KWELI Mkojo wa Sungura unaweza kutumika kama mbolea na dawa ya kuulia wadudu kwenye mazao

KWELI Mkojo wa Sungura unaweza kutumika kama mbolea na dawa ya kuulia wadudu kwenye mazao

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Nimekuwa nikiona wafugaji wa sungura wakivuna mkojo wa wanyama hao na kudai kuwa unaweza kutumika kama mbolea na dawa ya kuulia wadudu kwenye mazao. Wakuu wa JamiiCheck uhalisia wa hili ni upi?
1751656259597.jpeg

​
 
Tunachokijua
Sungura amekuwa ni mnyama pendwa wa kufugwa hasa kwa rika la watoto na vijana. Amekuwa akitumiwa kama kitoweo kinachowavutia watu wengi hivyo kumfanya kuwa na thamani zaidi. Wigo wa matumizi ya mnyama huyu umeongezeka kutokana na baadhi ya watu hasa wakulima ambao wamekuwa wakitumia mkojo wa Sungura kama kiua wadudu na mbolea kwa mazao.

JamiiCheck imepitia tafiti mbalimbali za kisayansi, kutaka kupata uhalisia juu ya matumizi ya Mkojo wa Sungura kama una mchango wowote katika kupambana na wadudu waharibifu kwenye mazao pamoja kuongeza rutuba kwenye udongo na kuchochea ukuaji wa mimea.

Kwa mujibu wa Utafiti uliochapishwa katika jarida la MDPI unabainisha kuwa mkojo wa sungura umekuwa ukitumika kama dawa ya asili ya kuua wadudu na kuzuia magonjwa hatari yanayoathiri mazao. Mbali na kutumika kama kiua wadudu, mkojo wa sungura pia ni mbolea bora ya kikaboni. Kwa mfano, mkojo wa sungura umetumika kama mbolea hai kuboresha uotaji na ukuaji wa mazao.

Utafiti huo unazitaja nchi za Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi na Nigeria ambazo zimekuwa zikitumia mkojo wa Sungura kama kiua wadudu na mbolea. Kwa mfano, nchini Uganda ilibainika kuwa matumizi ya mkojo wa sungura uliokusanywa shambani huongeza rutuba ya udongo na kuua wadudu waharibifu.

Wakulima wadogo wameripoti kuwa kunyunyiza mkojo wa sungura kwenye mimea husaidia kudhibiti wadudu wengi waharibifu, hasa viwavi, aphids, nondo, wadudu wanaokula majani ndani (leaf miners), utitiri na whiteflies wanaoshambulia mazao kama mboga, mahindi, tikiti maji, kahawa, ndizi na parachichi, miongoni mwa mengine.

Pia inabainishwa kuwa una kiwango kikubwa cha nitrates, phosphorus na potassium ambavyo ni virutubisho muhimu vinavyohitajika kwa ukuaji wa mimea, na pia kuwa rafiki kwa mazingira.

Utafiti mwingine uliochapishwa katika tovuti ya Wiley Online Library, ambao ulihusisha majaribio ya kisayansi, ulifanyika Chuo Kikuu cha Egerton Njoro, Kenya, unaeleza kuwa kunyunyizia mimea ya nyanya mkojo wa sungura kwenye majani hupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya nzi weupe, viwavi (nymphs), na mayai yao. Vilevile, matumizi ya mkojo wa sungura bila kuchanganywa na maji yanaonesha uwezo wa juu zaidi wa kudhibiti nzi weupe katika hatua zote za ukuaji.

Ili kudhibiti kuungua kwa majani ya mimea pindi mkojo wa Sungura unapotumiwa kama kiua wadudu, inashauriwa kutumia kiwango cha kawaida ama kuchanganya na maji kiasi ili kuyaacha majani salama.​
Hili siyo la kuuliza hili. Wenzenu wanapiga hela kwa mradi huu wa kuuza mkojo wa sungura na kinyesi chake kwa gharama kubwa sana.
 
Mkojo wa sungura unaweza kutumika kama mbolea ya maji, na pia una harufu kali na kemikali ambapo unaweza kutumika kama dawa ya kuua au kufukuza wadudu kwenye mimea.

Binafsi nachukia sana harufu ya mkojo wa sungura, usiposafisha vizuri eneo lao harufu ile inakuwa kero sana.
 
Nimekuwa nikiona wafugaji wa sungura wakivuna mkojo wa wanyama hao na kudai kuwa unaweza kutumika kama mbolea na dawa ya kuulia wadudu kwenye mazao. Wakuu wa JamiiCheck uhalisia wa hili ni upi?
​
Niliwahi kusikia kutoka kwa wakulima wa mpunga, wanatumia sana mkojo wa Sungura kuua wadudu waharibifu kwa kunyunyiza kwenye mpunga
 
Nimekuwa nikiona wafugaji wa sungura wakivuna mkojo wa wanyama hao na kudai kuwa unaweza kutumika kama mbolea na dawa ya kuulia wadudu kwenye mazao. Wakuu wa JamiiCheck uhalisia wa hili ni upi?
watu wanasema, kuwa ni bidhaa ya asili, na salama kwa mazingira, wanyama na binadamu ukilinganisha na mbolea za viwandani au viuatilifu vyenye kemikali.
 
Back
Top Bottom