SoC02 Mke wa Kabwela

SoC02 Mke wa Kabwela

Stories of Change - 2022 Competition

Kritiko X

New Member
Joined
Jan 11, 2019
Posts
1
Reaction score
0
Habari wana JF
Nipo hapa kushiriki shindano la "stories of change"
Andiko langu limetokana na kisa kinachomuhusu dada mmoja ambaye alifika ninapoishi akiwa na wanawe kutafuta kazi
Mazingira yake (ambayo huhitaji kuwa daktari wa falsafa au saikolojia kung'amua kuwa ni magumu mno)ndiyo yaliyonipa msukumo wa kusema jambo kumuhusu kwa mtindo wa hadithi ambayo nimeisimulia kwa lugha ya ushairi(kwa sehemu kubwa)
Nafahamu wapo wengi wenye hali sawa na yake,na pengine kupitia andiko hili tunaweza sukumwa kufanya jambo.Asante na karibuni!

********************************
Mke wa kabwela na wanawe,

Mmoja mdogo mgongoni na mwingine mkubwa kidogo akiwa anatembea mwenyewe

Wanapita mtaani wakibisha hodi majumbani na kueleza shida yao

Hawaombi chakula wala maji,bali wanatafuta kazi

Tena hawana makuu,wanataka yoyote ile iwe ya kufua , kuosha vyombo au pengine hata kufagia ili mradi tu wajipatie riziki

Hadi inapotimu saa saba mchana hakuna mafanikio, nyumba zote jibu ni lilelile,"hakuna kazi,jaribuni kwingine"

Mama mtu amejawa uchovu lakini hawezi thubutu kuacha wala kukata tamaa,Ni lazima waendelee

Watoto nao wanalalamika njaa,tena yule mdogo inamliza kwa sauti njia nzima,namna gani isivyo na haya wala huruma

Masaa kadhaa baadaye wanakaa chini ya mti pembezoni mwa njia walau wajifute vumbi na kupumua.kitinda mimba wake amenyamaza kulia kinywa kikiwa wazi na mwili umemlegea

Leo ni miezi kadhaa tangu kabwela,baba wa familia,awatelekeze na kukimbia

kazi yake ilikuwa ukonda wa daladala,kazi iliyomuamsha mapema kuliko kawaida na kumrudisha nyumbani muda wa kulala

Ni ama hakuwa akipata kipato cha kutosheleza au pengine kuna anasa aliendekeza

Maana siku zote nyumbani hali ilikuwa mbaya na yeye naye alikuwa mtu wa kulalamika

Lakini japo maisha yalikuwa magumu hayakuwa kama ilivyo sasa

Mama ameachwa na familia na ni mwezi tangu kodi ya kibanda walichopanga imeisha

Yeye na wanae hawana msaaada na wanaishi kwa kutangatanga

Wakipata wanakula,na wakikosa wanapokea chochote watachopewa wanapoomba kwa wasamaria

Hawana makazi maalumu wala ya kudumu, hivyo popote giza linapowakuta ndipo wanapolala

Yeye na kabwela walikutana tu kimjini mjini wote wakiwa wamekuja kutafuta

Matarajio yao ni kwamba wakiishi pamoja,itasaidia kupunguza ukali wa maisha

Maana kila mmoja atachangia anakachokipata ,kama walikuwa sahihi ama vinginevyo mimi sijui

Lakini walipoanza kuishi pamoja kabwela akabadilika akamwambia anataka abaki nyumbani alee familia

Sababu Kwa desturi za kwao anapotoka,yeye ndiye anatakiwa kutunza nyumba

Kabiashara kake ka genge kakafa na
Mtaji wake nao kabwela akautaka

Basi akabaki kusubiri kuletewa na alichoachiwa mezani hakikutosha kuhudumia nyumba.Hata kuunga mboga tu ilikuwa anasa kubwa.

