Sababu walizoeleza Yanga kwa nini hawataki kulipwa sawa na vilabu vingine ni za kitoto, ni kweli wao ni klabu kubwa ni sawa na Simba lakini lazima wakumbuke Azam Media group hawadhamini vilabu wao wanadhamini ligi sasa labda watuambie hao vilabu vikubwa kama wanaweza kucheza ligi bila hivyo vilabu vingine wanavyoviita vidogo.
Na kingine watwambie mgawo wanaopata kutoka Vodacom je ni tofauti na mgawo wanaopata vilabu vingine? Je vipi kuhusu gate collection wanapocheza na hivyo vilabu vidogo wanagawana sawa au Yanga kwa sababu ni klabu kubwa wao wanapata zaidi? Na kama wanapata sawa kote huko kwa nini hizi za Azam wanataka wapewe tofauti na wengine?
Wao kama ni klabu kubwa na wanaamini wanaweza kuingiza hela kutokana na ukubwa wao si watafute wadhamini wengine kama vile walivyopata kutoka TBL. Yanga wanatakiwa wakubali hicho kiasi ili Azam waonyeshe hiyo ligi na timu ndogo kama ndugu zao Toto wasiwe wanawagharamia siku wanacheza na Simba.
Suala la kwamba tenda haikuwa wazi mimi sina uhakika nalo lakini TFF wenyewe wanasema dau la Azam ndo lilikuwa kubwa zaidi kuliko la supersport sasa wao walitaka supersport wapewe eti tu kwa sababu wanaonekana
sehemu kubwa Afrika kwani Yanga wanafanya biashara gani nje ya Tanzania wanataka waonekana nje? Wao si ni wa hapa hapa tu.
Kusema kwamba wana ugomvi na Azam wa kimchezo na wanatolea suala la Mrisho Ngasa kama mfano sio sawa, labda Yanga wangeweka wazi kwamba ugomvi wao na Azam ulianza lini? Je ulianza kipindi kile Yanga wanafungwa mfululizo au ulianza tu baada ya wao kumuuza Ngasa kwa Azam? Au ulianza pale Azam walipotaka kumuuza Ngasa kwa utovu wa nidhamu alivyoibusu jezi ya Yanga huku akijua yeye ni mchezaji wa Azam? Ieleweke Yanga walitamka wazi kabisa kupitia kwa aliyekuwa katibu wao (Mwesiga) Ngasa hakuwa na thamani ya zaidi ya TZS.20M kwa hiyo wao wasingeweza kutoa zaidi ya hapo, sasa wanapotaka kutuaminisha kwamba Azam hawakutaka kuwauzia Yanga si kweli ila wao walitaka wampate kwa bei chee sababu Ngasa anaipenda Yanga.
Ninachoona hapa kwa sababu ni ngumu kutofautisha Azam FC na makampuni mengine ya Bakhresa na Bakhresa mwenyewe kama ilivyo ngumu (kwa sasa) kutofautisha Yanga na Manji, nalazimika kuamini Manji na Bakhresa watakuwa na msuguano wao wa kibiashara, nalazimika kuamini hivyo kwa sababu makamu mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga na katibu mkuu Mwalusako walishiriki vikao vyote na hoja zao zilijibiwa na wenyewe wakaondoka kwenye vikao wameridhika iweje leo wageuke, je ni shinikizo la mwenyekiti Manji au ni shinikizo la wajumbe wengine wa kamati ya utendaji? Kwa vyovyote vile mwenyekiti Manji ni kila kitu kwa Yanga (kwa sasa) hivyo lazima atakuwa yeye ndo aliyebatilisha waliyokubaliana kina Sanga kwenye vikao.
Hoja ya kwamba Azam Media Group hawawezi kudhamini kwa haki kwa sababu nao ni washiriki kwenye ligi haina uzito kwa sababu kuna mifano ya makampuni yanayodhamini ligi za nchi mbali mbali na yenyewe yakiwa na timu inayoshiriki kwenye ligi hiyo; mfano: Supersport wana timu inayoshiriki ligi kuu ya Afrika kusini na wao ni wadhamini wa ligi hiyo; EABL wanadhamini ligi kuu ya Kenya na wao wana timu inayoshiriki hiyo ligi; Mashindano ya vilabu ya CECAFA yanadhaminiwa na Rais wa Rwanda ambaye ndo Amiri jeshi mkuu wao na mara nyingi timu ya APR ambayo ni timu ya jeshi inashiriki haya mashindano, kama haitoshi Manji aliongeza udhamini wa mashindano ya CECAFA ya vilabu huku akijua kwamba yeye ni mwenyekiti wa Yanga na timu yake mara nyingi inashiriki kwenye hayo mashindano.