Wakuu kwema?
Katika pitapita zangu mtaani nimesikia barabara ya Njombe - Songea imejengwa na Malkia wa Uingereza na kwamba Hayati Queen Elizabeth II ndiye mmiliki wa mashamba ya chai maeneo hayo.
Ila kubwa zaidi ni kuwa, Njombe kuna kijiiji kizima ambacho ni mali ya Malkia huyo. Je, hili lina ukweli ndugu zangu?
- Tunachokijua
- Mkoa wa Njombe ulianzishwa Machi 1, 2012 na kutangazwa katika Gazeti Rasmi Na.9 kwa agizo Na.72. Katika kutekeleza madaraka aliyopewa Rais na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 2(2), mkoa wa Njombe ulianzishwa baada ya uamuzi wa Rais wa kuupanga mkoa wa Iringa kuwa mikoa miwili ya Njombe na Iringa.
Mkoa umegawanyika katika Wilaya nne ambazo ni Njombe, Wanging’ombe, Makete na Ludewa. Pia kuna Mamlaka za Serikali za Mitaa sita ambazo ni Halmashauri za Mji wa Njombe na Makambako, Halmashauri za Wilaya za Njombe, Makete, Wanging'ombe na Ludewa.
Mkoa upo katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Njombe na sehemu ya Mikoa ya Morogoro. Imepakana na Mkoa wa Iringa upande wa kaskazini, Mkoa wa Morogoro upande wa mashariki na Mkoa wa Ruvuma upande wa Kusini.
Jamhuri ya Malawi kupitia Ziwa Nyasa na sehemu ya Mkoa wa Mbeya inapakana na Mkoa wa Njombe upande wa Kaskazini-Magharibi, wakati upande wa Magharibi mipaka inashirikiwa na Mkoa wa Mbeya tena.
Mkoa wa Njombe una jumla ya eneo la kilomita za mraba 24,994 kati ya hizo kilomita za mraba 21,172 na kilomita za mraba 3,822 zimefunikwa na ardhi na maji mtawalia.
Makabila asilia ni Wabena, Wakinga, Wapangwa, Wamanda, Wanyakyusa, Wanji, Wamagoma, Wamahanji, na Wakisi.
Madai ya uwepo wa Kijiji Mkoani humo kinachomilikiwa na Hayati Malkia Elizabeth II
Kutokana na uwepo wa madai haya, JamiiForums imezungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri Njombe, Kuruthum Amour Sadick anaelezea anachokifahamu:
"Tangu nimefika Njombe, kuna sehemu ya mashamba ya Chai ambayo inamilikiwa na Wazawa na nyingine inamilikiwa na raia wa Kenya.
Sehemu nyingine kuna wawekezaji wadogowadogo wazawa ambao nao wanafanya shughuli za zao la chai, katika majukumu yangu hakuna sehemu ambayo nimekabidhiwa na kuelezwa kuwa sehemu fulani inamilikiwa na Malkia au familia yake.
Ninachokijua hata wamiliki wa mashamba ambao tulikuwa tunawadai kwenye masuala mbalimbali ni raia wa Kenya na nilikutana na Mkurugenzi wao Mkenya kujadiliana naye kuhusu malipo waliyokuwa wakitakiwa kulipwa.
Nitafuatilia kama kuna kitu kama hicho, naamini kama kingekuwepo tungeona hata kwenye masuala ya vibali ambavyo vinatumiwa wakati wa malipo na wakulima wenyewe au wamiliki wa mashamba.”
Malkia wa Uingereza, Elizabeth II alifariki dunia Septemba 8, 2022 akiwa na miaka 96 huku akiwa ni Kiongozi wa Kifalme aliyetawala kwa muda mrefu zaidi (miaka 70) katika historia ya Taifa hilo.
Kufuatia kifo chake, mtoto wake mkubwa, Mwanamfalme Charles, ndiye alirithi mikoba ya utawala.