Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa amesema wao kama asasi za kiraia kila uchaguzi wamekuwa wakiandaa ajenda za wananchi kupitia ilani ya asasi za kiraia na kukabidhi kwa vyama vya siasa kabla hawajaandaa ilani zao.
Ngurumwa amesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025, iliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM imejibu mambo mengi yaliyokuwa yakisubiriwa na Watanzania ikiwemo mchakato wa Katiba Mpya.
“Ilani yetu tuliizindua mwaka jana na tukapeleka wa vyama vya siasa kama ulivyosikia wamekiri (CCM) kutoka mwaka jana tumewapelekea Ilani yetu. Lengo ni kwamba vyama vya siasa viende kutengeneza Ilani zenye ajenda za wananchi na asasi za kiraia,” amesema.
Amesema wakati mwingine wananchi wanashindwa kuzieleza changamoto zao kwa viongozi wanapokwenda kwenye kampeni kwa sababu ya muda hata hivyo zaidi ya asilimia 85 ya mapendekezo yao waliyopeleka katika vyama vya siasa yamechukuliwa kwa sehemu kubwa.
“Na kati ya mapendekezo ambayo kwa haraka haraka ni ya msingi na ni kiu ya Watanzania kwa muda mrefu ambayo yalikuwa kwenye ilani yetu namba moja ni Katiba Mpya. Tulieleza kabisa kwenye ilani yetu kwamba tuanzie pale tulipoishia,” amesema.