Mkaguzi Kata ya Mwaya Mkoani Morogoro atoa mafunzo ya TEHAMA VETA - Mwaya

Mkaguzi Kata ya Mwaya Mkoani Morogoro atoa mafunzo ya TEHAMA VETA - Mwaya

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
WhatsApp Image 2026-08-11 at 12.28.59.jpeg
Mkaguzi wa Polisi Kata ya Mwaya, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro, Mkaguzi wa Polisi (INSP) Masengi Marwa, ametoa mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mwaya kuhusu matumizi sahihi na salama ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Mkaguzi huyo, ambaye pia amebobea katika masuala ya TEHAMA na mawasiliano ya habari, amesema matumizi sahihi ya teknolojia ni muhimu katika kujenga kizazi chenye ujuzi na maarifa yanayoweza kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
WhatsApp Image 2026-08-11 at 12.28.59 (1).jpeg

WhatsApp Image 2026-08-11 at 12.28.58 (1).jpeg
Katika mafunzo hayo, INSP Masengi amewataka wanafunzi hao kutumia fursa zinazopatikana kupitia teknolojia kujifunza zaidi na kuongeza ujuzi wao, hususani katika masomo yanayohusiana na sayansi ya kompyuta.

Amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kuwa na utamaduni wa kusoma na kujifunza kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandaoni, huku akiwashauri kutumia wataalamu wa masuala ya kompyuta pale wanapohitaji msaada au ufafanuzi zaidi ili kuwa mahiri katika fani hiyo.

“Dunia ya sasa inahitaji wataalamu wa sayansi ya kompyuta ni muhimu kutumia teknolojia kama nyenzo ya kujifunza, kuongeza maarifa na kujenga ujuzi utakaowasaidia katika maisha na kazi zanu,” amesema INSP Masengi.

Aidha, amewatahadharisha wanafunzi na watumiaji wengine wa teknolojia dhidi ya kutumia ujuzi wa TEHAMA na mitandao ya kijamii kufanya vitendo vya uhalifu, akieleza kuwa Jeshi la Polisi lina wataalamu wenye uwezo wa kufuatilia na kuchunguza uhalifu unaofanyika katika mitandao na mifumo ya kidijitali.

Amewataka kutumia ujuzi wa teknolojia kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya Taifa, badala ya kuutumia katika vitendo vinavyoweza kusababisha madhara kwa watu wengine au kuchukuliwa hatua za kisheria.

Vilevile, amewataka wanafunzi na wananchi kwa ujumla kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu na kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi salama na yenye tija ya teknolojia, pamoja na kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na uhalifu unaofanyika kupitia mitandao na teknolojia za kidijitali.
 
Back
Top Bottom