Mke asiye na mume, akamchumbie nani?

Mke asiye na mume, akamchumbie nani?

vukani

JF-Expert Member
Joined
Dec 30, 2009
Posts
244
Reaction score
166
Isingekuwa vigeni, mwanamke kuchumbia
Ningepita mitaani, mume kujitafutia,
Nisimuudhi Manani, ndio nimejizuia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Ndege maingainga, si jambo la kujitakia,
Mume mwema natamani, vipi tajitafutia?
Na mwanamume haini, sitaki kunichumbia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Nimetulia nyumbani, sina mume kunioa,
Wanifuatao ndani, si wachumba wa kuoa,
Hutaka kunirubuni, maasini kunitia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Ndege maingainga, si kosa langu sikia,
Niliolewa zamani na mume mwenye udhia,
Kanitia kilabuni, pombe kumchuuzia
Mke asiye na mume akamchumbie nan?

Mimi nikamuamini, huku machozi nalia,
Mume hii kazi gani, alokataza jalia?
Kheri tukate kuni, mimi nitakuuzia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Akapanda hasirani, na maneno akafyoa:
Mke wee mke gani, dini lini ulijua!
Alipozidisha kani, ndoaye nikajivua.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Wako mabwana wa shani, ningependa kunioa,
Hawamtii shetani, Munguamewaongoa,
Nao wamomashakani, kwa mabibi walooa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Tu wema hatujuani, wake na waume pia,
Twaingia mashakani, kwa wenzi waso murua,
Namlilia Manani, mume mwema kunioa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Nawe muombe, ndoa yenu kutulia,
Tusikuone mwakani, viragoumepania,
Mke na mume nyumbani, mumche Mola Jalia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Shairi hili limetungwa na Sheikh Amri Abedi, nami nimeona niliweke hapa.
 
Malenga nakusalimu, heshima zote pokea
mchango wako muhimu, sote twaukubalia
swalilo kweli gumu, ila pole kwa kufiwa
mke asiye na mume, asubiri tachumbiwa!

Mvumilivu hula mbivu, wahenga walishasema
subiri ufike Kivu, Moshi na Dari salama
usikubali uvivu, hata ukipata homa
mke asiye na mume, asubiri tachumbiwa!

Kosa la kwanza si kosa, ila kosa kurudia
subiri takuja posa, bora mwema kubakia
simwumize wa Kilosa, kwa kosa la Majalia
mke asiye na mume, asubiri tachumbiwa!
 
Back
Top Bottom