Mkasa wa kusisimua wa Rojaz katika kipindi cha sitasahau cha radio free africa
Sehemu ya 6
Kiukweli niliondoka pale magereza akili yangu ikiwa haijakuwa sawa na fikara nyingi zikiwa zimenitinga na kujiuliza sana huyu mtu amesema anataka kunipa utajiri,utajiri huo atanipa katika mazingira gani? Je atatoka? Je kuna mtu atanambia nikamuone? Au nini ni nini katika sakata hili? Kiukweli sikuweza kumuelewa hata kidogo huo utajiri napewa katika njia gani😂
Siku zikakatika nami kama kawaida yangu nikawa naendelea na mishe zangu zakusaka mkate wangu na pia bila kusahau wale watoto wa huyu ndugu sikuwatupa kwani pale ninapopata japo kidogo nilikuwa naenda kuwatembelea nao wakawa wanaifurahikia hali hiyo pamoja na mama yao,kiukweli nilijitahidi kuziba pengo la huyu ndugu yangu ambaye alikuwa katika mikono ya dola na ilikuwa haijulikani ni lini atakuwa huru ili kuweza kujumuika tena na wapendwa wake.
Baada ya masiku kadhaa ya mihangaiko hatimaye nikaenda tena kumtembelea yule ndugu na kubwa kuliko yote ni kuona ni kwa namna gani huyu ndugu ananielezea huo utajiri alioniahidi,nilifika pale magereza na kutimiza masharti kama inavyotakikana kwa yule anayekuja kumtembelea mfungwa na hatimaye nikafika na kukutana na ndugu yule,kiukweli alifurahi sana na kunambia "umekuja ndugu yangu? nimefurahi sana sana sana na je vipi vijana ulifanikiwa kwenda kuwatembelea?"
Nikamjibu "vijana hawajambo wanaendelea salama na masomo yao na wanakusabahi sana na kiukweli wamekumiss mno" baada ya kumwambia maneno hayo alikaa kimya kwa sekunde kadhaa na akatoa pumzi kubwa ya kuonesha kama mtu aliyekuwa kwenye tafakuli nzito na akanambia "ni kweli wanangu wanaumiss uwepo wangu na najua hata mie nimewamiss sana ila ndio hivi hatuwezi kupingana na majaaliwa ila naamini uwepo wako utaziba kwa kiasi kikubwa pengo langu kwani kile ambacho nilikuwa nakipambania kwa ajili ya kesho bora ya wanangu na mchumba wangu wewe utaenda kukitekeleza kwa niaba yangu kasoro vile ambavyo tumeapizana kuwa usije ukavitenda,nimekuamini ndugu yangu na nimeamua kukuelezea siri nzito iliyokuwa ndani ya mkebe wa moyo wangu na hakuna yoyote niliyewahi hata kumpa dondoo,kufungwa kwako kulikuwa umeletwa maalum ili uje unipokee kijiti na uende kutekeleza kile nilichokuwa nakitamani kwenda kukifanya" akasita kuendelea kwa kitambo kidogo na machozi yakawa yanamlenga ila kiukweli sikuwa najua ni machozi ya furaha kwa uwepo wangu au huzuni,kiufupi sikuelewa nami nikawa kimya nikiwa namsikiliza kwa umakini maneno yake.
Akaendelea kunambia ndugu yangu mimi nina utajiri,elewa nina utajiri na ninakusisitizia kuwa nina utajiri ambao utakwenda kubadili dunia yako na kwa muda niliokaa nawe hapa gerezani naamini wewe ndio mtu pekee utakayeweza kutekeleza maagizo nitakayokupa,ninao ndugu wa damu ila kwakuwa nimekwama humu nao wamenisusa na hawataki hata kujua hali yangu je nami natakiwa kujishughulisha kuhusu hali zao? Akalitupa swali kwangu nami nikamjibu "ni kweli usemayo ila hauwezi jua wametingwa na mambo gani" akadakia "je wewe hauna mambo yako? Mbona umekuwa ukija mara kwa mara hapa kuja kunitembelea,je niseme kinachokuleta ni hili jambo? Mbona umekuwa ukija kabla yakukutamkia kuhusu hili? Wewe ni ndugu yangu na nipo tayari kukubadilishia maisha yako na ya watu wangu wa karibu,wakuwazingatia ni watoto,wewe mwenyewe,mchumba wangu na kiasi mama wa watoto ila sikukatazi kuwatizama ndugu zangu lakini kwangu hawana umuhimu wowote ni wewe tu kama itakupendeza" kiukweli maneno yake yalinivuruga sana na nikawa nataka anielezee sasa na aache kuzunguka kwani ile hamasa yakutaka kuelezwa ikawa imenipanda.
