DOKEZO Miundombinu duni yakwaza elimu kwa Watoto wenye ulemavu Mkoani Mwanza

DOKEZO Miundombinu duni yakwaza elimu kwa Watoto wenye ulemavu Mkoani Mwanza

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Mwanza. “Changamoto ya ngazi na vyoo, halafu kuna mawe, kwa hiyo ukienda vibaya unaweza kujikwaa. Katika ufaulu mtu asipofikisha wastani wa 64, anapata viboko, wakati huku mwanzo hajapata vitabu vya kutosha.”

Kauli ya Joasen Julius, mwenye ulemavu wa miguu na kuzungumza, ikiweka wazi uhalisia mchungu unaowakabili wanafunzi wenye ulemavu katika taasisi za elimu mkoani Mwanza.
Picture1.jpg

Moja ya ngazi za kupandia wanafunzi wenye ulemavu katika Shule ya msingi Bulale zikiwa zimeanza kumomonyoka, hali inayohatarisha usalama wao. PICHA: Dominic Allen​
Ngazi zisizopitika, vyoo visivyofikika pamoja na uduni wa vifaa maalum vya kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu hugeuka kuwa vikwazo vinavyohatarisha sio tu usalama bali pia kuathiri ufaulu wao kitaaluma.

Miundombinu isiyo rafiki kwa watoto wenye ulemavu imekuwa tatizo sugu katika baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani Mwanza, hali inayowalazimu wanafunzi hawa kutumia nguvu zaidi ili kupata kile ambacho wenzao wanapata kwa urahisi.

Kutojengwa kwa miundombinu bila kuzingatia viwango vya ufikivu kunakwenda kinyume na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, katika sehemu ya 3.2.1 iliyoweka hakikisho juu ya upatikanaji wa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo, ikiwemo kwa watoto wenye ulemavu.

Picture2.jpg

Ngazi za kupandia katika Shule ya msingi Amina Makilagi, iliyopo Buhongwa jijini Mwanza, zikiwa zimemomonyoka na kuharibika, hali inayowaweka kwenye hatari wanafunzi wenye ulemavu wanaozitegemea kufika madarasani. PICHA: Dominic Allen.
Picture3.jpg

Moja ya majengo ya madarasa katika Shule yasingi St. Benjamin, iliyopo Mwasonge, likiwa halina ngazi au njia maalum ya kupandia kwa wanafunzi wenye ulemavu, hali inayowakosesha urahisi na usalama wa kufika darasani. PICHA: Dominic Allen.
​
Vifungu vya 27 na 28 vya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 vinalinda haki yao ya kupata elimu bila ubaguzi, ikisisitiza kuwa wanapaswa kufurahia fursa sawa za kielimu kama raia wengine wote.

Hata hivyo, licha ya sera kuweka matumaini katika mioyo ya watoto wenye ulemavu, hali halisi katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Nyamagana, Ilemela na Misungwi, inakinzana na ahadi hizo.

Simulizi ya mateso
Joasen Julius ambaye ni kijana mwenye ulemavu wa miguu na kuzungumza, mkazi wa Bulale, kata ya Buhongwa jijini Mwanza amesema baadhi ya wanafunzi walemavu wana changamoto ya uelewa kulinganisha na wanafunzi wengine, hivyo hujikuta wakiachwa nyuma darasani.

“Watu wenye ulemavu wanapata changamoto ya uelewa, kwa sababu mwalimu akija ubaoni atafundisha, yaani atajumulisha, hakuna cha sijui huyu ni mlemavu hajaelewa, huyu anataka kufafanuliwa, hata kuandika unakuta mwingine anaandika polepole,” amesema Julius.

Julius pia amezungumzia adhabu za ukatili bila kujali hali walizonazo.

“Mtu mwenye ulemavu wa mikono anaweza akawa ana akili lakini akashindwa jinsi ya kusoma kwa bidii kutokana na kuchelewa kumaliza kuandika, lakini bado anaadhibiwa bila kujali haki yake,” anazungumza kwa masikitiko ya Julius.

Ameizungumzia pia changamoto ya umbali wa ilipokuwa shule anayosoma na kufikika kwa madarasa kwa wanafunzi wenye ulemavu, akieleza kuwa imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wenye ulemavu kupata haki ya elimu.

