MSHAHARA WA SPIKA, JAJI MKUU WAONGEZWA MARADUFU
Waandishi Wetu
SERIKALI imewaongezea mishahara viongozi wa kisiasa, majaji, wakuu wa mikoa na wilaya kuanzia Julai mwaka huu, huku jaji mkuu na spika wakiongezewa maradufu.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa mshahara wa jaji mkuu na spika, ambao ni viongozi wa mihimili mikuu miwili ya nchi, umepanda kutoka Sh2,760,000 hadi Sh4,850,000 kuanzia mwezi Julai na ongezeko hilo ni sawa na asilimia 75.7
Kwa mujibu wa habari zilizothibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari kutoka mihimili yote ya dola, mshahara wa naibu spika umepanda kwa Sh92,000, kutoka Sh2,080,000 hadi Sh2,172,000 na mbunge kutoka Sh1,840,000 hadi Sh1,921,000, ikiwa ni ongezeko la Sh81,000 kwa mwezi.
Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilillah aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa amesikia kuhusu nyongeza hiyo ya mishahara, lakini hana taarifa rasmi wala namna yoyote ya kuthibitisha, kwa kuwa mishahara hiyo haimuhusu.
"Viwango vya mishahara kwa viongozi wa serikali vinawekwa na serikali, mimi hainihusu hivyo siwezi kuthibitisha hilo. Nimesikia tu kama mlivyosikia ninyi," alisema Dk Kashilillah alipotakiwa na gazeti hili kuthibitisha ongezeko la mishahara ya wabunge.
Katika viwango hivyo vipya vya mishahara ambavyo Mwananchi imefanikiwa kuviona, jaji wa Mahakama Kuu ameongezewa mshahara kutoka Sh2,160,000 hadi Sh3,645,000, ikiwa ni ongezeko la Sh1,485,000 huku jaji wa Mahakama ya Rufaa ameongezewa Sh1,940,000 (kutoka Sh2,310,000 hadi Sh4,250,000).
Vyanzo vimeeleza kuwa mshahara wa waziri umepanda kwa Sh102,000 (kutoka Sh2,320,000 hadi Sh2,422,000) na mshahara wa naibu waziri umepanda kutoka Sh1,960,000 hadi Sh2,046,000, ikiwa ni ongezeko la Sh120,000.
Mkuu wa mkoa, ambaye anapata mshahara wa Sh2,172,000, sasa atalipwa Sh2,080,000 na mkuu wa wilaya amepandishiwa mshahara wake kutoka Sh1,840,000 hadi Sh1,921,000 kwa mwezi.
Vyanzo hivyo vya habari vimedokeza kuwa viwango hivyo vipya vya mishahara, havijumuishi posho za vikao, mafuta ya gari na fedha za kujikimu.
Habari zinaeleza kuwa jaji mkuu anapata posho ya madaraka ya Sh6 milioni kwa mwaka na jaji kiongozi anapata posho ya Sh3 milioni, kwa mujibu wa viwango hivyo vipya.
Majaji 70 wanapata posho ya simu na umeme inayofikia Sh 386,400,000 kwa mwaka na posho ya mavazi ya Sh35 milioni kila mmoja.
Habari zinadokeza kuwa majaji 70 wametengewa lita 100 za mafuta ya gari kwa juma, lita moja imekadiriwa kugharimu Sh1,500 hivyo kupewa Sh600,000 kwa wiki ambayo ni sawa na Sh504 milioni kwa mwaka.
Moja ya vyanzo vyetu vya habari kilidokeza kuwa nyongeza hiyo ni ya kawaida ambayo inaenda sambamba na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma, ingawa mwaka huu kwake imeonekana kuwa kubwa zaidi.
"Hili ni kweli; mishahara yetu imeongezwa kuanzia Julai, lakini sisi tulidhani ni nyongeza ya kawaida inayoenda sambamba na nyongeza ya mishahara ya watumishi wengine wa umma, lakini ukweli mambo ni mazuri zaidi," alisema.
Akiwasilisha hotuba yake kwa mwaka 2000/2010, waziri wa Nchi, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma, Hawa Ghasia alisema serikali inatarajia kutumia Sh1,774 trilioni kugharamia mishahara kwa watumishi wa umma,
Fedha hizo pia zitatumika kulipa mishahara kwa watumishi waliopo kazini, ajira mpya, upandishaji vyeo watumishi, kulipia madai ya malimbikizo na mapunjo ya mishahara ya watumishi wa umma nchini.
"Serikali itaendelea kuhakikisha watumishi wake wanapandishwa vyeo na kurekebishiwa mishahara yao ipasavyo," alisema Waziri Ghasia wakati akiwasilisha makadirio ya wizara ambayo wabunge waliyapitisha bila marekebisho.
Suala la mishahara hiyo mipya limekuwa siri kubwa hasa ikizingatiwa kuwa wakati wa bajeti ya serikali ya mwaka huu, waziri mwenye dhamana hakuweka bayana viwango vipya vya mishahara ya watumishi wa umma.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zilisema kuwa serikali hivi sasa iko katika mkakati muhimu wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wenye taalumu ili kuzima wimbi la wasomi kukimbilia nyadhifa za kisiasa.
"Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia madaktari na wanataaluma wengine wanaacha taaluma zao wanakimbilia ubunge kwa sababu anaona labda atateuliwa kuwa waziri na maslahi ni mazuri,¡"kilidokeza chanzo chetu cha habari.