Mjomba akaiharibu siku

Mjomba akaiharibu siku

Mtambuzi

Platinum Member
Joined
Oct 29, 2008
Posts
8,809
Reaction score
15,421
Ilikuwa ni mwaka 1987, wakati huo nilikuwa naishi na kaka yangu mkubwa maeneo ya Kinondoni Msufini. Basi siku moja asubuhi tukapata mgeni na hakuwa mwingine bali ni mjomba wetu ambaye alikuwa ni dereva wa malori makubwa huko Arusha. Sasa ilitokea kapata safari ya kuleta mzigo huku Dar na ndipo alipokuja kututembelea.Huyu Mjomba alikuwa na mdogo wake aliyekuwa akiishi Ilala na shughuli zake zilikuwa ni Kushona nguo pale pale Ilala. Lakini kwa bahati mbaya hakujua alipokuwa akiishi mdogo wake, hivyo kaka akanitaka nimpekele mjomba kwa mdogo wake, kisha nirudi naye kwa sababu atalala hapo nyumbani.

Tulipofika Ilala kwa mjomba mdogo, tukamkuta akikoboa Mahindi ya makande kwa kutumia kinu, na mkewe alikuwa amekaa na mashoga zake hapo hapo uwani wakisukana. Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Jumapili.Mjomba alifurahi sana kumuona kaka yake na alitukaribisha ndani na kutuagizia soda, na kisha akatoka zake nje kuendelea kukoboa mahindi. Mkewe aliingia ndani na mashoga zake na kututambulisha kwao kisha akatoka kuwasindikiza.

Baadae alirudi na kundelea na shughuli za ndani huku mumewe akindelea kukoboa mahindi huko nje. Alipomaliza alimkabidhi mkewe yale mahindi ali ayabandike jikoni halafu akamuomba kaka yake tutoke kidogo kunyoosha miguu.Tulienda kwenye baa moja iliyokuwa mtaa wa pili, kwa ajili ya kupata moja moto moja baridi, kwa kuwa sinywi pombe niliagiza soda.

Mjomba na mdogo wake waliagiza bia na kuanza kunywa huku wakipiga soga na kupeana habari za nyumbani.
Kumbe mjomba mkubwa alikuwa na dukuduku lake na pombe zilipomuingia ndipo akaanza kumpasha mdogo wake.‘Bwana mdogo unajua unajua unanitia aibu, tena umenidhaliisha sana, yaani huyu Mzaramo wako amekutawala mpaka basi, hivi kweli wewe ni wa kukoboa mahindi na mkeo amekaa na mashoga zake wakisukana na kuchapa umbeya?' Mjomba alianza kumfokea mdogo wake.

Mjomba mdogo alitaka kumjibu lakini akamkata kalma na kumuonya asidhubutu kuongea mpaka amalize kuongea yeye…..Basi mjomba akaendelea kumpasha mdogo wake kuwa anadhalilisha ukoo wao na kamwe hatakuja kwake na asije akafunga ndoa na huyo mwanamke kwa sababu hana maadili na hana heshima hata kidogo.

Wakati wote mjomba mdogo alikuwa kajiinamia akimsikiliza kaka yake huku akiendelea kunywa bia moja baada ya nyingine.Nilijaribu kumnyamzisha mjomba, lakini wapi aliendelea kumfokea mdogo wake mpaka akatosheka, ndipo tukarudi nyumbani ili tupate chakula cha mchana kisha tuondoke kurudi Kinondoni.

Tulipofika tu Mjomba mdogo akamrukia mkewe na kuanza kumpiga huku akisema, "Mimi siku zote naishi na wewe kumbe umenitawala mpaka kaka yangu leo amenitolea uvivu na kunisema waziwazi, haiwezekani unitawale kiasi hicho…………….. na leo utanitambua"

Wakati purukushani hizo zinaanza, wote tulishikwa na butwaa kwanza tusijue la kufanya, mara ghafla akaja jirani moja nakuingilia kati, na mjomba mkubwa naye akaanza kuamulia ule ugomvi, lakini mdogo wake aliendelea kubwabwaja yale maneno aliyoelezwa na mjomba mkubwa kule Baa…….. Binti wa Kizaramo naye hakukubali alikuwa akijibu mapigo na kuporomosha matusi akimtukana mjomba mkubwa waziwazi kuwa ni mbeya na mzandiki mkubwa aliyekwenda pale kuvunja uhusiano wao…….. alimwambia kama anadhani kuwa anafaidi basi atamvalisha khanga ili aolewe yeye…………….

