JE, UNAUFAHAMU USABATO NA ASILI YAKE?
Baadhi ya wasomaji katika ukurasa wa Askofu Mwamakula wametafuta kujua asili na chanzo cha Kanisa la Wasabato. Historia ya Kanisa hili haijulikani sana pengine kutokana na sababu mbili: mosi, Wasabato hawakazi sana kuhusu historia (ecclessiogy) yao, lakini wanakaza juu ya mafundisho (doctrines) yao na ushawishi wa viongozi (charisma) wao kama vile Ellen G White. Pili, Makanisa ya kihistoria (mainstream churches) hawafundishi juu ya asili na historia ya Wasabato, bali wao hukazania kuufundisha Usabato kama imani potofu (sect au cult). Huu ni udhaifu mkubwa sana.
Kwa maoni yetu, upungufu wa pande zote mbili juu ya historia ya Kanisa la Wasabato hautendi haki na hivyo umepelekea kuwepo kwa ombwe lisilokuwa na sababu juu ya Kanisa hili ambalo linakua kwa kasi duniani hasa katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama vile Tanzania, Kenya na Rwanda. Ni lengo la andiko hili la Askofu liwe sehemu ya kujenga kiu ili watu watafute kuijua zaidi historia ya Wasabato na viongozi wao.
Kumbukumbu zetu zinaonyesha kuwa Usabato umepitia hatua nyingi tangu ulipoanzishwa na hatua hizi ziliambatana na changamoto za hata migawanyiko mingi kama ilivyo kwa Makanisa mengine katika historia ya Ukristo. Kwa hiyo, tunaposema juu ya Usabato, tunamaanisha vuguvugu ambalo lilikuja kuzaa madhehebu mengi ya Kisabato. Madhehebu ya Kisabato yapo katika milengo 3: mlengo ule wa Kibatisti (Baptisti), mlengo wa Kipentekoste na mlengo mwingine ambao hautagusiwa hapa na hii ni kutokana na ufinyu wa nafasi.
Milengo hiyo watu wasipoielewa wanaweza pia kufanya kosa la kuweka Wasabato wote katika kundi moja. Watu watashangaa kuona kuwa wakati Wasabato hufanya bidii katika kufanya mikutano ya hadhara kama Wapentekoste, ila wengine hawafanyi badala yake hufanya bidii kuimarisha Kanisa la mahali kama Wabatisti. Milengo hiyo haina ugomvi na Makanisa au madhehebu mengi ya Kikristo na mara nyingi hushirikiana nayo. Lakini mlengo wa tatu ni ule hulenga zaidi katika kushambulia madhehebu mengine kama wafanyavyo Wamomoni.
Kwa ufupi, panorama (historia) ya Usabato au Seventh-Day Adventism (S.D.A) na matawi yake ni kama ifuatavyo:
Mwaka 1830, William Miller alianzisha Tawi la kwanza la Seven Adventist lililoitwa Millerites kutokana na jina la mwanzilishi ambapo msingi wa kuanza kwa Kanisa hili ni tafsiri ya kitabu cha Danieli 8:14 iliyojengwa katika mikokoto (mathematical calculations) ya Williams Miller aliyekadiria kuwa kuja kwa Yesu mara ya pili ingekuwa kati ya 21 Machi 1843 na 21 Machi 1844. Pia unabii wa Hiram Edson juu ya Danieli 8:14 kuhusu siku 2,300 ulikuwa ndio msingi wa kuanza kwa vuguvugu hilo la Usabato.
Mwaka 1835, lilizaliwa tawi la Kisabato ambalo liliitwa American Millennial Association. Neno hili millennial limetumika hapa makusudi kwa sababu ya mikazo ya kitheologia wakati huo ya premillenial, amillenial na postmillennial. Lakini Mwaka 1860, lilizaliwa tawi lingine la Kisabato ambalo liliitwa Seventh-Day Adventists. Mwaka huo huo wa 1860 lilizaliwa tawi lingine ambalo liliitwa Advent Christian Church. Mwaka 1865, lilizaliwa Kanisa lingine la Kisabato lililoitwa Church of God (Seventh Day).
Kwa ujumla, kama vile hakuna Kanisa moja la Kipentekoste, kama vile hakuna Kanisa moja la Kibatisti na kama vile hakuna Kanisa moja la Ki-Asemblies of God, ndivyo pia hakuna Kanisa moja la Kisabato. Usabato ni vuguvugu au kwa Kiingereza (movement) ambalo limepitia hatua nyingi na pia linaendelea kupitia hatua kadhaa. Kwa sababu hiyo, ni vizuri watu waepuke kosa la kuuweka Usabato wote katika kapu moja.
Tahadhari kubwa ichukuliwe katika kuuongelea Usabato kwa kuwa yapo matawi au Makanisa ya Kisabato yamejikita katika kufundisha unabii na mafundisho ya watu ambao ni waasisi wao. Lakini yapo pia Makanisa ya Kisabato ambayo mafundisho yao misingi yao ni Biblia. Pengine swali hapa ni watu watajuaje tofauti hizo. Hapa hatuna jibu jepesi hasa kwa watu wachanga na wanaotoka katika dini nyingine. Kigezo ni kama mkazo mkubwa wa mafundisho yao uko katika kufundisha mafundisho ya manabii wao badala ya kufundisha Biblia kwa ujumla wake.
Andiko hili ni msimamo binafsi wa Askofu Mwamakula na wala hauwezi kuwa msimamo wa Wasabato wote na pia hauwezi kuwa ndio msimamo wa Kanisa lote Katholiko. Lengo la andiko hili sio kuzua mjadala au mabishano ya kidini, bali lengo ni kuwasaidia watu ili kuelewa kuwa zipo tofauti ndani ya Usabato na kwamba Usabato usichukuliwe kama Kanisa moja.
Pia watu wajue kuwa wapo Wasabato ambao ni orthodox (wako katika misingi ya Ki-Biblia) na wapo pia ambao ni cult/heretic (walioondoka katika misingi ya Ki-Biblia). Kwa ufupi, Usabato ni vuguvugu kama ulivyokuwa Upentekoste. Ni maoni yetu kuwa Wasabato wenyewe wanao wajibu wa kuandika historia yao kwa ufasaha. Mafundisho (doctrines) hayawezi kuchukua ile nafasi ya historia. Upungufu huo wa historia ya kuanza, kukua na kuenea kwa Usabato utoshe.
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula ambaye ni mwandishi wa makala hii, ni Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani. Pia, ni mhadhiri wa falsafa, theologia, literature, ecclessiogia, missiologia, utafiti na soshologia. Amefundisha masomo hayo kwa miaka kadhaa katika Chuo Kikuu, St. John's University of Tanzania.
Dar es Salaam, 3 Aprili 2024; saa 8:25 alasiri
Sabato ilianzia eden Mungu alipopumzika siku ya saba,
MWANZO 2:1-4
1Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. 2Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya. 3Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba. 4Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.
ikatunzwa hata Jangwani wakati waisrael wakisafiri kwenda kanani
Kutoka 16:23-26
Mose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Bwana. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ”
24Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. 25Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Bwana. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. 26 Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo chochote.”
Sabato Ikakumbushiwa tena kwenye amri kumi na Yesu na mitume waliitunza Kutoka 20:8
Yesu alielekeza baadhi ya vitu vya kufanya siku ya sabato
MWANZO 2
1Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. 2Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya. 3Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba. 4Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.
Sabato ilikuwepo miaka Yote, lakini mnamo mwaka 321, baada ya wapagani kuingia ndani ya kanisa waliiondoa sabato na kuiweka jumapili, na wale waliokuwa wanapinga wengi waliuwawa na wengine walikimbilia misituni, Kuanzia mwaka 1776 watu wengi kutoka ulaya walianza kukimbilia Amerika ambako kulikuwa na uhuru wa Dini, hivyo hata wale waliokuwa wanatunza sabato maporini ikabidi wakimbilie Amerika, ijapokuwa walikuwa katika Nchi yenye uhuru wa Dini, lakini bado hawakujitokeza kwa uwazi sana, maana walikuwa wanawaogopa Wakatoliki.
Ndipo ulipofika mwaka 1845, ikabidi waanze kudhihirisha imani yao ikiwemo kutangaza sabato ya kweli, maana watu wote walikuwa wanatunza jumapili. Watu hawa wakaandaa vijizuu vinavyoonesha umuhimu wa sabato, February 8, 1845 bwana mmoja aliyeitwa T.M Preble alichapisha vijarida, kinachonesha kwamba sabato ni moja ya amri kumi za Mungu, vijajarida na vipeperushi hivyo viliwafikia watu wengi wakiwemo wachungaji wa makanisa ya jumapili, na wengi wakaacha kufanya ibada jumapili baada ya kuujua ukweli.
Siku moja James White na Ellen White walipata kijarida chenye somo la sabato, na baada ya kusoma kijarda hicho na wakarizika na ushahidi wa mafungu, ndipo na wao wakaanza kutunza sabato.
Kama ambavyo Ellen mwenyewe anashuhudia akisema:
“”Kaika kipindi cha kipupwe cha mwaka 1846, tulianza kutunza sabato ya Biblia, kufundisha na kuitetea””, Testimonies Vol 1 Uk. 75.
Lakini watu wengi hudai kwamba Ellen ndiye aliyeanzisha sabato huo ni #UWONGO MKUBWA, maana Ellen G White naye alihubiriwa na baada ya kuuamini hle ujumbe akajiunga na watunza sabato, wakati huo tayari kulikuwa na watu waliomtangulia kuupokea ujumbe wa sabato.
Lakini baadhi huaminishwa kwamba Ellen alipata maono ya sabato, na kuiona amri ya 4 inang’aa kupita nyingine, na ndipo baada ya hapo ndipo akaanzisha utunzaji wa sabato.
Ni kweli maono hayo alipata, lakini akiwa tayari anatunza sabato, na alipewa kama uthibitisho kwamba sabato ni kweli inabidi itunzwe. Yeye mwenyewe Ellen anashuhudia akisema:
“”Niliamini ukweli juu ya suala la sabato kabla sijaona chochpte katika maono kinachohusiana na sabato. Ilikuwa baada ya miezi kadhaa nimeanza kutunza sabato ndipo nilionyeshwa umuhimu wake na nafasi yake katika ujumbe wa malaika watatu””:
Ellen G White letters 2, 1874( Maandiko ya awali xxiii)
Na kuanzia hapo wakapatikana watu wengi waliojiunga na watunza sabato, na ilipofika mwaka 1863, ndipo likapatikana jina la Seventh Day Adventist (SDA) Ikiwa na maana ni Watu wanaosubiri marejeo ya Yesu mara ya pili, wakiitunza sabato ya siku ya saba.
Hivyo ukifuatilia kwa Umakini utaona kwamba:
Ellen G White hajawahi kutabiri kwamba mwisho wa Dunia ni mwaka 1844
Ellen G White hajawahi kuanzisha kanisa, wala sabato,
William Miller hajawahi kutunza sabato wala kuanzisha Kanisa.