Mkasa wa kusisimua wa Rojaz katika kipindi cha sitasahau cha radio free africa
Sehemu ya 12
Hofu,hofu,hofu,kiukweli hofu ilinivaa na nikamwambia kaka "mimi sijui hizi taarifa umezipata wapi,inawezeka nipo katika hatari lakini mimi nipo tayari kuipokea hiyo hatari kwani siwezi kuvunja makubaliano tuliyokubaliana na yule mtu,siwezi kufanya hivyo hata siku moja,mimi ntakuwa mtu wa ajabu sana" na kaka amesema amenitumia mimi kwa makusudi kwanza ni kijana mdogo ni vigumu mtu kugundua kama amekutumia wewe na amekataa kutumia ndugu zake kwa sababu hataki kuweka ndugu zake kwenye matatizo ila anakutumia wewe awanufaishe ndugu zake" nilikataa na hata nilipopata muda wa kuwa mwenyewe niliyakataa maneno ya kaka,niliyakataa alafu nikajisikia kuugua ndani kwanini nimeyazungumza kwa sababu nilikuwa na amani kabla sijazungumza,nilifanya mishe zangu kwa amani kabla sijatoa siri hii,kaka aliendelea kunisumbua toka nilipomueleza kuhusu zile pesa,kaka alinisumbua sana alitaka tuonane huku akinitumia meseji za vitisho na hasa kaka alichokuwa ananitishia ni kwamba mimi nafatiliwa kwa sababu ya movement ambazo nimekuwa nazo kule gerezani,hofu ya kwenda gerezani ikaingia kwangu na nikajikuta nahofia kwenda tena gerezani,nilikuwa katika msongo mkali wa maisha yangu.
Nilitoka na kwenda kwa watoto wa mshkaji wangu,nilienda kuwatizama watoto kwani mpaka sasa hivi ilipofikia wanaishi katika mazingira mazuri kwa sababu nilishawatoa kule walipokuwa wakikaa mwanzo,sasa wanakaa pazuri,wanasoma pazuri na mama yao ana majukumu ya kazi pia,nilipoenda kuwatembelea walifurahi kwani sasa mimi nimekuwa moja kati ya majawabu kwenye maisha yao,wananihesabu sasa mimi ni ndugu,ni anko mzuri,niliona kama ni watu ambao naweza nikakaa nao nikajisikia nafuu kutokana na msongo wa mawazo nilioupata ghafla,kwa muda ambao nilikaa na hawa watoto walizungumza na mimi kwa upendo sana kwa mfano huyo mkubwa alisema "anko nashukuru sana nafikiri bila wewe sijui tungekuwa katika mazingira gani lakini umetufanya tunaishi katika nyumba nzuri,umekuwa kama malaika kwangu,mdogo wangu na hata mama,sasa hivi hatupiganii chakula kwani tunakula vizuri na tunakula tunachokitaka,nashukuru sana" huyu mkubwa alinambia maneno haya.
Moyoni mwangu naona nafanya kitu kilicho kizuri kwa sababu watoto hawa walikuwa katika mazingira yasiyo mazuri hata nyumba waliyokuwa wakiishi na sasa wana furaha ina maana sasa watasoma vizuri kwakuwa ada inalipwa kwa wakati,nilitumia muda mrefu kukaa hapa na nakumbuka nikiwa hapa kaka alinipigia simu na nikapokea,kaka aliniuliza "uko wapi" nikamwambia "nipo tu kwenye mizunguko ya hapa na pale" akanambia "usiwe ukawa umeenda uko gerezani" nikamwambia "hamna"" akanambia basi njoo tuonane tuongee maana sasa hivi naona unanikwepa,ukiongea na mimi kwenye simu unakuwa kama hutaki,nilipita ofisini kwako pale,mbona kama sikuelewi elewi sasa hivi" nikamwambia "kaka niko na majukumu hapa nafanya nikitoka nitakutafuta" akasema "sama kuna jambo la msingi nataka tuongee" nikamwambia "sawa".
Baada ya kuona yatosha kukaa hapo nikaondoka na kumtafuta kaka,kaka alinambia "utanikwepa mpaka lini,mimi ni kaka yako,hauwezi kunikwepa kwani damu ni nzito ndugu yangu,utanikwepa mpaka lini" nikamwambia "kaka naomba tuwe na mipaka,najua unanionea huruma sana na haupendi nipate matatizo yoyote yale lakini kaka siwezi kukata connection yoyote na mtu yule,nilimuapia mbele ya Mungu na maswali unayoniuliza sina majibu yake na kuna vitu nilikuambia siwezi kukwambia na nakusisitizia siwezi kukwambia,sijui alipopata pesa na hajawahi kunambia alipozipata ninachojua ni pesa halali na zinasaidia watu kwa namna moja au nyingine kwani wenye uhitaji wanapata mahitaji hilo ndio latosha na mimi wajibu wangu ni kutimiza kile ambacho angekitimiza yeye kama angekuwa uraiani,sijaona kosa langu na kama kutakuwa na hukumu mimi nipo tayari kwa kuhukumiwa lakini si kwenda kinyume na makubaliano na yule mtu,adhabu yangu itakuwa ni kubwa sana,moto wangu utakuwa ni wa kuni zilizochochewa sana,siwezi kufanya hivyo kwani naona unajisumbua sana kwa kutumia maneno mengi ya kuniogopesha,niko tayari na kama kuna watu wananifatilia acha wanifatilie nitawajibu majibu ambayo naamini wanastahili kuyapata" kaka akashangaa na majibu yangu na akanambia "huyo mtu ni bora kuliko ndugu yako wa damu? Nikamjibu "ndugu si kuzaliwa tumbo moja tu,ndugu anaweza zaliwa tu katika maisha ya mtu na sio lazima mtoke ukoo mmoja,mtu huyu amenifanya mimi kuwa ndugu yake na ameweza kunieleza mambo ambayo hakuweza kumueleza hata ndugu zake na amenieleza mimi,kaka umesema vyema kwanini anieleze mimi,ameniamini kwa udogo wangu,ameamini kwenye utu nilio nao ndani yangu,unajua kaka mimi ni mtu wa haki na nimekuwa mtu ambaye sipendi kutamani vya mtu mwengine,sijatamani vitu vyake,waweza kuona kama niko katika utumwa lakini mimi sioni kama utumwa kwa sababu ni kweli pesa ni za kwake si za kwangu" kaka akanambia "utakuja kustuka umechelewa sana,huu ni ujinga,yaani wewe akili zako bado changa,mjinga wewe,hujielewi na hauelewi ninachokisema" tulizozana na kaka na kunipa maneno yakunicrush lakini sikujali wala nini,sitaki kuyafata wala kuyaweka moyoni anayoniambia,yeye amepata wapi jina atajua mwenyewe japo iliniogopesha sana kwakuwa mimi sikumtajia majina ya yule mtu.
Niliendelea na maisha yangu huku maswali yakiwa mengi sana,wanajamaa wakawa wanaulizana,yaani mfano hapo mtaani kwenu kuna mshkaji unamjua ile kiundani yaani kindakindaki na hata mzunguko wake wa pesa alafu ghafla anaibuka na kufanya mambo makubwa hadi kuagiza magari,anafungua mabiashara na unasikia taarifa zake za mambo yake ya fedha hapo lazima watu wahoji,amepata wapi pesa zote hizo,tunamjua mtu huyu alikuwa fukara wa kutupa imekuwaje leo? Kwa kupitia mimi nimeamini pesa zinaweza kumfikia yoyote kwa njia yoyote kwani kwangu zimekuja katika mazingira ambayo sikuyatarajia.
Nasikia ndani yangu kumtembelea mshkaji,nasikia sana lakini kwa sababu nilipatwa na hofu nikajikuta siendi na nikaendelea kutulia na kuendelea kuchonga mipango mingine zaidi na zaidi,ninapoona kuna sehemu ya kuwekeza nafanya hivyo na nilielezwa kuna eneo la madini na watu walinipa maelezo kwa undani zaidi na nikaambiwa ukitupa pesa yako uko hautapoteza hivyo nikakata shauri kusafiri kabisa kwenda uko ambako ndiko kunafanyika hiyo biashara ili kujiridhisha,nilienda na nilikaa takribani mwezi mmoja.,kwa huo mwezi wote sikuwa najishughulisha na chochote zaidi ya hayo masuala ya madini lakini nikiwa napata mrejesho kwa biashara zangu nyingine kujua maendeleo yake na nashukuru Mungu kwenye magari kulienda poa kwakuwa niliwapa watu sahihi,watu waaminifu na wenye kujielewa,chombo cha moto usipokuwa na watu sahihi tegemea majanga na kwakuwa mimi nimetokea katika mambo ya magari haikuwa tabu kwangu kupata watu hao na niliwawekea kiwango rafiki ili wote mimi na wao asiumie yoyote kati yetu,sote tunufaike na hata wao walipokuwa wakinihoji kuhusu pesa zangu niliwajibu "usiniulize maswali mengi sana hata wewe majira yatakujia na utapata pesa kikubwa fanya kazi kwa uaminifu" hayo ndio yalikuwa majibu yangu,sasa naitwa bosi na mambo kiukweli yalibadilika sana kwangu,nilitazama biashara ya madini na nikapata elimu ya biashara hii nikaona iko powerful,nikaona nina sababu ya mimi kutupa kete huku kwa jinsi ambavyo niliiona,kwa jinsi ambavyo nilituliza akili yangu,sina elimu kubwa lakini nina utulivu sana wa akili na katika neema ya pesa niliyopata huwezi amini nilichanganyikiwa siku nimeziona zile pesa,nilipata mshtuko (hata wewe waweza kukutana nayo hiyo hali)ukifikiria wingi wake na tena zinakuja kuwa za kwako wewe ndio mmiliki lakini namshukuru Mungu katika hali ya kupata pesa na kuwehuka nilipowehuka mara ya kwanza lakini sikuwahi kutumia pesa katika mambo yasiyo sahihi,mimi ni kijana nikweli,wa kijiweni ni kweli lakini sikuwahi kujiingiza katika makundi ya ulevi na vitu kama hivyo,pesa yangu inatoka kwa ajili ya kufanya kitu sahihi na sio kufuja.
