JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Mikataba mbalimbali ya kimataifa, bara na kanda inalinda tasnia ya habari, waandishi wa habari, na watetezi wa haki za binadamu kutoingiliwa na Serikali. Mikataba hiyo inaweka wajibu kwa Serikali kufuata, kuendeleza, na kulinda uhuru wa kutoa maoni na kujieleza.
MIKATABA YA KIMATAIFA TAMKO LA KIMATAIFA LA HAKI ZA BINADAMU (UDHR)
Kifungu cha 19 cha Tamko hilo kinasema: Kila mtu ana haki ya uhuru wa kutoa maoni na kujieleza; haki hii pia inahusisha uhuru wa mtu kuamini katika maoni yake bila kuingiliwa kwa namna yoyote, na uhuru wa kutafuta na kusambaza taarifa, maoni na mawazo yake kwa njia yoyote bila ya kujali mipaka.
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) Tanzania imeridhia mkataba huu mwaka 1976, na hivyo inawajibika kisheria kufuata masharti ya mkataba huo.
Kifungu cha 19 cha mkataba huo kinazungumzia uhuru na haki ya kujieleza:
1. Kila mtu atakuwa na haki ya kuwa na maoni na kuyaamini maoni hayo bila ya kuingiliwa kwa namna yoyote.
2. Kila mtu atakuwa na haki na uhuru wa kujieleza; haki hii itahusisha mtu kutafuta, kupokea, na kusambaza taarifa na mawazo ya aina mbalimbali, kwa njia ya mdomo au maandishi, na bila ya kujali mipaka, kwa kuandika au kuchapisha, kwa njia ya sanaa, au njia nyingine yoyote atakayoichagua.
3. Utekelezaji wa haki zilizoainishwa kwenye aya ya 2 ya kifungu hiki kinaendana wajibu na majukumu maalum.
Kwa hivyo, haki hiyo inaweza kuhusisha vikwazo mbalimbali, hata ambavyo ni vya muhimu na vitawekwa kwa mujibu wa sheria:
(a) Vinavyolenga kulinda haki na heshima ya watu wengine;
(b) Vinavyolenga kulinda usalama wa nchi au utulivu wa kijamii, au afya na maadili ya jamii.
Haki ya uhuru wa kujieleza inahusisha kuchambua, kujadili kwa uwazi, kutoa kauli zinayoweza kukwaza, kushitua, kusumbua na kukosoa wengine.
Upvote
1