Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Juni 18, 2025 kwenye mitandao ya jamii kulikuwa na video inayosambaa ikimwonyesha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya chama cha NRM, Dk Tanga Odoi akimkabidhi fomu ya kugombea ubunge Jenerali Moses Ali (86) akiwa kwenye gari lake.
Kutokana na hali yake ya afya na umri mkubwa, Jenerali Ali hakuweza kushuka kwenye gari lake, hivyo alitangazwa hapo hapo kuwa mgombea ubunge katika jimbo la Adjumani Magharibi kupitia chama tawala cha NRM, jambo lililoibua hisia mbalimbali mitandaoni, wengine wakisema wakimsifu kwa uzoefu na uongozi wake wa muda mrefu na wengine wakihoji uwezo wake wa kiafya na umuhimu wa uongozi wa kizazi kipya.
Jenerali Ali ni nani?
Jenerali Moses Ali ni mwanasiasa na jenerali mstaafu maarufu nchini Uganda akiwa ameitumikia Serikali kwa miaka 54 hadi sasa. Alizaliwa Aprili 5, 1939 katika Wilaya ya Adjumani na amehudumu katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na jeshi, siasa, na uasi wa kivita.
Alianza kazi jeshini na kuwa mshirika wa karibu wa dikteta Idi Amin aliyemteua kuwa Waziri wa Fedha. Baadaye walitofautiana na alinusurika jaribio la kuuawa mnamo mwaka 1978.
Baada ya kuanguka kwa utawala wa Idd Amin mwaka 1979, Ali alikimbilia msituni na kuanzisha kundi la waasi la Uganda National Rescue Front (UNRF) kupinga serikali ya Rais Milton Obote.
Miakaya 1980, alifanya maridhiano na Rais Yoweri Museveni, akaunganishwa na jeshi la Taifa na kupandishwa vyeo hadi kuwa Jenerali.
Siasa na uongozi Serikalini
Baada ya Rais Museveni kuingia madarakani, Jenerali Ali alishika alipanda vyeo jeshini hadi kufikia kuwa jenerali na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza (2016–2021) na Naibu Waziri Mkuu wa Pili na Naibu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni (2021 hadi sasa)
Alichaguliwa tena kuwa Mbunge wa Adjumani mwaka 2011 akiwa na umri wa miaka 72.
Moses Ali ni kielelezo cha historia ya Uganda — kutoka enzi ya Amin, maisha ya msituni kama muasi, hadi kuwa mshirika wa karibu wa Museveni kwa miongo kadhaa. Hata akiwa na miaka 86, bado anajihusisha kikamilifu na siasa, ingawa kuna mjadala kuhusu nafasi ya viongozi wakongwe katika uongozi wa taifa.