanzania na Dubai, utakaribisha mikataba mingine mingi ya utekelezaji ambayo itasainiwa kati ya DPW na TPA.
Maeneo ya utekelezaji ni saba awamu ya kwanza, na mawili awamu ya pili. Hivyo, jumla tisa.
Ibara ya 5, kipengele cha nne cha Mkataba, inasema Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha TPA haizingatii proposal nyingine nje ya DPW katika maeneo ya ushirikiano awamu ya kwanza, hadi ipite miezi 12 tangu kusainiwa kwa Mkataba huu.
Mantiki; Mkataba ulisainiwa Oktoba 25, 2022. Endapo itapita miezi 12 bila DPW na TPA kusaini mkataba wowote wa utekelezaji, maana yake, Mkataba huu utakuwa umeisha muda wake. TPA wanaweza kufanya kazi na kampuni nyingine yoyote.
Ibara ya 23, kipengele cha 1 (!) na (ii), inaeleza kuwa Mkataba huu utafika kikomo endapo shughuli zote za mradi zitafika mwisho au muda wa mikataba yote ya utekelezaji wa miradi utafika tamati.
Kumbe; mikataba ya utekelezaji wa miradi ndio itaamua ukomo wa Mkataba huu.
Ibara ya 23 (2) na (3), inaeleza Mkataba huu unaweza kusitishwa kabla ya muda. Taratibu zimeelezwa.
Ibara ya 23 (4), nimeona ndio ambayo imeshitua watu na kudhani Mkataba ni wa milele. Inasema, Tanzania na Dubai, hazipaswi kushutumiana hadharani, kujiengua, kusimamisha au kusitisha Mkataba hata kama kuna upande utakiuka mkataba au kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia.
Kipengele hicho kinaeleza kuwa tatizo lolote likitokea, yafuatwe masharti ya ibara ya 20 ambayo inaeleza jinsi ya utatuzi wa migogoro kisheria.
Ufafanuzi; haitakiwi kushutumiana. Nakumbuka mwaka 2017, Tanzania ilitoka hadharani na kuishutumu Accacia kwa kuiibia Tanzania.
Kipengele hicho kinataka, Mkataba baina ya Tanzania na Dubai, kusiwe na kushutumiana hadharani. Bali, utaratibu ufuatwe wa kisheria kana ulivyoandikwa ibara ya 20.
Leo, Tanzania na Dubai wamesaini Mkataba. Upande mmoja unaweza kupata faida na kuamua kuzusha mgogoro. Au Rais mwingine kaingia Tanzania, mtawala mpya ameingia Dubai, mambo yanabadilika, uhusiano wa kidiplomasia unavunjika.
Sharti la kipengele hicho ni kuwa Mkataba usivunjike kisa kuna mgogoro, bali masharti ya utatuzi wa mgogoro yafuatwe kama yalivyoainishwa ibara ya 20.
Je, ibara ya 20 inasemaje? Ukitokea mgogoro, pande mbili zinaketi kuzungumza. Ikishindikana, shauri linakwenda kwenye Baraza Usuluhishi na Uamuzi (Arbitration Tribunal). Kila upande unateua mwakilishi mmoja.
Pande mbili zitakubaliana na kuteua Mwenyekiti wa Baraza ambaye hatoki Tanzania wala Dubai. Na eneo la kusikiliza shauri linatakiwa kuwa neutral. Imeandikwa itakuwa Johannesburg, Afrika Kusini.
Endapo hakutakuwa na mwafaka wa kuunda Arbitration Tribunal ndani ya siku 30, shauri litapelekwa Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi na Uamuzi (PCA), The Hague.
Mpaka hapo, dhahiri, hakuna wa kung’ang’ania Mkataba hata kama umekiukwa au mazingira hayaruhusu kuendelea, isipokuwa utaratibu uchukue mkondo.
MATATIZO YA MKATABA
Nilishaeleza na narudia, Mkataba umeipa mamlaka makubwa TPA kupokea proposal kutoka DPW na kusaini. Halafu hiyo Mikataba ndio ya utekelezaji (HGAs).
Mikataba hiyo ya utekelezaji, ndio kila kitu. Yenyewe ndio itaamua ukomo wa Mkataba huu. Vilevile fedha na mchanganuo wake, upo huko.
Sasa, ukikosekana uadilifu, na kwa sababu TPA ndio wamepewa rungu la uamuzi, kuna shida itatokea.
Ushauri; kwa vile TLS ni jumuiya ya kisheria inayotambulika Kikatiba, ingependeza jumuiya hiyo ikawa inachambua mikataba ya utekelezaji, kisha ipite Baraza la Mawaziri kabla ya TPA na DPW kusaini.
Kuna suala la Upekee (Exclusivity), hapa nitakopa mitazamo ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na ndugu yangu, Godlisten Malisa.
DPW wamepewa Exclusivity ya miradi ya bandari za Tanzania, ila Serikali haijaibana Dubai ili kusiwe na mgongano wa masilahi.
Zitto amehoji, DPW wanapata exclusive Tanzania, je, Tanzania imehakikisha kampuni hiyo haiendeshi Bandari ya Mombasa? Maana bandari za Dar na Mombasa zinashindana kibiashara.
Malisa anasema, DPW wamepewa haki ya kuendesha bandari zote Tanzania, ikiwemo Mtwara. Wakati huohuo, DPW wanaendesha Bandari ya Beira, Msumbiji. Vipi kuhusu mgongano wa kimasilahi ikiwa Tanzania ina malengo ya kuikuza Bandari ya Mtwara?
Ipo hoja ya Wakili Fatma Karume kuwa awamu ya pili ya maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Dubai, inazungumza bandari zote za Tanzania, maana yake na Zanzibar imo. Wakati huohuo TPA ndio wamepewa mamlaka ya kusaini mikataba ya utekelezaji na DPW. Hilo ni tatizo, maana TPA hai-opareti Zanzibar.
FAIDA ZA MKATABA
Ibara ya 4, Kiambatanisho 1, faida ni kuboresha ufanisi na kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inatoa huduma za usafiri wa maji world class.
Ibara ya 13, kipaumbele cha Watanzania kupata ajira kwenye miradi, na kampuni za Watanzania kupata kipaumbele cha kupata kazi kwenye miradi.
Katika utangulizi, inaeleza matamanio ya Tanzania kukuza mapato ya bandari na kukuza pato la taifa (GDP).
NINI KIFANYIKE
Ibara ya 25 na 26, inatoa masharti ya Mkataba huu kuingizwa kwenye sheria za ndani. Kwa mantiki hiyo, hauwezi kutekelezwa mpaka upite bungeni.
Ibara ya 22, imetoa ruhusa ya mabadiliko ya Mkataba kufanyika wakati wowote, kwa maandishi na pande zote zikubaliane na kusaini.
Hivyo, mabadiliko yafanyike katika maeneo yenye kasoro ili kuondoa wasiwasi mbele ya safari.
By Ndimi Luqman MALOTO