JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Wakuu, leo Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na JamiiForums tutashiriki mjadala muhimu utakaohusu Mbinu za Kukomesha Ukatili na Mauaji ya Wenza.
Mjadala huu unalenga kutoa elimu, kuongeza uelewa, na kuchochea hatua za pamoja katika kukabiliana na changamoto hii ya kijamii. Tunakaribisha maoni na maswali kutoka kwenu ili kufanya mjadala huu kuwa wa kina na wenye tija.
Wazungumzaji wetu wa leo ni pamoja na: Dkt. Anna Henga - Mkurugenzi Mtendaji, LHRC; Mchungaji Richard Hananja; Dkt. Rose Reuben - Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA; Dkt. Pascal Kang'iria - Mratibu wa Afya ya Akili, Arusha; Rehema Maro - Mkuu wa Programu, WiLDAF Tanzania.
Mjadala utaongozwa na Wakili Getrude Dyabene,. Tunaamini kuwa majadiliano haya ni hatua muhimu katika kujenga jamii salama na yenye kuheshimiana.
Karibuni sana kushiriki na kuchangia kupitia link hii: x.com
====
Dkt. Rose Reuben, TAMWA
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben amesema kuwa pamoja na ripoti na taarifa za Ukatili zinazotajwa kwenye Vyombo mbalimbali, bado kuna matukio mengi ya Ukatili yanayosikika chini kwa chini na hayaripotiwi
Ameongeza kuwa, jambo lingine linalochangia Ukatili ni inapotokea wenza wameshindwana na kisha kuanza kushindana, ambapo upande mmoja unaweza kuamua kufanya jambo baya ili tu kumkomoa mwenzake, hivyo kuwa kama adui
Amesema "Ugomvi huo unaweza kwenda mbali na kuathiri hata Watoto kama wapo, majirani, ndugu au kazini na hivyo kuathiri Utendaji wa yule hasa anayefanyiwa Ukatili"
Dkt. Pascal Kang’iria
Dkt. Pascal Kang’iria amesema Jamii inapaswa kujiuliza kuwa siku hizi kuna taarifa nyingi za matukio ya Ukatili, Je, ni kwamba uwepo wa Mitandao na teknolojia imesababisha upatikanaji wa taarifa kwa urahisi au ni kwamba matukio hayo hayakuwepo na sasa yanaanza kuibuka?
Amesema "Pia inawezekana taarifa nyingi za Matukio ya Ukatili zinaweza kuwa zinachangiwa na mwamko wa Watu kuwa na uwezo wa kuzungumza tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma"
Wakili Getrude Dyabene
Wakili Getrude Dyabene amesema "Sheria haitambui kuhusu #Ubakaji ndani ya Ndoa, lakini kuna matukio mengi ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakitokea kwa pande zote, kwa maana ya Wanaume na Wanawake"
Ameongeza kwa kusema kuwa kuna umuhimu wa #Sheria kuangalia hilo, kwa kuwa halizungumzwi lakini lipo na kumekuwa na wengi wanaoumia
Wakili Dyabene amesema "Katika Sheria zetu tumekuwa tukiomba Serikali iweke Sheria maalum ya Ukatili, kwa kuwa kuna mapungufu kadhaa katika Sheria zetu"
Ameongeza kwa kusema kuwa kuna ukatili unaohusiana na masuala ya Teknolojia, (Cyber Crime Act) lakini ni vema kukawa na Sheria moja kwa moja inayogusia #Ukatili
Aidha, amesema kuwa inatakiwa mtu anapotoa taarifa au kushtaki kuhusu Ukatili kuwe na nafasi ya kumuweka Mwathirika sehemu salama pale inapobidi.
Mdau
Hassan Kayungi (Mdau) amesema kuwa jambo lingine linalochangia Ukatili ni matarajio
Amesema "Unaweza kukuta mtu anaingia katika Ndoa na kukutana na kitu ambacho sicho alichokitegemea, anaanza kutafuta njia mbadala ambayo inaweza kuwa siyo nzuri kwa Mwenza wake"
Ameongeza kuwa Changamoto ya Afya ya akili inaweza kuchangia ukatili akitolea mfano kwa Wanaume anaweza kuwa na vitu moyoni, hana nafasi ya kuzungumza na aporejea nyumbani anakuwa hayupo tayari kupokea kile ambacho mwenza wake anakifanya kama vile kuongea sana