Naam,
Mwandishi nadhani kuna kipengele aidha kakiruka kwa makusudi ama hajui au hata ameandika na wachapishaji wakaona wakiweke kapuni.
Katika kundi la Sita basi kasahau kitu. Basi mimi nitaliita kundi la saba.
Kundi la saba na la ajabu ni la waganga wa kienyeji na wapiga ramli. Rais wetu ni mwafrika halisi kwa hiyo hajakumbatia kikweli kweli dini yoyote ya kigeni. Kwa hali hiyo, si vibaya nikisema, kwa uafrika wake ni mfuasi wa siri wa dini za jadi. Hili si tusi, dhambi wala dharau. Nimemshuhudia mwenyewe kwa mazungumzo ya ana kwa ana akihangaika na kulalamika juu ya mnyukano wa dini mbili kubwa hapa nchini (Uislamu na Ukiristo) na kweli haumpi raha hata kidogo.
Anajua jinsi dini hizi mbili zinavyotuhumiana juu ya maamuzi ya rais na serikali yanayozigusa dini hizi mbili. Wakiristo wanadai kwa wazi na sirini kuwa rais anawapendelea waislam wakati waislam nao wakidai wakiristo wanapendekelewa sana na serikali ya rais wetu. Matokeo yake ni rais kukosa msimamo na kubaki kulalamika na kutilia shaka kila ushauri anaopewa na watu watokao pande hizi mbili.
Kuna uvumi wa muda mrefu sasa kuwa rais wetu anapata faraja pale anaposhauriwa na waganga wa kienyeji kwa sababu anaamini hawana mgongano wa maslahi katika dini hizi mbili kuu! Kimantiki na kimsingi hii ni njia nzuri ya kutatua mnyukano wa dini kubwa pale unaposhauriwa na mtu wa tatu au wa katikati.
"Uvumi" huu umeendelea kueleza kuwa katika harakati za kuwasikiliza hawa waganga, rais amejikuta njia panda katika maamuzi mbalimbali. Ushauri wa waganga humfikia rais ama moja kwa moja au kupitia wapambe maalum, lakini utekelezaji wa ushauri huo huonekana kwa njia mbalimbali kama vile tabia sugu ya rais kuchelewa katika matukio mbalimbali na tabia ya rais kutoroka na kwenda sehemu huria kama michezoni. Mara kadhaa ndani na nje ya nchi, rais amekutwa katika maeneo yasiyo rasmi bila maandalizi wala kuwamo katika ratiba. Najua rais ana maisha binafsi lakini ni ruksa kuyahoji hasa yanapoonekana kuwa rasmi kwa kuwa yanatokea mara kwa mara.
Inasemekana kuwa kwa ushauri wa waganga rais pia amejikuta katika misiba, mazishi, kutembelea wagonjwa nyumbani na hospitali, sherehe za harusi, na hafla za asasi za kiraia zenye utata. Imesikika pia waganga hawa ndiyo wanaosikilizwa hata katika masuala ya afya yake kuliko hata madaktari wa ndani na nje ya nchi.
Eneo hili limejaa uvumi, umbeya na maneno ya mitaani yanayochangamsha mabaraza na vijiwe, lakini cha msingi na kinachogomba ni pale yanayosemwa yanapofanana na yanayosemwa. Ikiwa uvumi huu au sehemu yake ina ukweli, basi kundi hili ndilo pekee linalomshauri mheshimiwa rais katika mambo mengi na kwa hiyo ndilo limeshikiliwa mustakabali wa taifa letu kwa sasa.
Katika mazingira ambamo makundi mengine yamenyamazishwa, salama yetu iko wapi tunapokuwa mikononi mwa hawa washauri ambao ushauri wao haujapimwa na chombo chochote kinachojulikana?
Pimbi