Akanambia "najua nakuvuruga ila utaenda kijiji flani (akakitaja) na uko katika iko kijiji ndipo ilipo asili ya ukoo wangu na kuna ndugu zangu wengi tu na utakapofika pale yoyote utakayeonana nae mwambie nataka kwenda kwenye mji wa ukoo flani (akautaja ukoo wake),ni ukoo maarufu sana na pale katika nyumba ya familia kuna shangazi yangu,kaka yangu mkubwa na baba mkubwa" akavuta pumzi kidogo na kuendelea "najua unajiuliza ukifika utajielezaje kwao na wasijue dhumuni lako kuu lililokupeleka uko,wewe ni mtoto wa kiume najua hautashindwa kupata namna yakucheza na akili zao,nenda kijijini nami nitakupa maelezo makuu nawe jukumu lako ni kuyatekeleza maelekezo" nikawa namsikiliza tu huku nikitikisa kichwa kukubaliana nae na ikizidi ni kusema "ndio" yule ndugu aliendelea "utakapofika pale wewe waweza kuwaeleza kuhusu mimi na kutia ufundi wako zaidi na wala usiharakishe ulichokifata,soma mazingira usiwe na pupa ukawastua kwani nimeficha hazina kubwa na hiyo haipo ndani ya hiyo nyumba kuu ya ukoo" alipofika hapo nikawa nawaza na kuwazua,akaendelea kunielekeza " pembeni mwa hiyo nyumba kuna kijumba ambacho hakijamalizwa kimeachwa kama pagale ndipo ulipo mzigo huo ninaotaka uufate,ndani ya iko kijumba kuna kitanda cha kamba na ndipo ninapotaka uende kwani hiyo hazina nimeifukia chini ya kitanda iko,zingatia mzigo huo ni wako wewe na uamuzi wakuwatizama wengine nimeukabidhi kwako" kiukweli nilivuta pumzi ndefu na kujiuliza peke yangu hiyo hazina gani na chanzo chake ni nini na kama aliyeyasoma mawazo yangu akasema "wewe ni mwanaume najua hautashindwa kuipata hiyo mali na utatoka nayo na kwenda kutekeleza yale tuliyoahidiana leo" nikawa najiuliza je ni dhahabu,almasi,pesa au ni nyara gani ambayo ndugu huyu ameniambia na kunisisitiza kuwa ni hazina na natakiwa nitoke nayo na nikishatoka nayo nisiyafungue bali nihakikishe kwa nafanya kila liwezekanalo hazina nifike nayo mjini na nikishafika tu nisichelewe na nihakikishe narudi kule magereza na kunipa maelekezo zaidi ya nini chakufanya,tukafanye maongezi na kumpa vitu ambavyo nilikuja navyo kama sabuni na vinginevyo na tukaagana na akanambia "kila la heri ndugu yangu na nategemea ndani ya muda mfupi ntakuona ukija hapa ukiwa mtu mwingine kabisa,kapambane ndugu yangu" nami nikamjibu na kutabasamu lakini ndani ya ubongo wangu sikuwa hata na chembe ya tabasamu kwani nilikuwa na mawazo lukuki nikitaka kujua hiyo hazina ni hazina gani,chanzo chake,kwanini mimi na mengine mengi yalinizonga.
Kiukweli sikuweza kukaa kwa amani kwani kila nililowaza halikuweza kupata hitimisho na nikizingatia ndugu huyu alinitaka kwenda mwenyewe na nisishirikishe mtu yoyote kwani yeye amenipa madaraka mimi na niyatekeleze mimi tu,siku hii niliingia kulala mapema na hata chakula ni kama niligusa tu na saa 1 nipo ndani ya kitanda na hata usingizi uliponichukua wala sikufahamu nilijistukia ni kumekucha na lindi la mawazo likaniandama upya😂
Nilijizoazoa hapo na kufanya usafi wa mwili huku tafakuli kubwa ikiwa ni kwa namna gani nitaweza kwenda uko kijijini kwenye hiyo "hazina" niliyoambiwa na yule ndugu kule jela,nikiwa na viakiba vyangu vya pesa nikanunua vijizawadi ili nitakapofika kule nisiwe mnyonge katika mapokezi,kwakuwa yule ndugu alinijuza baadhi ya ndugu muhimu nami nikanunua kitenge na fulana mbili na sukari kilo mbili na chumvi na hatimaye nikajikongoja na kuelekea stendi kupanda gari za kwenda uko kijiji husika,kiukweli wakati wote wa shughuli zangu za udereva sikufanikiwa kufika maeneo ya uko,kwangu ulikuwa ni mazingira mageni kabisa na kwakuwa nililazimika kwenda kukawa hakuna budi na kweli nilifanikiwa kufika na nilipofika katika kituo ambacho yule ndugu alinielekeza kushuka nilifanya hivyo,mara baada ya kushuka nikasogea ng'ambo kidogo na kukuta sehemu watu wamechangamana wakifanya shughuli mbalimbali kama ufundi na ukodishaji wa baiskeli,wauza matunda,mazao ya chakula na hata mafundi nguo,kiufupi ilikuwa ni senta flani imechangamka nami nikajongea na kuwakuta kinamama wakiwa na biashara zao za vitafunwa, nikawajulia hali na kuwauliza kama nilivyopewa maelezo na yule ndugu yangu wa jela,kiukweli ukoo wao walikuwa ni watu wanaofahamika sana na haikunipa tabu kuweza kupelekwa hadi katika mji wao,nilipewa vijana wawili wadogo ambao walisisitizwa nipelekwe hadi mlangoni,kiukweli maisha ya vijijini ile heshima kwa mgeni bado ina nguvu sana.