Nilipokamilisha lililonipeleka kule machimboni nikarejea zangu na nyakati hizo kaka aliendelea kunijafuta lakini wakati mwingine nilimfungia tu vioo kwakuwa alivyokuwa anazidi kuniambia nikawa naona kama napokea vitu ambavyo vinaharibu akili yangu lakini ni kaka yangu unajua siwezi kumkwepa siwezi kumfukuza siwezi kumkataa kwahiyo tulikutana niliporejea akanambia" vipi mwenzetu unasafiri unaenda mkoa kienyejienyeji tu" nikamwambia "kaka niko busy sana,niko busy sana" akasema "busy unamtumikia mtu? Yaani nguvu zako,akili zako mdogo wangu tena Mungu amekubariki una kipaji,una kipaji cha biashara unajua,mimi ndio najua hiyo siri kama hujui ndio maana watu wanakutumia,yule mtu atakuja kufight siku anatoka gerezani" nikamwambia "kaka mbona wewe unazungumza vitu vingi,umenitajia majina ya huyo mtu,umenambia hawezi kutoka atafia gerezani mara unaniambia siku atatoka je nielewe lipi" akasema "wewe ndio unaelewa zaidi,wewe si ndio unataka kumfaitia atoke" nikamwambia "kaka nisamehe mimi niliyekueleza ukweli" akasema "sio hivydn mdogo wangu,sio hivyo mimi nimekuja hapa tuzungumze jambo" nikamwambia "kaka sitaki kuzungumza jambo lolote,unaharibu sana akili yangu nakuomba kama kuna mengine yakuzungumza tofauti na ya yule sawa"
Nakumbuka kaka maneno alizidi kuzungumza na mimi lakini zaidi kaka aliniambia "nina shida na pesa" na mimi kaka akiniambia ana shida na pesa wala sioni ugumu moyo wangu kumpa pesa,nilimuuliza "kaka una shida na kiasi gani cha pesa" aliniambia ana shida ya milioni mbili ya kitanzania na nikamwambia "sawa kesho utapitia pale dukani kwangu" yaani pale kwenye duka langu la nafaka,akasema "sawa,tupate muda wa kuzungumza mdogo wangu acha kutumika tu,unatumika tu na mtu kwa sababu gani wakati unaweza kujisimamia mwenyewe" nikamwambia "kaka sawa na ninakuelewa unachosema lakini nakushukuru kwa ushauri" Kiukweli ingawa nilikuwa na woga kwa maneno ya kaka lakini toka nimerejea kutoka kule machimboni hamu ya kwenda kumtembelea mshkaji ilinishika sana,nilijiambia ngoja niende kwani sina namna na nakumbuka nilienda gerezani na nikapata chance ya kumuona na ujue sijaja siku nyingi,mshkaji alifurahi kuniona lakini akanambia "Rojas mbona tena umepotea? Nikamjibu "kwani napaswa kuwa nakuja mara kwa mara kiasi hicho? Akanambia "kwanini Rojas unanijibu hivyo bwana ? Mimi ni ndugu yako na wewe si nimekuambia ndio barua yangu wakunijulisha watoto wangu wanaendeleaje,nitapata wapi taarifa ya kujua maendeleo yao,je wanaishi mazingira gani? Sina chochote kutoka kwako zaidi ya kunieleza kuhusu hali ya watoto wangu" nikamwambia "unisamehe bure nina mambo nimekuwa nikiyafatilia na yamekuwa yananikeep busy" akasema "najua lakini nipe taarifa za watoto" nilimpa picha za watoto ambazo nilipiga nao nyakati flani nilipokuwa nimeenda kuwaona,alifurahi sana,kiukweli alifurahi sana,akanambia "mbona Rojas huna raha? Huna raha nakuona" nikamwambia "mimi nina raha tu,ninakufurahia kwa sababu una furaha" akasema "vipi kuna kitu hakiko sawa?
