JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
JamiiForums kwa kushirikiana na Kituo cha Runinga cha StarTV, itaendesha Mjadala kuhusu Nafasi ya Vyombo vya Habari na Waandishi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024
Mjadala huo utakaoongozwa na Mtangazaji Edwin Odema 'Chief Odemba', utahusisha Waandishi wa Habari na Watangazaji wakiwemo Masoud Kipanya, Salim Kikeke, John Marwa, Salome Kitomari, Khalifa Said na Gerlard Hando ambapo watachambua, kutafakari na kujadili kuhusu Uhuru wa Habari katika Uchaguzi
Mjadala utakuwa Mubashara kuanzia Saa 3:00 Usiku hadi Saa 5:00 Usiku.
Wananchi wote mnakaribishwa kuwasilisha maswali anuai mliyonayo kuhusu mjadala huu ambapo maswali hayo yataulizwa moja kwa moja kwa Washiriki wakati wa majadala huu
PIA SOMA
- Kuelekea 2025 - LGE2024 - Wajibu Wa Vyombo vya Habari katika Uchaguzi
==========================
MAONI YA WACHANGIAJI WALIOPO KWENYE MJADALA
Khalifa Said - Mwandishi na Mhariri wa The Chanzo, amesema;
"Mimi nadhani jibu la swali lako ni NDIO, tumepoteza ushawishi kwenye mitazamo ya Wananchi na watu ambao tunawahudumia hawaoni Waandishi wa Habari au Vyombo vya Habari vikitumikia maslai yao. Wananchi wanahiyo dhana, wanahiyo picha kwamba vyombo vya habari na waandishi wa habari hawapiganii maslai ya wananchi, vimejikita kutetea maslai ya viongozi au wawakilishi wa tabaka tawala."
"Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana ya kisheria na kikanuni, mazingira ambayo yanavilazimisha vyombo vya habari viache kutimiza dhima yao yakuiwajibisha serikali na badala yake vinakuwa visemeo vya serikali."
"Tuna sheria ngumu, kanuni kali lakini pia kuna practices ambazo hazipo hata kwenye sheria na kanuni lakini zinachangia kwenye kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari."
"Suala la pili ni uwezo wetu sisi kama Wanahabari katika kuchambua, kufichua mambo ni mdogo, ukiangalia kwenye chombo cha habari kuchambua mambo hakuridhishi, na picha inajengeka kwenye mitazamo ya wananchi kwamba sasa hivi hawana ule ushawishi."
John Marwa - Mwanahabari wa Jambo Online Media, amesema;
"Unatishiwa na watu ambao hawapendi habari unazoandika. Wanaweza kuwa watu binafsi, sekta binafsi, au hata watawala, kwa sababu habari hizo zinaweza kuwanyima maslahi yao ya kiuchumi, kibiashara, au kiuongozi."
"Kwa mfano, ukimwandika mfanyabiashara anayekwepa kodi, utapata vitisho kwa sababu wana nguvu za kiuchumi na wanaweza kukufanyia lolote. Vivyo hivyo, ukiandika kuhusu mienendo isiyo sawa ya viongozi wa serikali, unaweza kushughulikiwa kwa sababu wana nguvu za kiuchumi au kisiasa."
"Katika mazingira haya, waandishi wanajikuta wakihofia usalama wao na kuchagua kuandika habari za kusifia (PR Stories) ili kuepuka migogoro. Hii ni changamoto, hasa tukiona waandishi waliowahi kuandika habari za maslahi ya jamii walivyokumbana na matatizo makubwa."
"Jambo jingine ni kujipendekeza (uchawa). Waandishi wa habari wanapojipendekeza kwa kundi fulani, iwe kundi linalotawala au kundi la wafanyabiashara, na kuwapa sifa, ambako wana amini wanaweza kupata maslahi ya kiuchumi au nafasi za kipekee. Kwa hali hiyo, wanakuwa wamesahau kabisa jukumu lao la kuandika habari zinazowahusu wananchi na badala yake wanachagua kuandika habari ambazo zinalingana na matakwa ya watu walio madarakani."
"Kuna watu tumewaona, waandishi wenzetu waliokuwa kwenye newsroom, waliandika mambo ya kujipendekeza na matokeo yake walipata vyeo au dili za kiuchumi zilizobadilisha maisha yao. Hii ni changamoto kubwa kwa uandishi wa habari unaolenga maslahi ya jamii."
Salome Kitomary - Mhariri wa Gazeti la Nipashe, amesema;
"Mimi naona ni 50/50. Kwanini naona hivyo? Ili kupata matokeo sahihi ya jambo unalolizungumzia, lazima utafiti ufanyike. Tunaposema waandishi wa habari tumepoteza ushawishi, tunapaswa kuwa na ushahidi wa utafiti unaothibitisha hilo."
"Kuna mambo mengi yameikumba tasnia ya habari, si Tanzania pekee bali duniani kote. Kwa mfano, ukisema leo hii magazeti hayasomeki, si tatizo la Tanzania peke yake; hata duniani kote hali ni hiyo. Sababu kubwa ni kasi ya ukuaji wa teknolojia, ambayo imeleta mabadiliko makubwa na kutulazimisha kuikubali teknolojia kama sehemu ya kazi zetu."
"Habari nyingi ambazo zimekuwa zikishinda kwenye mashindano mbalimbali ni zile zinazochochea mabadiliko katika jamii. Hivyo, tunapozungumzia dhana ya kushuka kwa ushawishi wa waandishi wa habari, tunapaswa kuzingatia muktadha wa eneo husika na upande tunaouangalia."
"Pamoja na changamoto hizi, kuna umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari kuhakikisha wanatoa haki sawa kwa watu wote. Kwa mfano, katika kipindi hiki cha uchaguzi, ni wajibu wa vyombo vya habari kuripoti taarifa za vyama vyote kwa usawa na uwazi."
Gerald Hando - Mwanahabari, Wasafi Media, amesema;
"Kuna haja kubwa ya vyombo vya habari kuwa makini katika kuripoti habari ili kuepuka taarifa potoshi, hasa wakati huu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025."
"Nipongeze JamiiForums kwa mchango wake wa kufungua macho ya watu na kusaidia kuepusha upotoshaji wa taarifa zisizo za kweli. Katika kipindi hiki cha uchaguzi, kumekuwa na wimbi la habari nyingi za kupotosha, na kukosekana kwa sehemu ya kupata taarifa sahihi kunaweza kuwa changamoto kubwa."
"Ni jukumu la kila mwandishi wa habari mmoja mmoja pamoja na vyombo vya habari kutambua changamoto hii na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha wananchi wanapata habari za kweli na zenye usahihi."