The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Mitandao ya kijamii imerahisisha sana uwepo wa majadiliano ya mtandaoni kuhusu masuala yoyote yanayoigusa jamii husika. Mitandao imekuwa ni uwanja wa kutafuta suluhu za matatizo ambayo jamii inakumbana nayo, lakini pia imekuwa kijiwe ambapo watu hubadilishana mawazo na pengine kupeana mbinu mbalimbali za kujikwamua katika changamoto binafsi za kiuchumi, kiafya n.k.
Kuna mambo mengi ambayo watu wanajifunza kwa kuwa kwenye mitandao ya kijamii. Iwe ni habari kuhusu uvumbuzi mpya, au kuhusu historia na burudani. Mitandao ya kijamii hutusaidia kujifunza mambo mapya ambayo yana faida kubwa kwetu kama watu binafsi. Sio tu kwamba watumiaji wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kuongeza uelewa na ufanisi wao katika mambo fulani, lakini pia wanaweza kupata fursa za kujikwamua kiuchumi.
Katika uwanja wa kidemokrasia, mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika kama nyenzo muhimu sana katika kupaza sauti zao kwa mamlaka, kuibua ubadhirifu, rushwa na uhujumu uchumi. Ni nyenzo inayochochea uwajibikaji na kuifanikisha dhana ya utawala bora.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wake huo mitandao ya kijamii imekuwa ikipitia changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa namna moja au nyingine wananchi wa mataifa mengi wamekuwa wakinyimwa fursa ya kutumia mitandao hiyo kwa sababu mbalimbali.
Mnamo 2021, kwa mfano, serikali za Nigeria na Uganda kila moja ilichukua hatua kwa kulipiza kisasi dhidi ya mitandao ya kijamii baada ya majukwaa hayo kuondoa machapisho ya viongozi fulani na wafuasi wao kwa kushindwa kutimiza masharti ya matumizi ya mitandao hiyo.
Hata hivyo, hali bado ni tete kwenye maeneo mengine mengi. Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Access Now inayoitwa Weapons of control, shields of impunity: Internet shutdowns in 2022, Mtandao wa Twitter ulizuiliwa mara 13 katika nchi 11 huku Facebook ikizuiliwa mara 13 katika nchi 12. Mtandao mwingine wa Instagram ulizuiliwa mara 10 katika nchi 9 huku WhatsApp ikipambana na changamoto hizo mara 10 katika nchi 9.
Google Services nayo haikuachwa salama kwani yenyewe ilizuiliwa mara 9 katika nchi 8 huku Telegram ikikutana na rungu hilo mara 8 katika nchi 6. TikTok ilizuiliwa mara 4 katika nchi 4, wakati IMO messenger ikifungiwa mara 2 katika nchi 2 na Signal ikipotezwa hewani mara 5 katika nchi 4. WeChat na Clubhouse zote zilifungiwa mara 2 kila moja katika nchi 2.
Hatua hizo zilizochukuliwa dhidi ya mitandao hiyo inaonesha wazi kuwa bado viongozi wengi duniani wana uoga wa uhuru wa maoni. Hawapo tayari kuwajibishwa na kuna mashaka ya kuwa wanapata shida na mtiririko wa taarifa ambao unamulika matendo yao katika jamii.
Hata hivyo, mitandao ya kijamii haipaswi kuwa adui wa serikali na mamlaka, inapaswa kuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa sera zao na kukaribiana na wananchi. Ni muda sahihi kwa viongozi kuona mitandao ya kijamii kama kioo cha uongozi wao kwa wananchi.
Katika siku zijazo, tunatarajia viongozi wengi zaidi kukumbatia aina hii ya utawala wa uwazi kwa kuwa inakuwa rahisi kwao kuchangamana na wapiga kura wao, tofauti na zamani wakati wanasiasa na viongozi wa serikali walilazimika kusafiri ili kukutana na wananchi. Sasa hivi ukumbi wa mikutano ya hadhara ni mtandaoni.
Kwa wananchi mitandao ya kijamii inaweza kutoa matumaini ya ukombozi katika tawala za kimabavu kwani inawapa sauti wale ambao hapo awali walitengwa na mijadala ya kisiasa na vyombo vya habari. Mitandao ya kijamii inaruhusu wananchi kuwa chanzo cha mawazo na mipango ya kimaendeleo kwa njia rahisi zaidi kuliko hapo awali.
#KeepItOn