Vigogo kitanzini (Tanzania Daima)
na Ratifa Baranyikwa na Kulwa Karedia
SASA ni dhahiri kuwa Rais Jakaya Kikwete amedhamiria kuandika historia mpya kwa kuwa rais wa kwanza wa Tanzania kumfikisha mahakamani mtangulizi wake.
Ingawa hatua hiyo inaelezwa na wafuatiliaji wa mambo kuwa inaweza kuwa na athari mbaya kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na serikali anayoiongoza, inabaki kuwa nguzo yake kuu ya kurejesha imani kwa wananchi wanaotaka kuona akitekeleza ahadi zake kama ambavyo amekuwa akiahidi mara kwa mara.
Tamko la serikali lililotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Alhamisi, Aprili 24, bungeni Dodoma, kuwa inafuatilia taarifa za tuhuma kuhusu matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, na iwapo ikithibitika kuwa walitenda makosa, watachukuliwa hatua zinazostahili, linaonyesha kuwa sasa Mkapa anaweza kufikishwa mahakamani.
Katika kuonyesha dhamira ya dhati ya serikali yake kuhakikisha inatekeleza matakwa ya wananchi ya kutaka kuwepo uchunguzi kwa viongozi wa juu serikalini wanaotuhumiwa kutumia madaraka yao vibaya, Rais Kikwete jana aliwaambia waandishi wa habari kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, kuwa juhudi za kupambana na vitendo vya rushwa zinaendelezwa bila ajizi.
Rais Jakaya Kikwete, ambaye jana aliongoza mamia ya Watanzania kuadhimisha miaka 44 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, sherehe zilizofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam bila kuwepo kwa mtangulizi wake, Mkapa, aliwaomba wananchi kushirikiana na serikali yake katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi.
Katika taarifa yake hiyo iliyotolewa Ikulu, alisema mafanikio ya mapambano yanayoonekana hivi sasa yanategemea zaidi ushirikiano wa wafanyakazi na akawataka kuwa mstari wa mbele katika harakati hizo.
Aidha, aliwataka kuzingatia kujiepusha na vitendo vya kupokea au kutoa rushwa, kwa sababu nao wananungunikiwa na umma kujihusisha navyo.
Taarifa hiyo ambayo Kikwete anaeleza kuwa hatakuwepo katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi, ilieleza kuwa wafanyakazi wakiipiga vita rushwa, vigogo wanaodaiwa kupokea rushwa watapata wakati mgumu wa kufanikisha vitendo vyao viovu.
Rais amewaomba wafanyakazi wafanye mambo matatu, kwanza, wajiepushe wao wenyewe na vitendo vya rushwa
.wakatae kutumika katika vitendo vya rushwa
na wasaidie kutoa taarifa za rushwa ili zifanyiwe kazi na wahusika wabanwe, inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Rais Kikwete.
Tamko hili la Rais Kikwete ambaye jana alitangaza kutohudhuria sherehe za Mei Mosi kutokana na kuwa safarini katika nchi za Uganda na Ethiopia, limetafsiriwa na wafuatiliaji wa mambo kuwa hatua yake ya kwanza ya kuuthibitishia umma wa wafanyakazi kuwa hakuna kiongozi atakayesalimika kama atabainika kuhusishwa na rushwa.
Aidha, walieleza kuwa Rais Kikwete amelazimika kutoa tamko hilo ili kupoza dukuduku la wafanyakazi kuonyesha hasira yao kwa serikali katika maadhimisho hayo, jambo linaloweza kuzidi kujenga taswira mbaya kwa serikali yake.
Pamoja na Mkapa, tamko la Waziri Mkuu Pinda, sambamba na lililotolewa jana na Rais Kikwete, yanonyesha kuwa viongozi wengine waandamizi walio katika hatari ya kufikishwa mahakamani iwapo tuhuma zinazoelekezwa kwao zitathibitika kuwa kweli, ni pamoja na Andrew Chenge na Basil Mramba, ambao walikuwa mihimili na washauri wa karibu wa Mkapa wakati wa utawala wake.
Tayari Chenge ambaye alilazimika kujiuzulu wadhifa wa uwaziri hivi karibuni ameanza kuchunguzwa kwa tuhuma za kuhusika na kashfa za rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo Tanzania iliuziwa na Kampuni ya BAE ya nchini Uingereza.
Wachambuzi wameeleza kuwa iwapo Mkapa na Chenge watathibitika kuhusika na makosa ya jinai, basi haitakuwa rahisi kwa Mramba kuachwa pembeni kwa sababu alikuwa mshauri mkuu wa masuala ya fedha wa Mkapa.
Katika hatua nyingine, kutoonekana na ukimya wa sasa wa Mkapa umeanza kuzusha hisia tofauti miongoni mwa jamii.
Mkapa jana pia hakuonekana katika sherehe za maadhimisho ya miaka 44 ya Muungano huku viongozi wengine wastaafu wakihudhuria sherehe hizo.
Ukiacha Mkapa, viongozi wastatafu waliohudhuria ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Haikufahamika hasa sababu za kutohudhuria kwa Mkapa katika sherehe hizo, ikiwa ni mara ya pili kukosekana katika matukio makubwa ya kitaifa na yale yanayokihusu chama chake, ambacho alikuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka kumi.
Mkapa hakuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi uliofanyika Butiama, mkoani Mara mwishoni mwa Machi, mwaka huu.
Wadadisi na wachambuzi waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili walieleza kushangazwa kwao na kutoonekana kwa Mkapa katika matukio hayo makubwa ya kitaifa na kichama na kudai kuwa huenda kunasababishwa na uzito wa tuhuma zinazomkabili.
Baadhi ya tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa ni pamoja na kumiliki Kampuni ya kuzalisha umeme ya Tanpower Resources Ltd, ambayo ilishinda zabuni ya kununua mradi wa kuzalisha umeme kutoka mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ulioko Mbeya.
Madai hayo ambayo ni miongoni mwa yale yaliyoelezwa kuchunguzwa na Serikali, yanaelezwa kuwa huenda ni moja kati ya mambo yanayomkosesha raha kiongozi huyo na kumfanya ashindwe kujumuika na viongozi wenzake hata katika masuala muhimu.
Aidha, sherehe hizo za muungano ambazo jana zilifanyika kwa mbwembwe za aina yake, hazikuhudhuriwa pia na viongozi wengine wa vyama vya siasa.
Watu wengine mashuhuri ambao hawakuhudhuria sherehe hizo ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Andrew Chenge.
Matukio ya jana yalivuta hisia za wengi katika sherehe hizo zilizoanza majira ya saa 4:05 asubuhi, baada ya Rais Kikwete kuwasili uwanjani hapo akiwa katika gari la wazi pamoja na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Wakati akiingia uwanjani, rais aliweza kuvumilia mvua iliyokuwa ikinyesha.
Sherehe hizo pia zilipambwa na mbwembwe za helikopta za jeshi pamoja na ndege za usafirishaji zilizopita uwanjani hapo zikitokea upande wa kaskazini mwa uwanja huo.
Katika kuadhimisha sherehe hizo, Rais Kikwete jana alitoa msamaha kwa wafungwa 3,300.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, kwa vyombo vya habari, ilisema msamaha huo utahusu wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya miaka mitano.
Alisema msamaha huo utawahusu wafungwa wazee na wenye umri zaidi ya miaka 40, lakini hauwagusi wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, waliokamatwa na dawa za kulevya, unyanganyi wa kutumia silaha, wanaotumikia kifungo cha maisha, kujamiana na wenye makosa ya kuwapa mimba wanafunzi.