Majibizano yalikuwa ni makali na yenye kila aina ya kashfa na matusi ya nguoni yakimuhusisha mjomba mkubwa………………..ilibidi majirani wamuulize mjomba kulikoni anataka kuvunja uhusiano wa mdogo wake na mpenzi wake?

Mjomba hakuwa na la kusema alibaki kimya akiwa ametahayari. Alinishika mkono na kuniambia tuondoke kwani mambo yameharibika.

Majirani walibaki kutuangalia wakati tunaondoka huku wakifyonya…………………. Ilikuwa ni fedheha kwetu
 
Hapo fundisho aache kufuatilia maisha na unyumba wa watu. Akiwakuta wamelala kuelekea kusini awaache hivyo hivyo ni maisha yao na wameyakubali. May be kama aliona jambo baya au angeanza mdogo wake kulalamika hapo sawa. Ila hayo ameyataka mwenyewe
 
Hata hela huwa ni uchafu kama zikiwekwa mahala ambapo hapastahili!
 
Daa kwel ni zaman nlikuwa na mwaka 1 tu.

Nilikuwa na miaka 16 wakati huo.............. tukio hili lilinifundisha kutojihusisha na ndoa au mahusiano ya watu, kwani wao wenyewe wamekubaliana kuishi maisha yao, sasa kwa nini nikereke wakati hayanihusu..............
 
Huyo mjomba alikosa busara kwan mwanaume kumsaidia mkewe kazi haimaanishi ndio kumtawala,kama angekuwa na busara na amehis tatizo angelifanyia uchunguzi kwanza na kutafuta namna ya kuliwasilisha kwa mdogo wake na sio kumfokea, kwan kutawaliwa kwa mwanaume kunahusisha mambo mengi,alistahili hayo matusi kwa kupagawishwa na pombe za bure!
 
Huyo mjomba mkubwa alikuwa mchonganishi sana, japo naona naye mkewe mjomba mdogo adabu ilikuwa ndogo, anapiga story na mashoga wake huku mumewe anakoboa mahindi kwenye kinu? anyway hapo ilikuwa ni zaidi ya mapenzi.
 
Mfume dume umetawala hichi kisa sababu kaka angemkuta mdogo wake anapiga stori na marafiki na mdada huyu ametoka kuchota maji ndoo kichwani mtoto mgongoni na kifurushi cha mzigo mkononi sidhani kama angemfokea mdogo wake kwanini mkeo anabeba mizigo yote na wewe umekaa hapa...naamini mjomba mkubwa amejifunza hapo kutoingilia mambo ya watu tena..
 
Mfume dume umetawala hichi kisa sababu kaka angemkuta mdogo wake anapiga stori na marafiki na mdada huyu ametoka kuchota maji ndoo kichwani mtoto mgongoni na kifurushi cha mzigo mkononi sidhani kama angemfokea mdogo wake kwanini mkeo anabeba mizigo yote na wewe umekaa hapa...naamini mjomba mkubwa amejifunza hapo kutoingilia mambo ya watu tena..


Avartar yako nimeipendaaa
 
Mfume dume umetawala hichi kisa sababu kaka angemkuta mdogo wake anapiga stori na marafiki na mdada huyu ametoka kuchota maji ndoo kichwani mtoto mgongoni na kifurushi cha mzigo mkononi sidhani kama angemfokea mdogo wake kwanini mkeo anabeba mizigo yote na wewe umekaa hapa...naamini mjomba mkubwa amejifunza hapo kutoingilia mambo ya watu tena..

Unajua Lolyz, kitu ambacho wengi humu hawajakijua ni kwamba tukio hili lilitokea mwaka 1987, ambapo kile kinachioitwa usawa kwa wanawake kilikuwa hakizungumzwi kama tunavyozungumza leo. Mwanaume alionekana mtu wa ajabu kumsaidie mkewe na yeye akiwa amekaa na kupiga soga. hayo yalionekana ni matusi.
 
Back
Top Bottom