Nilifikishwa tena nikiwa nimebebewa ile mizigo yangu na nikatambulishwa kwa mama mtu mzima ambaye tulimkuta ndio anatua mzigo wake wa kuni na jembe,nilikuja kumjua baadae kuwa ndio yule shangazi niliyehadithiwa na yule ndugu yangu,nikakaribishwa na baada ya salamu kama ilivyo ada nikajitambulisha mimi ni nani na ujio wangu pale,nilimpamba sana yule ndugu na kuwaeleza kuwa tulikutana jela na alinisaidia sana katika kuyakabili mazingira yale kwakuwa sikuwa na nguvu yakuweza kupambana na watemi wa jela ambao wengi wao wametawaliwa na utemi hata kama haujawafanya jambo lolote,kiukweli shangazi alinikaribisha na akawaita na baadhi ya wanandugu na kunitambulisha kwao, wakati wa jioni shangazi akaniandalia maji huku akiingia jikoni na kuandaa chakula na pia kulikuwa na kijana ambaye kiuwajihi alikuwa amenizidi kama miaka miwili au mitatu sema ugumu wa maisha na msoto wa kazi ngumu kijijini yeye alikuwa amejengeka kimwili nami nikionekana kimbaumbau,nilikuja kumjua jina lake kama Kaombwe,Kaombwe alikuwa nami katika kunipa kampani na ni mtoto wa baba yake mkubwa yule ndugu yangu wa kule jela.
Chakula kililetwa kilikuwa ni ugali wa mtama na mboga ya majani na maziwa ya mtindi tukawa tunakula huku michapo ya kimaisha na Kaombwe ikawa namuelezea vitu na wema mbalimbali ambao ndugu yao tumetendeana nia ilikuwa ni kumjibu kimtindo isi ajue nia ya kunileta pale kijijini,nikajifanya kuwa hali yangu ya kiuchumi imekuwa na nafuu sana na kutokana na wema wa yule ndugu nimeonelea kuja kuangalia ni kwa namna gani nami naweza kuacha alama katika mzizi wa ukoo wake ili hata atakapotoka aone ni kwa namna gani nimeuthamini wema wake kwangu,Kaombwe alifurahia na akawa analeta maswali ya udadisi kujua kama ni muda gani watu wanavyolala jela,je kifungo uwa kinahesabiwaje,nyapala anapataje cheo iko na mengine mengi nami nilimjibu kadri nilivyoweza kwani niliamini hawa ndio wenyeji wangu na kufeli au kufanikiwa kwa jambo langu kuna mchango mkubwa kutoka kwao.
Mara baada ya kumaliza michakato ya kuoga na kula nikaelekezwa chumba cha kwenda kupumzika na ni chumba ambacho nilishea na Kaombwe,kwakuwa sikuwa mwenyeji na kuogopa kuwaboa wenyeji nikawaaga na kuingia ndani huku mawazo yangu yote yakiwa katika hazina niliyoambiwa na kwanza kukiona iko kijumba ila nikayakumbuka maneno ya yule ndugu kuwa "usiwe na papara wewe tulia soma mazingira kila linalotakikana ulifanye kwa umakini na usiwape nafasi ya kukuwekea shaka" kweli nikayazingatia,usingizi haukuja kiukweli sauti za wadudu wa vijijini,chafya za ng'ombe na hata mapito ya watu ingawa haikuwa ya kivile yote niliisikia,usingi uligoma kabisa na hata Kaombwe alipoingia ndani kuja kulala nilimsikia kuanzia anabadili nguo hadi usingizi kumchukua na kuanza mikoromo mimi sikuwa na hata lepe la usingizi,mimi kitabia kwanza eneo likiwa jipya kwangu usingizi uwa unachelewa sana kuja sasa ukichanganya na hili sakata yaani ndio kama umenambia leo mkesha umekuhusu.
