macho_mdiliko
Platinum Member
- Mar 10, 2008
- 25,191
- 48,765
Mchezaji wa zamani wa timu ya Arsenal, kutoka Togo Emmanuel Adebayor amefikia hatua ya kutaka kujiua kwa sababu ya visa na mikasa na ndugu zake. Hata timu yake ya sasa Tottenham imebidi impe mapumziko. Usome mkasa mzima kama ulivyotafsiriwa:
Source Emmanuel Adebayor accuses brothers of holding KNIFE to his throat in third Facebook statement - Mirror Online
Ninapoamua kuandika leo, ni kwa sababu kaka yangu Kola Adebayor na mdogo wangu wameamua kuweka wazi tena hadharani mambo ya familia kwenye; mitandao ya kijamii, barua kwenda kwenye timu yangu na kwenye redio.
Miaka 25 iliyopita kaka yangu mkubwa anayeitwa Kola, alienda Ujerumani na kuwa tumaini pekee la familia yetu. Tulikuwa na matumaini kuwa angebadilisha maisha yetu. Miaka kadhaa baada ya kuondoka Togo, tulikuwa bado hatuna umeme wala simu. Siku alipotaka kuongea na sisi alikuwa anapiga simu hotel inayoitwa Atlantic ambayo iko karibu na nyumbani kwetu na sisi tulikwenda pale kuongea nae.
Nilipopata bahati ya kwenda kucheza mpira wa miguu Ufaransa kwa mara ya kwanza, tulikuwa tunahitaji fedha kwa ajili ya tiketi ya safari yangu na matumizi mengine. Kaka yangu hakuwa na msaada wowote. Mungu pekee ndiye anayejua alikuwa anafanya nini huko Ujerumani.
Nilipowasili Ufaransa, nilishughulikia mambo yote ya vibali nikisaidiwa na timu yangu, na baadae waliniruhusu niishi kwenye shule yao ya mafunzo. Miezi michache baadae, kaka yangu alitaka kuja kunitembelea. Nilikuwa sina fedha za kutosha na zaidi nilikuwa naishi kwenye shule ya mafunzo. Hivyo basi nililazimika kukopa fedha ili niweze kumlipia hoteli ya kushukia. Sega N'diaye kutoka Kameruni ambae alikuwa rafiki yangu na mchezaji mwenzangu alikubali kunikopesha. Vilevile nililazimika kukopa fedha zaidi kwa ajili ya kumpa kaka yangu kwa ajili ya safari yake ya kurudi Ujerumani. Ikumbukwe kwamba huyu ndie kaka yangu mkubwa.
Miaka michache baadae mambo yalianza kuwa mazuri. Asante Mungu, nilisaini mkataba na timu ya Metz. Kuanzia muda huo, kaka yangu akawa anawasiliana na mimi kila alipokuwa na bili za kulipia. Mara aseme mtoto wake ni mgonjwa... ilibidi nizoee hizi kadhia.
Baadae, nilibahatika tena kupata mwaliko wa timu ya Monaco, na baade nikasaini mkataba wa kuichezea. Siku moja, Kola na marehemu mdogo wangu Peter Adebayor walikuja Monaco kunitembelea. Tena walikuja bila taarifa yoyote. Wahenga walisema damu ni nzito kuliko maji, hivyo niliwakaribisha. Waliwasili asubuhi na mapema na mimi nilikuwa ndio naelekea kwenye mazoezi. Niliporudi nyumbani, tuliongea na wakaniambia wanataka kuanzisha biashara ya magari. Ni dhahiri zilikuwa zinahitajika fedha nyingi. Niliwaambia kwamba nitaweza kuwasaidia mara tu nitakapolipwa fedha zangu. Kwa kipindi kile rafiki yangu Thierry Mangwa, alikuwa anakaa kwenye nyumba yangu kwa sababu alikuwa ana matatizo yake na alikuwa anahitaji sehemu ya kuishi. Siku moja, niliporudi kutoka kwenye mazoezi nilimkuta analia. Hakuniambia kilichomliza. Kaka zangu pia hawakuniambia kilichomliza. Siku nyingine, rafiki yangu kwa jina Padjoe alikuja kunitembelea na wakati anaondoka nilimpa kama euro 500 (kwenye shilingi milioni moja za kitanzania). Kumbe kaka yangu Kola aliona na akakasirika kweli kweli. Alikuwa haoni sababu ni kwanini nimpe zile fedha badala ya kumpa yeye. Mimi nilimwambia kitu kimoja: fedha alizokuwa anaomba ni nyingi sana na sikuwa nazo nyumbani. Tulikorofishana kwa hili jambo.
Siku nyingine tena, baada ya uchovu wa mazoezi niliamua kujipumzisha. Mara nikagutuka, na kukuta kisu kipo shingoni mwangu. Walikuwa ni kaka zangu. Walikuwa wanapiga kelele huku wakisema nawapotezea muda wao. Peter alikuwa na hasira sana na Kola alikuwa anamuunga mkono. Nikawauliza: Hii ndio njia pekee ya kutatua hili tatizo? Kama mnaona ni sawa basi niueni ili mchukue hizo fedha! Walipoona hivyo wakaweka kisu chao chini. Baada ya sokomoko hili, nikatoka nje na kupiga simu nyumbani kwa wazazi. Mama yangu alinishauri niwaripoti polisi kwani ndio ilikuwa njii pekee ya kuweza kuingia ndani kwa usalama. Pamoja na pilika zote, kesho yake bado nilienda kwenye mazoezi. Na nilifanya kama mama yangu alivyonishauri. Polisi alikuja na kusawazisha mambo. Bado kama wasemavyo damu ni nzito kuliko maji, niliamua kusamehe.
Baada ya siku chache Peter alienda kumtembelea mmoja wa marafiki wa Kolo anayeishi Parisi. Hivyo nikabaki nyumbani na Kola pekee. Nikaamua kumpa zile fedha haraka iwezekanavyo. Mungu peke yake ndie anayejua nilimpa kiasi gani!
Mwezi mmoja baada ya sakata lote hili, nilienda kutembelea nyumbani Togo na kushangaa wakati mama yangu ananilaumu eti ni kwanini niliripoti kaka zangu polisi. Akaenda mbali na kusema mimi ni mtu mbaya kwenye familia yetu. Hii ni hadithi nyingine amabayo nitasimulia siku nyingine...
Halafu kila nilipokuwa naenda nyumbani Togo, watu walikuwa wananiuliza ni kwanini kaka yangu haji nyumbani kusalimia miaka yote hii. Basi ikanibidi niandae safari ili aje nyumbani, na gharama zote zilikuwa juu yangu.
Siku ya tarehe 22.4.2005, tulipata habari mbaya za msiba. Nilipata habari kuwa baba yangu amefariki dunia. Nilichanganyikiwa! Nilimpigia simu kaka yangu mkubwa na kumweleza kuwa itabidi wote tuende. Halafu tena, nilihakikisha nimemnunulia tiketi ya ndege kwa ajili ya safari. Wote tulienda nyumbani na nilishughulikia gharama na mambo yote. Kabla baba yangu hajafa, alipokuwa hospitalini aliniambia nihakikishe wakati wa mazishi yake hakuna kuhuzunika. Alitaka mazishi yawe kama sherehe. Nimemwachia. Mungu aamue kama mazishi niliyofanya ndio alivyotaka baba yangu. Halfu mtu anayejiita ''bwana mkubwa'' kwenye familia yetu hakuchangia gharama yoyote. Na bado anapiga kelele eti sisaidii familia yetu.
Mwaka 2006, nilibahatika tena kwenda kuchezea timu ya Arsenal. Kuanzia kipindi hicho, kaka yangu hakuisha kuja na tuhuma za uongo juu yangu.
