- Source #1
- View Source #1
David Barnea, the head of the Israeli Mossad, has reportedly been killed in the recent Iranian strikes.
- Tunachokijua
- David Barnea ni mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Israel linalojulikana kama Mossad, aliyeteuliwa katika nafasi hiyo tangu mwaka 2021 akichukua nafasi ya Yossi Cohen aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo. Baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo moja ya majukumu yake makubwa yalikuwa ni kuizuia Iran dhidi ya uzalishaji wa silaha za nyuklia.Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Mgogoro kati ya Iran na Israel ulichukua sura mpya ya hatari mwezi Juni 2025, ukibeba historia ya chuki ya muda mrefu, mashambulizi ya maneno, na sasa mashambulizi ya moja kwa moja.
Chanzo chake ni cha muda mrefu, lakini hali ya sasa imechochewa na mfululizo wa matukio makubwa yaliyoanza rasmi kufumuka upya mnamo Aprili 13, 2024, wakati Iran ilirusha makombora na ndege zisizo na rubani zaidi ya 300 dhidi ya Israel ikiwa ni mara ya kwanza kwa Iran kuishambulia Israel moja kwa moja kutoka ardhi yake. Israel ilijibu kwa shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya Iran katika mji wa Isfahan, ikieleza kuwa ni kulinda mamlaka yake na kuzuia mashambulizi ya baadaye.
Tarehe 9 Juni 2025, shambulizi kubwa la anga lilitokea karibu na mji wa Kermanshah, magharibi mwa Iran, likielekezwa kwenye kituo cha kijeshi cha Kikosi cha Quds cha Jeshi la Mapinduzi la Iran (IRGC), na baadaye kuwa na muendelezo wa majibizano ya mashambulizi kwa nyakati tofauti.
Mtumiaji mmoja wa mtandao wa X alichapisha taarifa yenye madai kuwa David Barnea, mkuu wa shirika la ujasusi la Israel, Mossad kuwa ameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran.
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu umejiridhisha kuwa taarifa hiyo si ya kweli kwani haijachapishwa na chanzo chochote cha kuaminika. Hata hivyo taarifa iliyoripotiwa leo Julai 03, 2025 inabainisha kuwa Benjamin Netanyau waziri mkuu wa Israel alifanya mazungumzo na kiongozi wa Mossad David Barnea katika makao makuu ya Mossad mnamo tarehe 02, 2025.
Gazeti la mtandaoni la Times of Israel Julai 03, 2025 linamnukuu David Barnea, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika makao makuu ya Mossad, kuwa amesema Israel ilisababisha “madhara makubwa” kwa Iran katika operesheni ya siku 12 iliyofanyika mwezi uliopita, lakini ameashiria uhitaji wa Jerusalem kuendeleza operesheni zake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Tumejidhatiti kuendelea kuchukua hatua kwa uthabiti ili kuzuia tishio la baadaye kutoka Iran dhidi ya Israel na kujitahidi kutumia kikamilifu fursa za kimkakati zilizo mbele yetu,” alisema Barnea wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika makao makuu ya Mossad usiku wa kuamkia leo.
Aidha katika ripoti yake Times of Israel iliambatanisha picha ya Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyau alipofanya mazungumzo na kiongozi wa Mossad David Barnea katika makao makuu ya Mossad mnamo tarehe 02, 2025.