Nikamwambia "kila kitu kiko sawa" nikamuuliza "haujatamani kutoka hapa na siku moja kuwa huru? Akanambia "hakuna mtu hatamani kuwa uraiani" nikamwambia "unazo pesa za kutosha kwanini tusipiganie utoke gerezani,kuna faida gani ya **** na pesa zimehifadhiwa mahali zaidi ya kufanya kitu cha thamani ya wewe kuwa huru,unajua uhuru ni bora kuliko pesa? Akanambia "Rojas sentensi hii unaizungumza mara nyingi kwa sababu una moyo wa ajabu sana wewe mtu,najua unatamani nitoke lakini Rojas ni ngumu sana kunielewa" nikamwambia "niambie tu mimi nitakuelewa kwanini tusipiganie katika hili" akaniambia "Rojas nafurahi umekuja kwa sababu kuna kitu nataka nikwambie cha msingi sana" nikamwambia "ni cha tofauti na chochote ambacho umewahi kuniambia? Akaniambia "inawezekana,naona unanisisitiza sana kuhusu hili,nitakwambia,nitakwambia sababu" nikiwa hapa ananambia jambo mtu huyu.
Mtu huyu aliniambia "Rojas kwa mfano leo umekuja,nashukuru sana lakini kuna shida kidogo naomba ustop kuja hapa" niliposikia maneno haya nilishtuka sana na nikamwambia "kwanini? "Yaani Rojas kuna vitu vingi sana,kuna vitu vingi hadi nahisi kuchanganyikiwa" nikamwambia naomba aniambie ukitilia maanani kaka ameshaniambia hiyo sentensi,hivi vitu anavyoniambia pengine kweli kaka vitu anazungumza labda vina ukweli,nikamwambia "kwanini unashindwa kuniambia,niambie" akaniambia "kuna mtu yoyote ambaye ulishawahi kuzungumza nae chochote kuhusu mimi? Nikamwambia "hapana" akaniuliza "ni kweli Rojas? Nikamwambia "ni kweli" "mimi ni ndugu yako Rojas nieleze tu" nikamwambia "hapana,hapana kabisa" akanambia "nakuamini,hata mimi nilipopata hizo hisia nikakataa hizo hisia,nilisema hapana kwanza ni mapema sana,namjua Rojas hawezi kutoa siri yetu kwa mtu yoyote yule" nikamwambia "kwani kuna nini,kuna kitu gani mbona unanipa wasiwasi,kuna nini? Akasema "usije hapa,naomba uwaangalie watoto wangu kwa uaminifu kama tulivyokubaliana,najua una vingi umeplan kufanya,naomba ukavifanye na mimi niko pamoja na wewe" nikamwambia "unamaanisha nini? Akanambia "namaanisha niko gerezani lakini nipo uraiani pia macho yangu yanakutazama Rojas" nikamwambia "unamaanisha nini mbona unaniambia sentensi kama hiyo" akasema "sisi ni marafiki,sisi ni ndugu Rojas na kama muda wote nakuwaza si ina maana nakuwa pamoja na wewe,ndani yangu hisia zangu ziko sana kwako kwahiyo muda mwingi nakufikiria" nikamwambia "sawa,sasa nitumie muda gani kukb ndio nije nikuone" akasema "itapendeza kama miezi sita bila kuja kuniona na mimi nakutakia mafanikio na usisahau kwenda kumtembelea tena yule dada (yaani yule mwanamke wake)naomba utimize ahadi yako" nikamwambia "naomba uniambie kitu" akasema "sina cha kukuambia kwa sababu kama ungekuwa umemwambia mtu siri yetu ningekwambia lakini kwa sababu haujamwambia mtu yoyote sina hata sababu ya kukwambia kwani haina maana" nikamwambia "nambie" akasema "haujamwambia yoyote kwanini nikueleze haya" yaani moyoni natamani kumwambia nisamehe niliteleza nilimwambia kaka,naogopa nawezaje kusema wakati nilimuahidi ahadi hii kubwa kuwa sitatoa siri,nimekuwa dhahifu nimetoa siri nikazidi kumsisitiza "niambie,niambie,niambie" akaniambia "haujamwambia mtu yoyote kuwa na amani haya yote ntayamaliza mimi mwenyewe nenda tu,nenda tu Rojas usiwe na wasiwasi" nikamwambia "sasa kuna mazungumzo nataka tuongee kuhusiana na biashara" akasema "yote,yote hayo kayafanye vizuri usije,usije huku kabisa" nilitishika na maneno ambayo alinambia huyu ndugu na mimi nashindwa kumwambia ukweli wa mambo jinsi ulivyo.
Itaendelea!