SoC02 Mirathi ilivyo mbolea ya umasikini na upoteaji wa asilia ya vizazi

SoC02 Mirathi ilivyo mbolea ya umasikini na upoteaji wa asilia ya vizazi

Stories of Change - 2022 Competition

Pintuz

New Member
Joined
Aug 18, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Moja ya majukumu yangu ni kuwasaidia wafiwa kuandaa nyaraka muhimu za mirathi na kuwapa ushauri ni namna gani wanaweza kulinda mali za wapendwa wao marehemu na haki za warithi wao kisheria pindi wanapokuwa wamefiwa ikiwemo ufunguaji na uteuzi wa wasimamizi wa mirathi.

Katika utendaji wangu huu kwa kipindi cha karibu muongo mmoja sasa nimegundua MIRATHI NDICHO CHANZO KIKUU CHA UMASIKINI katika jamii zetu haswa hii ya watanzania ambayo mimi nimekuwa sehemu yake kwa kipindi kirefu sana.

Mimi ni mzaliwa wa nyanda za juu kusini, wilaya ya “X”, kijiji cha “A”. Babu na Bibi yangu wapendwa walifariki mnamo mwaka 1990 na 1996 kwa kuongozana. Na walicha makazi yao pale kijijini “A” ambapo imekuwa ndio sehemu yetu tunayofikia wakati wote tangu tupo wadogo mpaka leo hii nikiwa na mimi nina watoto (Vitukuu vya babu na bibi), na panaitwa “kwa Fulani” yaani jina la babu yetu.

Ule mji ambao babu na bibi yetu waliuacha wakati wanafariki ulikuwa na nyumba moja, hivyo baba zetu na shangazi zetu walishirikiana wakaongeza nyumba mbili katika eneo lile lile ili pawe na nafasi ya kutosha kutumudu watu wa familia zote tutakapokuwa tumekwenda katika mapumziko au shughuli nyingine za ukoo. Siku zote nimekuwa nikirudisha heshima kwa wazee wetu hawa kwa ]majitoleo yao ya uwekezaji katika eneo lile ambayo nasimuliwa kuwa yalifanyika miaka ya 1930 yaani miaka 92 nyuma.

Kiutaratibu Inapotokea marehemu amefariki, watu wake wa karibu ambao sheria imewaainisha wanatakiwa kufuatilia cheti chake cha kifo na baadae kufungua mirathi katika mahakama.

Shauri la mirathi linapofika mahakamani, mleta maombi akiteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hupewa kipindi kisichozidi miezi minne kukusanya na kugawa mali za marehemu kwa warithi wake pamoja na kulipa madeni yake. Na mara nyingi wateuliwa hawa wamekuwa wakitekeleza wajibu huo.

Hili la KUKUSANYA na KUGAWA MALI ZA MAREHEMU ndilo lililonifanya niandike andiko hili.

Wasimamizi wa mirathi wamekuwa wakitumia njia zifuatazo kugawa mali za marehemu:
  • Kuuza na kugawanya pato kwa warithi au warithi wao wenyewe kuuza na kugawana pato. Katika njia hii Mfano tuseme marehemu ameacha nyumba 2 na warithi wake wakiwa saba, mali huuzwa kwa manufaa yao saba.
  • Njia nyingine ni msimamizi kuwakabidhi warithi mali isiyohamishika warithi waimiliki kwa pamoja au warithi watawiwa vyumba katika nyumba hizo na kisha wao watapangisha wapangaji ambapo kila mmoja huchukua kodi katika chumba husika tuu.
Njia hizi zote hapo juu zimekuwa ndizo haswa kisababishi cha kukosekana kwa mwendelezo wa mali na utajiri na matokeo yake jamii kujikuta ikiendelea kutumbukia katika umasikini mkubwa na kwa sababu ya kuanza upya wakati wote.

Warithi wakikwisha kuuza nyumba na mali zingine walizorithi, pesa wanayoipata kila mmoja huenda kufanyia matumizi yake binafsi au na familia yake ambayo yanaweza yawe au yasiwe na tija. Hivyo mali au utajiri aliokuwa tayari umeanzishwa wa marehemu unakosa mwendelezo kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Mzunguko huu huendelea baada ya warithi nao wanapokwenda kuwekeza sehemu nyingine mbayo nayo pindi mrithi atakapofariki, warithi wake nao watauza na kugawana jasho lake.