Nadhani kama nilipata usingizi basi hayakuzidi masaa matatu na kilichonistua usingizi ni wenyeji wangu walikuwa wakichukua zana zao na kutaka kuelekea mashambani kwani wenyewi wa maeneo haya kwa namba kubwa walikuwa ni wakulima hivyo uwa wanajihimu mapema kwenda mashambani kabla jua halijachanganya na pale nilimsikia shangazi akiongea na Kaombwe,nyumba za vijijini hazikuwa na dari hivyo mtu aliyeko kolidoni anapotaka kumpa ujumbe aliye ndani anakuwa hapati tabu na shangazi akawa anamueleza Kaombwe asitoke abaki nami kwani wao wote wakiondoka mgeni haitakuwa vyema kubaki mwenyewe,nikajinyanyua na kutoka nje na kumsabahi shangazi nikamwambia kuna mzigo wako na nikachukua ule mfuko wenye zawadi na kumpa yeye zinazomuhusu na zile flana moja nikampa Kaombwe na nyingine nikaomba apatiwe baba mkubwa atakapoamka,kiukweli shangazi alifurahi sana maana sukari,chumvi na kile kitenge kiufupi nilimloga vibaya na hata wale wenzake walifurahia,nikawagusia kidogo kuwa kama nitajaaliwa nataka kumjengea nyumba rafiki yangu kuuenzi wema wake alionitendea.
Siku ile nilibaki nyumbani na Kaombwe tukipiga soga na tukihadithiana habari mbalimbali kama mambo ya siasa,mpira ingawa sikuwa shabiki kihivyo na hali ya mvua na ukame ambao wakulima wanakabiliana nao,kiufupi stori almradi muda usonge na ilipofika jioni watu waliokuwa wamekwenda mashambani wakawa wanarejea majumbani lakini pamoja na kubaki pale nyumbani sikuacha kuyakagua mandhari ya pale ili kuziona zile alama muhimu kama kile kijumba na kweli nilikiona kwani kilikuwa mita chache nyuma ya nyumba hiyo niliyofikia,ni kijumba ambacho kwa muonekano wake ni kama aliyekijenga hakukikamilisha ila inaonekana pamoja na kutokamilishwa kwake kulikuwa kunakaliwa uko nyuma kwani kulikuwa na matambaa kama kitenge (nadhani walifanya kama pazia)kilikuwa kimechokeana kinaning'inia katika kidirisha kidogo na mabaki ya mtungi uliovunjika na kubaki kama vipande vya vigae,sikuzunguka sana kwakuwa eneo lilipo hazina nilishaliona kilichobakia ilikuwa ni kuangalia namna gani nitaweza kuingia ndani ya pagale lile kuweza kuyaona hayo ya ndani kujua yaliyomo je yamo?
Jioni mara baada ya shangazi kurejea na kuanza kuandaa mazingira ya maakuli baba mkubwa alikuja akiwa amebeba jogoo na kumwambia Kaombwe alifanyie utaratibu,naye akalichinja na shangazi akalifanyia yanayopaswa kufanywa,wakati wa maakuli chungu kilichojaa minofu kiliwekwa mkekani na wote wakawa wananisisitiza mie kula kwani kuku yule haswa alikuwa ni wangu na wao wananisindikiza tu.
Siku ikaisha na mimi na Kaombwe baada ya muda mfupi tukajongea kuingia ndani kuimaliza siku na kuisaka siku mpyaambapo asubuhi na mapema wale wa kwenda mashambani wakaenda uko na Kaombwe akanambia kwakuwa nimemgusia nia yakutaka kumjengea rafiki yangu yeye anao vijana ambao anaweza kuwaandaa kwa ajili ya kunisaidia katika ujenzi nami nikamwambia ngoja tu wala hasiwe na shaka kikubwa natizama mandhari kwanza alafu kuna mambo nayafikiria ndio tutaangalia njia bora zaidi na baada ya muda akanitaka radhi na kuniaga kuwa anaenda kijiji flani kuna harakati zake akaweke sawa na hadi mchana tu angekuwa amesharejea na kunitengenezea yale mazingira kama ya kifungua kinywa na mengineyo,mara tu nilipohakikisha kuwa Kaombwe ameshaenda zake na mji ulikuwa kimya kwakuwa mazingira pia ya mji wao yalikuwa yamejitenga na kuzungukwa na mashamba yao ya familia,nikajongea kuelekea katika lile pagale kuweza kujiridhisha na yale maelekezo ya ndugu yangu na nilipofika nikawa naupambua utando wa tandabui ambao ulikuwa umesambaa katika kijumba kile na kusogeza kimlango kilichokuwa kimeshikiliwa na bawabu moja kwa juu,nikausukuma na kuingia ndani huku nikiyapa nafasi macho yangu kutengeneza nuru ya kuweza kuona vilivyomo ndani.
ITAENDELEA!