Hapo mtoto alikuwa mmoja tena bado mdogo,waliopoongeza mwingine
Maisha yakawa magumu zaidi

Habari mbaya kuliko,kabwela kazi akasimamishwa na akiba waliyokuwa nayo haikuwatosha

Kulala njaa ikawa kawaida na madeni waliyokopa hawakuweza tena kuyalipa

Kila kabwela alipotafuta kazi alikosa na hata vibarua alivyojishikiza havikudumu

Ikawa kawaida kuuza vitu vyao vya ndani kidogokidogo ili kutafuta unafuu Kila wanapokwama

Mwishowe chumba kikabaki cheupe,na familia nzima ikalala juu ya vipande vyake vya kanga

Nyumba ilinuka vundo la shida

Kabwela akaanza tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani tena anafika amelewa
Punde si punde akawa analala nje kabisa na hataki auulizwe sababu
Kabla bibie hajajua la kufanya, akatoweka moja kwa moja na hajawahi kurudi tena

Akiwa hana ndugu wala shughuli ya kufanya mjini,akaachwa mwenyewe kwenye kisiwa kilichozungukwa na bahari yenye dhoruba za shida na mateso kila upande

Macho ya watoto na matumbo yao yanamtazama yeye

Akaanza kuchakarika,na mungu hana choyo kwa mtafutaji

Akapata kazi kwa mama ntilie mmoja mjini

Majukumu yake yalikuwa ni kufwata mahitaji sokoni,kusaidia jikoni na kuosha vyombo

Malipo yalikuwa chakula, chake yeye na wanaye, pamoja na posho kidogo ya kufutia jasho

Kwa kudra zake Mungu na nidhamu yake ya akiba,akamudu kulipia pango

Hii ni kabla ya mgahawa wa mama ntilie aliyemuajiri haujafungwa,maana wateja wao waliowategemea walihama baada ya kuvunjiwa vibanda vyao vya biashara

Akarudi tena alipoanzia

Na kama mkosi,kila alipojaribu tena kutafuta kazi hakuwahi kufanikiwa

Ndipo wazo la kuzunguka majumbani likamjia

Kila siku asubuhi na mapema yeye na wanae wanaanza kupita nyumba moja hadi nyingine

zipo wanazofunguliwa mlango na kusikilizwa
Kwingine kutokana na muonekano wao usioridhisha wanafukuzwa kabla ya kusema kilichowapeleka
Wengine wanaishia tu kumuonea huruma na kutoa pole,japo inawafariji, yeye na wanaye walihitaji zaidi pesa

Kwa siku mbili mfululizo sasa hajapata tenda yoyote

Na hakuna walichotia mdomoni tangu siku iliyopita zaidi ya vikombe viwili vya uji wa ulezi waliopewa na msamaria mwema

Kama tujuavyo tumbo husahau mapema,hivyo kila uchwao linadai tena na tena kupatiwa huduma. Na kwa binadamu asiye na nyenzo za kulitimizia kila inapobidi na kwa kiwango linachohitaji,haachi kusumbuliwa

Mama na wanawe chini ya kivuli cha mti,kilichowakinga dhidi ya miale mikali ya jua lenye nguvu lakini hakikuwa na jeuri ya kuwakinga dhidi ya magumu ya maisha wanayopitia,hali zao dhoofu na matumaini yao hafifu

Watu kadhaa wanapita pale njiani wakienda na kurudi,pengine nao wana shida na matatizo yao binafsi yanayowafanya wapite pasi kushtushwa na wanachokiona, ama pengine watatu kama hawa si wa kwanza kuwaona maana siku hizi hali ngumu imetapakaa kila kona.

Usiku unapoingia mama mtu anaamua leo watalala hapa hapa na kesho wataona nini cha kufanya,japo alijua kabisa watarejea tena kwenye utaratibu uleule na kuendelea walipokomea labda muujiza utokee.

Ndani ya fuko lake yapo mapande kadhaa ya vitambaa

Kati ya yaliyopo anachukua baadhi na

kuyatandaza chini tayari kwa kulala

Mtoto mkubwa anatangulia kujilaza ,huku mikono yake iliyojaa mifupa kuliko misuli ikiwa imelikumbatia tumbo lake lililotepeta na kuingia ndani.

Mama mtu anahangaika kufungua kanga yake ila amshushe mdogo wake,ambaye kwa muda mrefu yupo kimya mgongoni

Anapofanikiwa anagundua kuwa ukimya huo ni kwa sababu mwanaye ameshalala muda mrefu,na katu hatamlalamikia tena njaa wala kumsumbua maana tayari alishaaga dunia!

Asante kwa kusoma,karibu kwa maoni.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom