View attachment 3531866
Kimya kingi kina mshindo mkuu, Waswahili wanasema. Hivyo ndivyo mikakati inavyopangwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kurejeshwa kwenye chama hicho kwa mlango wa nyuma kwa ajenda ya maridhiano.
Hii inakuja kufuatia juhudi zakumshawishi Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Tundu Lissu kushindikana, akitaka Serikali iendelee na kesi ya uhaini waliyoianzisha.
Taarifa kutoka vyanzo ndani ya chama hicho zinadai kuwa kumekuwa na juhudi za chini kwa chini za kumshawishi Lissu akubaliane na maridhiano yanayoandaliwa na CCM ili kesi yake ifutwe, lakini amewakatalia kata kata.
Lissu aliyekamatwa tangu Aprili 9, 2025 wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma na kuletwa Dar es Salaam ambako alifunguliwa mashitaka ya uhaini, anatarajiwa kufikishwa tena Mahakama Kuu masijala ndogo ya Dar es Salaam Februari 9, 2026 baada ya kesi yake kuahirishwa tangu Novemba 13.
Kabla ya kesi hiyo kuahirishwa, ilionekana kupoteza nguvu baada ya Mahakama kukataa kupokea ushahidi wa masingi wa shahidi wa tatu, huku Lissu anayejitetea mwenyewe akidai kuwa mpaka hapo kesi imekwisha na kilichokuwa kinasubiriwa ilikuwa ni uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Licha ya kesi hiyo kupoteza nguvu, inadaiwa kuwa kesi hiyo kwa sasa haina manufaa kwa Serikali ya CCM na kumekuwa na juhudi za kumshawishi Lissu akubaliane na hoja ya maridhiano ili aachiliwe huru, lakini amekataa akitaka mchakato wa mahakama uendelee.
Mikakati hiyo inakuja wakati Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche amenukuliwa akisema kuwa chama hicho hakiko tayari kwa maridhiano yasiyo na uwajibikaji. Aliyasema hayo Januari 3 alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya 2026.
Kauli ya Heche ilionekana kupinga kauli aliyotoa Rais Samia Suluhu Hassan katika salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, 2025 aliposema mchakato wa kuanzisha Tume ya Maridhiano umeshaanza.
Duru mbalimbali mitandaoni na ndani ya chama hicho, zinaelea kuwa Mbowe anaandaliwa kuunganisha vyama vikubwa vya siasa ikiwamo CHADEMA, ili kupigania hoja ya maridhiano, huku akijitanabaisha kuwa yeye ndiye mkombozi wa chama hicho.
Bado haijaeleweka Mbowe ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA atarudije kwenye nafasi za maamuzi za chama, lakini pia inaelezwa kuwa kinachotafutwa ni namna ya kumpa nafasi ya kushauri au kulainisha mambo kwenye chama hicho, ili kikubaliane na hoja ya maridhiano.
Kuonyesha kuwepo kwa mipango hiyo, mmoja wa makada wa Martin Maranja Masese aliandika kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), akisema hizo ni porojo,
"Tundu A.M Lissu alichaguliwa na mkutano mkuu wa CHADEMA. Hakuna kiumbe mwingine yeyote anaweza kumuondoa zaidi ya mkutano mkuu wa chama Taifa ambao ulimchagua. Hizo porojo nyingine za mazombi ya mbogamboga ni za wapumbavu waliolewa visungura tu na hawaelewi katiba ya CHADEMA."
Misimamo mikali ya Lissu, Heche
Misimamo mikali ya Lissu na Heche ndiyo inatajwa kuwa sababu ya kumuingiza Mbowe anayetajwa kusikilizwa zaidi na Serikali ya CCM. Ikumbukwe Mbowe ndiye aliyepeleka CHADEMA kwenye maridhiano ya awali baada ya kuachiliwa huru Machi 2022 baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kueleza Mahakama kuwa hayuko tayari kuendelea na kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili mwanasiasa huyo.
Katika kampeni zake za kuwania uenyekiti wa CHADEMA Januari 2025, Mbowe alitetea sana maridhiano aliyofanya na CCM ambayo hata hivyo yalivunjika bila kufika mwisho. Miongoni mwa mafanikio aliyoyataja ni pamoja na kuachiliwa huru kwa mamia ya wanachama wa chama hicho waliokuwa wamefunguliwa kesi za kisiasa na ununuzi wa ofisi ya makao makuu iliyopo Mikocheni Dar es Salaam.
Tangu aliposhindwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa Januari 22, 2025, Mbowe amekuwa kimya, licha ya misukosuko iliyokikumba chama hicho, huku mwenyewe kwa nyakati tofauti akisema viongozi wa chama wapo ndio wanapaswa kushughulikia changamoto hizo.
Hata hivyo, Mbowe alishiriki uzinduzi wa Dira ya Taifa ya 2050 uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam Julai 17, 2025, ambapo alionyesha matumaini yake kwa dira hiyo.
Mbali na kesi inayomkabili Lissu, CHADEMA pia imefunguliwa kesi na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Khamis na wenzake wawili wakidai kutokuwepo kwa mgawanyo sawa wa mali za chama hicho kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Kutokana na kesi hiyo, CHADEMA imezuiwa kufanya kazi kwa kutumia rasilimali zikiwemo ofisi, magari na nyinginezo zinazosimamiwa na Nodi ya wadhamini na katibu Mkuu tangu Juni 10, 2025. Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Februari 2026.
Pia, Mei 2025 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitengua uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa kamati kuu akiwamo Katibu Mkuu, John Mnyika, Godbless Lema, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar). Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala ambaye pia aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Hatua hiyo ilikuja kufuatia kada wa chama hicho, Lembrus Mchome kukishitaki chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya siasa kuwa idadi ya wajumbe wa Baraza Kuu waliopitisha uteuzi huo haikutimia.
Hata hivyo, CHADEMA walipinga suala hilo mahakamani na Agosti 2025 Mahakama Kuu Kanda ya Manyara ilikubali ombi la chama hicho kufungua kesi na ilisitisha uamuzi wa Ofisi ya Msajili mpaka kesi hiyo itakaposikilizwa.
Wakati hayo yakielezwa, baadhi ya waliokuwa makada wa CHADEMA wakimuunga mkono na baadaye wakahamia Chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA, wameonekana wakitoa matamko ya kukosoa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na hata kuwaomba radhi Watanzania.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia CHAUMMA, Patrick Assenga, ambaye hivi karibuni amefanya mahojiano na Jambo TV na kutangaza kuunga mkono msimamo wa CHADEMA kuhusu kutaka maridhiano yenye uwajibikaji.
Mwingine ni aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo la Hai, kupitia CHAUMMA James Mbowe aliyezungumza kupitia mtandao wa Instagram akiomba msamaha kwa hatua yake ya kuhama CHADEMA na kukiri kwamba uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 haukuwa huru wala wa haki.