Kabla ya kulima wewe unataka mpunga wa nini?, kufanyia biashara (kuuza) , au kula mwenyewe na familia yako tu. Kama nusu biashara nusu matumizi ya nyumbani, cha kufanya ni lazima ujue katika eneo lako aina gani ya mpunga unaopendwa na walaji.
Aina za mpunga zipo nyingi ila kuna mbegu ndefu na mbegu fupi
Mbegu ndefu
- super Shinyanga, super mbeya, super Kilombero (super india) hizi hotofautiana majina kutokana na mikoa ila wengi huzitambua kwa sifa zake
- mbawa mbili, pamba ( huwa nyeupe kabisa) kitumbo, n. k
Mbegu fupi
- sallo S5 ( hufanana kidogo na super), salo chekechea, sali 360 n. k zipo nyingi sana
MAANDALIZI
Inategemea na ukanda wenu lkn kwa Morogoro huandaa shamba baada ya kuchoma majani na kuja kulima kuanzia mwezi wa 11 mwishoni hadi wa 12. Majani yanapoanza kuota yakiwa mateke piga dawa aina ya Round up ( hufanya kazi kwa siku 21) au dudusate ( hufanya kazi kuanzia siku 15) au dynasate au kiua magugu kizuri. Kama mfuko wako unakidhi unaweza ukalima tena ili kupunguza ng'olezi ila kama hautoshelezi inatosha kwa hapo
KUPANDA
Mbegu za mpunga mrefu humwagwa kwa kutawanywa na trekta hufukia. Mbegu ya salo unaweza ukamwaga na kufukia kwa trekta au kuotesha kitaru kisha kupandikuza japo ya kitaru inagharama kubwa ila mavuno mengi pia.
PALIZI
Hapa wakati mpunga umeanza kutoka una kama mwezi unakuwa umeshika udongo vizuri unaweza ukapiga dawa aina ya 2 4D ukichanganya na Rice paddy au kuna dawa inaitwa white gold nadhani jina limenitoka huuzwa bei ghali kidogo kama 50,000 hivi hii. Kisha unakuja kuokoteza baadhi ya majani machache tu shambani.
Baada ya hapo kwa mikoa mingine huamia ndege ila kwa mikoa mingine baadhi ya pande za Ifakara huwa hawana usumbufu wa ndege
KUVUNA
Mpunga mzuri huvunwa ukiwa nyama nono yaani kabla ya kukauka sana na gharama za uvunaji hutegemeana na eneo / mkoa husika
. Mpunga mrefu kuna uwezekano wa heka moja kama umehudumia vizuri ikatoa gunia 9 hadi 12 ya debe saba na gunia 7 hadi 10 za debe 10 kwa heka
Mpunga mfupi wa salo unaweza ukatoa gunia 20 hadi 30 kwa heka kwa gunia la debe saba
MAUZO
inategemea soko lako ulilolenga kama mwezi wa 12 gunia huuzwa kwa bei ya Tsh 100,000 /=, lakini unaweza ukakoboa gunia la debe saba na kutoa kilo 60 hadi 67 na kuuza mchele kwenye mashine kwa bei za jumla ambapo mwezi wa 12 kilo huwa Tsh 1600, 1800 hadi 2000
CHANGAMOTO
Kuna magonjwa ambayo husababishwa na ufinyu wa mvua kama serenge, ugonjwa wa mabaka baka, kama unalima kilimo shadidi kupambana na panya, na mpunga kukosa madini ya nitrojeni kwa wengine huweka mbolea au kupiga booster ya maji pale wanapoona mpunga umeanza kudumaa.