Posted Date::3/27/2008
Wananchi wapinga wabunge kuongezewa mishahara
Na Muhibu Said
Mwananchi
SIKU moja baada ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutaka waongezwe mishahara na posho, baadhi ya watu nchini wamepinga madai hayo.
Watu hao wamewataka wabunge kueleza bayana mahali zitakapopatikana fedha za kuwaongezea mishahara na posho, huku wengine wakiwataka kufikiria mara mbili matakwa yao kabla ya kuyawasilisha.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Nestory Ngulla alisema jana anawapongeza wabunge kwa kuona kile ambacho wafanyakazi wamekuwa wakikidai muda mrefu, huku wakipata upinzani mkali kutoka serikalini.
Hata hivyo, alisema wabunge wanapaswa kueleza wapi fedha za kuwaongeza mishahara na posho zitakapopatikana kwani serikali siku zote imekuwa ikishindwa kuwaongeza wafanyakazi mishahara kutokana na bajeti yake kuwa finyu.
"Tunawapongeza wabunge kwa kuona umuhimu wa kudai nyongeza ya mishahara na kwa kuanzisha hoja hiyo. Sasa watuambie pesa zitatoka wapi ili na sisi tuongezwe," alisema Ngulla.
Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Makani alipinga wabunge kuiagiza serikali kuwaongezea mishahara na posho akisema kwamba, hatua hiyo siyo sahihi.
Makani ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa chama hicho alisema wabunge hawapaswi kudai nyongeza ya mishahara kwa kuwa wao si wafanyakazi na kuwataka wafikirie mara mbili madai hayo.
"Wao si wafanyakazi, walitaka Ubunge na Ubunge ni kujitolea. Sasa sidhani kama ni sahihi kuagiza waongezwe mishahara na posho. Wangefikiria mara mbili kabla ya kutoa agizo kwa serikali," alisema Makani.
Naye wakili maarufu nchini, Mabere Marando alisema wabunge kudai nyongeza ya mishahara ni haki yao akisema kwamba, wanastahili wanapaswa kulipwa mishahara kutokana na kazi yao.
Marando alisema ana uhakika fedha za kuwaongeza wabunge mishahara na posho zipo na kwamba, kinachotakiwa ni utekelezaji ili kuwawezesha kutembelea majimbo yao.
"Kama serikali inaweza kuwalipa matapeli Sh152 milioni kwa siku, itashindwaje kuwaongeza wabunge mishahara? Nasema wabunge waongezwe na wafanyakazi waongezwe," alisema Marando.
Wakichangia mada katika Semina ya Bunge iliyofanyika katika Ukumbi wa Dar es Salaam International Conference Centre (DICC) jijini juzi, wabunge zaidi ya 10 kutoka vyama vyote walisema, sasa umefika wakati wa mishahara na posho zao kuongezwa ili kuwaepusha kujiingiza kwenye vishawishi.
Katika mjadala huo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta ndiye aliyeanza kutoa hoja hiyo kwa kupendekeza kwamba, waongezwe mishahara na posho na kisha kuungwa mkono na kila mbunge aliyesimama kuchangia hoja hiyo.