Lakini pia kwa warithi ambao wanaamua kugawana baadhi ya vyumba na kuchukua kodi kila mmoja kivyake. Hizi ni nyumba au mali zisizokuwa na mwenyewe. Hukosa usimamizi na matunzo kwa sababu hakuna juhudi za pamoja za kufanyia marekebisho nyumba hizo matokeo yake hubaki kama magofu na kupoteza thamani yake ya awali ambayo ilikuwa nayo kipindi ikiwa na mmiliki mmoja. Mwisho wa siku nao huamua kuziuza kutokana na migogoro baina yao wao kwa wao

MADHARA YA MUDA MREFU
  • Jamii kukosa utajili/mali/ uchumi endelevu hivyo kuathiri uchumi wake na wa nchi kiujumla
  • Jamii kupoteza asili yake, vizazi vijavyo havitakuwa na sehemu ya kurudi kutembelea kwa babu na bibi kwasababu yameuzwa.
  • Kuharibika kwa utaifa na muunganiko wa pamoja na dhana ya umoja.

Jambo hili halikuathiri wengi wa mababu na mababa zetu ndio maaana utakuta kuna kijijini kwa babu na bibi ambapo ndipo wakati wote tukihitaji kurudi tunarudi. Babu na bibi zetu hawakuwahi kuuza mali za wazee wao ndio maana wamekuwa na kwao panapofahamika kwa wakati wote.

SULUHISHO

JAMII IACHE UBINAFSI.

Si kila sheria ni sheria nzuri na si kila utaratibu uliowekwa na mamlaka unafaida chanya kwenye jamii husika.

Kinachowafanya warithi kuikimbilia na kuikumbatia sheira hii ya mirathi ni kwa sababu jamii imekosa upendo wa dhati na mshikamano. Watu wametawaliwa na ubinafsi. Kutaka utambuzi binafsi wa ni vitu au mali gani mtu anazimiliki yeye binafsi.

Jamii imepotoka kwenye mfumo wa umuliki mali wa jumla yaani kwa ukoo. Hakuna tena mashamba ya kina Fulani kwa manufaa ya kina Fulani bali kuna shamba la Fulani yeye binafsi kwa faida yake na watoto wake. Nao watotto wanataka ubinafsi wa sehemu yao peke yao hawataki kufaidika kwa pamoja na watoto wenzao kwa ushirikiano.

WITO KWA SERIKALI.
Natambua nia ya serikali ilikuwa nzuri ilipoweka utaratibu wa kulinda mali za wananchi wake pale wanapofariki. Lakini njia hii imekuwa na madhara makubwa sana na imekuwa upanga wa kuigawa jamii na kuwaathiri kiuchumi.

Natoa wito kwa serikali kupitia wataalamu wa sheria na wadau wake waangalie ni namna gani nyingine inaweza kutumika kulinda mali za marehemu na haki za warithi pale inapotokea bila kufanya mgawanyo kama ilivyo sasa.

NJIA NINAZOPENDEKEZA,
  • Wananchi waelimishwe umuhimu wa kuzisajili na kuzirasimisha mali zao.
  • Warithi wasiruhusiwe kuziuza mali zilizokwisha rasimishwa na marehemu kipindi akiwa hai.
  • Majukumu ya msimamizi wa mirathi yasiwe na ukomo. Msimamizi abaki kuwa msimamizi wa mali hiyo kwa manufaa ya koo ya marehemu na warithi wake.
  • Uwigo wa warithi upanuliwe. warithi iwe ni ukoo husika ili asiwepo mtu binafsi wa kujimilikisha na kuuza yeye binafsi.
  • Mahakama itoe adhabu kali kwa wale watakaokiuka sheria ya kutouza mali ya marehemu.
  • Jamii ijikite katika kuendeleza utajiri na uchumi uliopo badala ya kutegemea kuanza upya kila siku.
  • Sheria ya mirathi ifanyiwe marejeo kurekebisha majukumu ya msimamizi wa mirathi ikiwemo kutomruhusu kugawa mali za marehemu.
  • Wasomi katika kila koo wajifunze kuanza kuzifanyia kazi jamii zao. Koo ni taasisi, kama ina muhasibu, ina mwanasheria watumike kufunga hesabu za matumizi ya mali za marehemu ili kuziendeleza kwa faida ya ukoo mzima.
………………

PINTUZ Mwana Andiko
 
Upvote 1
Back
Top Bottom