“Unaweza kukuta muda mwingine barabara inajaa maji, ukiteleza, madaftari yanaanguka, yakishaanguka kwenye maji yanaloana, kwa hiyo ni changamoto,” amezungumza Julius.

Athari za kiafya
Abdulrahman Lugone, Mweka Hazina mstaafu wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), amesema baadhi ya watoto wenye ulemavu wamejikuta wakiathirika kiafya kutokana na kutojengewa vyoo maalum kwa ajili yao, hali inayowalazimu kuchangia vyoo na wanafunzi wasio na ulemavu.

“Wanaathirika kiafya, kwa sababu kuna maradhi kama vile UTI, wanaambukizwa kwa njia hiyo, na maradhi yote ambukizi ambayo yanatokana na mazingira machafu ambayo mtoto mwenye ulemavu anayetambaa yanaweza kumuathiri,” amezungumza Lugone.

Mtaalam wa masuala ya afya, Joyce Lukumay, ameeleza kuwa ni kweli watoto wenye ulemavu wapo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya mlipuko na maambukizi kutokana na kukosekana kwa vyoo maalum kwa ajili yao.

“Ni lazima wapate madhara, wanapata maambukizi, magonjwa ya kuambukiza ya mlipuko, kuna kipindupindu, homa za matumbo,” ameeleza Lukumay.

Katika wilaya ya Ilemela, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, wilaya hii ina jumla ya shule za msingi 130, kati ya hizo 76 ni za serikali na 54 ni za binafsi, huku shule za sekondari zikiwa ni 54, kati ya hizo shule 32 ni za serikali na shule 22 ni za binafsi.

Wadau
Abdulrahman Kange, Diwani wa kata ya Nyamanoro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema kuwa miundombinu katika shule za msingi katika kata hiyo sio rafiki sana, kulingana na mahitaji maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu ili kupata elimu bora, sawa na wanafunzi wengine.

“Ni rafiki (miundombinu), lakini si rafiki sana, kwa sababu kutokana na mazingira ya mahitaji ya vifaa vyao katika shule zetu,” ameeleza Diwani Kange, huku akizitaja shule ya Mwenge na Karume kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu, ikiwemo vifaa vya kujifunzia pamoja na walimu maalum kwa ajili yao.

“Kwa shule zetu za Mwenge na Karume hali yao ni zuri, kwa sababu walimu hao wapo na wanafunzi hao wapo, na wanaendelea kupata taaluma kupitia walimu wetu. Kwa hiyo, kimsingi hapo ni sehemu ambayo ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,” amezungumza Diwani Kange.

Magege Hailala Magege, mkazi wa Kata ya Nyamanoro, ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Ilemela, amesema baadhi ya shule katika wilaya hiyo ziko katika maeneo ya milimani, hivyo ni ngumu kufikika kwa urahisi kwa wanafunzi wenye ulemavu, hivyo kuwanyima fursa ya elimu wanafunzi hao.

“Miundombinu sio rafiki kwa watoto wenye ulemavu, kwa kuwa baadhi ya shule zipo milimani, kwenye miinuko ya milima, hapajatengenezewa miundombinu ya kufika shuleni. Shule ya sekondari ya Nyamanoro ipo juu ya mlima, shule ya msingi ya Ibungilo ipo juu ya mlima na sehemu hizo hakuna usafiri wa moja kwa moja,” ameeleza Magege.

Magege akiwa ni mkazi wa Ilemela kwa takriban miaka 40, amesema kutokana na idadi chache ya wanafunzi wenye ulemavu katika baadhi ya shule wilayani hapo, kwa muda mwingi vyoo vyao huwa vimefungwa ili kuepuka kuchafuka na kuharibika, jambo ambalo linapelekea wanafunzi hawa kutumia vyoo vya jumuiya.

“Baadhi ya vyoo vipo vya watoto wenye ulemavu, lakini kwa muda mwingi vinakuwa vimefungwa mara nyingi ili kukiepusha visiharibike au visichafuke, wanavifunga,” amezungumza Magege.

Kwa mtazamo wake Magege, kutokuwepo kwa mazingira rafiki katika shule za msingi za msingi na sekondari kumekuwa na chanzo wanafunzi hawa kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.