Tarehe 22.07.2013 tulipata habari mbaya kwenye familia yetu. Kaka yangu Peter Adebayor alikuwa amefariki. Kifo chake kilinisikitisha na kuniathiri. Kitu kimoja kinachonihuzunisha mpaka sasa ni kuwa Kola alikuwa ananituhumu eti mimi ndiye niliyesababisha kifo cha Peter. Alisema eti duka nililomfungulia Peter lilikuwa halina hadhi. Akawa anatuma meseji na kusema eti maisha yangu ya mpira yataharibika. Nilikuwa nimefanya mengi kwa Peter wakati akiwa hai, nilimleta Metz na Monaco. Yeye Kola anaweza kusema alifanya nini kwa Peter? Hakufanya chochote! Mtu mwenyewe hata kwenye mazishi hakufika pamoja na fedha zote nilizomtumia kwa ajili ya nauli ya kuja.
Pia anasema nimemfanya mama yetu ataabike, lakini anasahau kwamba wakati akiwa Ujerumani mimi ndio nilikuwa niko na mama bega kwa bega. Na mara nilipoanza kupata kipato kwa ajili ya mpira, nilijitahidi kwa njia zote uzijuazo kumtunza mama yangu. Hili ni jambo la kawaida. Lakini kaka yangu haridhiki kamwe. Alisema nilimnunulia mama gari mkweche. Mbona asimnunulie zuri sasa? Nachokitaka ni yeye kuwajibika. Kama anaona sifanyi inavyopaswa, basi aonyeshe ''ukaka'' wake. Ameishi Ujerumani zaidi ya miaka 20 lakini hajawahi hata siku moja kumchukua mama akamtembelee. Hata kwenda kusalimia nyumbani kwenyewe ni majanga. Kila siku anasema eti baba alisema niwajengee kila mmoja nyumba yake. Sidhani baba yangu alisema vile. Hili kweli linaingia akilini? Kama kaka mkubwa, alitakiwa yeye ndiye anayefanya haya yote niyafanyayo kwa ajili ya familia. Aache kujifichaficha na afanye majukumu yake. Kwanza alipokuja Ulaya, alikuwa na umri wa kuweza kuwa mchezaji kama mimi. Mbona hapa kuna madereva lakini bado wanaweza kusaidia familia zao. Wanawaleta mpaka wazazi na ndugu Ulaya. Mbona anapiga kelele wakati haya yote yamemshinda? Kwanza angejaribu hata kumleta Rotimi, Bidemi au mtoto wake Azizi kabla hajapayuka mambo ya ''kusaidia familia''. Matendo yashinda maneno.
Watu wengi wanadai eti sijawahi kwenda shule, lakini wanasahau ni kwasababu hatukuwa na uwezo. Siwezi kuwalaumu wazazi wangu kwa jambo hili. Hata hivyo namshukuru Mungu kwani leo hii naongea lugha zaidi ya tatuna naweza kumsomesha binti yangu. Najivunia hili. Watu wanaweza kunidharau kwasababu ya kutokwenda shule lakini mwisho wa siku kinachoamua ni mafanikio yako na vitu unavyojifunza. Ni kuhusu maisha yanakufunza nini na wewe unajifunza nini.
Kuna wakati nilikwisha kukata tamaa. Unaweza kumuuliza dada yangu Iyabo Adebayor ni mara ngapi nilitaka kujinyonga. Nilificha haya mambo kwa miaka mingi. Lakini nikifa hakuna atakayejua mikasa yangu na hakuna atakayejifunza kutokana na hii mikasa. Kuna watu wanasema haya mambo nisiyaseme hadharani, lakini mtu ni lazima ujitoe, mtu ni lazima uyazungumze. Najua watu watajifunza kutokana na mkasa wangu. Kwa wote wanaonijua, nafanya mambo yangu kwa ajili ya taifa langu na watu wangu. Na ujumbe kutoka kwa kaka mdogo kwenda kwa kaka mkubwa: Acha kuvuta sigara, acha ulevi. Hiki ndicho kisa changu!
Source Emmanuel Adebayor accuses brothers of holding KNIFE to his throat in third Facebook statement - Mirror Online