“Athari ni kubwa, kwa sababu maendeleo ya shule (wanafunzi wenye ulemavu) yanategemeana na mazingira, sasa wanapokutana na sehemu ambayo haina mazingira rafiki, uwezo wa kukaa na kushika yale wanayofundishwa unakuwa ni mdogo,” maoni ya Magege.

Baadhi ya wakuu wa shule walikataa kutoa taarifa za shule zao wakitaka kibali cha Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza.

Hata hivyo, hadi makala hii inachapishwa, Land Dwellers ilikuwa imefanya jitihada za kuwasiliana na ofisi ya Mkurugenzi kwa ajili ya kupata kibali hicho, lakini hakukuwa na mafanikio.

Katika mkoa wa Mwanza, takwimu zilizotolewa mwezi Januari, 2025 na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, idadi ya watu wenye ulemavu kwa mkoani hapa ni 10,896 ambapo kati ya hao wenye ulemavu wa viungo ni 5,362 wenye ulemavu wa macho 1,416 viziwi ni 1,862 huku wenye matatizo ya afya ya akili ni 2,004 na mwenye ualibino ni 609.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mkoa, Mwanza ina shule za msingi 914, huku shule za sekondari zinazotoa elimu kuanzia ngazi ya kidato cha kwanza hadi cha nne zikiwa ni 25. Licha ya uwepo wa shule hizi, changamoto za kukosekana kwa miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu zinatajwa kuwa jinamizi linalozikumba.

Ripoti
Kwa mujibu wa takwimu za "Mapitio ya takwimu za watu wenye ulemavu yaliyomo kwenye ripoti ya Tathmini ya hali kuhusu haki za watu wenye ulemavu – Tanzania (2021/22) imeeleza kuwa, kiwango cha watoto wenye ulemavu nchini Tanzania wanaokamilisha elimu ya msingi ni asilimia 49 ikilinganishwa na asilimia 83 ya watoto wasio na ulemavu.

Ripoti hiyo imesema shule na madarasa mengi hayafikiki kwa wanafunzi wenye ulemavu kutokana na umbali na usafiri usio rafiki, miundombinu ya shule ikiwemo vyoo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mbinu mbadala za mawasiliano, pamoja na ufadhili mdogo au kipaumbele kidogo cha kugawa fedha kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa miundombinu shuleni.

Pia, ripoti ya “Ujumuishwaji wa watoto wenye ulemavu sio anasa ni haki” ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ya mwaka 2021 imebainisha kuwa kote duniani, mtoto mmoja kati ya 10 ana ulemavu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto wenye ulemavu wanakosa fursa ikilinganishwa na watoto wasio na ulemavu katika hatua nyingi za ustawi wa wao, ambapo wanakosa mahitaji ya msingi ikiwemo afya, elimu na ulinzi.

Makumba Mwemezi, ambaye ni Mkuu wa idara ya utafiti, ubunifu na uchambuzi wa sera kutoka shirika la HakiElimu, amesema shule zote zinatakiwa kuwa na miundombinu ambayo inaweza kuwapokea watoto wote kulingana na uwezo wao.

“Shule zote zinapaswa kuwapokea kulingana na uwezo wao. Uwezo wao kwa maana ya maumbo, uwezo wa kufika au kutofika, na mambo mengine,” amefafanua Mwemezi.

Mwemezi ameeleza kuwa suala la changamoto za miundombinu kwa upande wa wanafunzi wenye ulemavu ndiyo kubwa zaidi, kwani shule nyingi hujengwa bila kuwepo na mazingira wezeshi ya kuwafanya wanafunzi hao kupata haki ya elimu jumishi na bora.

Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi, ACT Wazalendo Taifa, Mbarala Maharagande, anaona suala la bajeti kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu bado halijapewa kipaumbele ipasavyo.

“Bajeti ya nchi haijatoa kipaumbele katika eneo hilo. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya 2024/25 ameonesha kwamba kuna matumizi yasiokuwa ya lazima shilingi za Kitanzania bilioni 347. Kwa hiyo, bado changamoto iliyopo vilevile ni serikali kutotoa kipaumbele kinachostahiki na kutofanya matumizi mazuri ya rasilimali zetu,” amezungumza Maharagande.

Andiko la: Dominic Allen
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.

Pia soma ~ Pengo la uwajibikaji na changamoto ya miundombinu kwa watoto wenye ulemavu katika shule za Mwanza
 
Back
Top Bottom