Mkuu wa Wilaya Rorya asema wana Rorya tuchangamkie fursa kupitia Ziwa Victoria

Mkuu wa Wilaya Rorya asema wana Rorya tuchangamkie fursa kupitia Ziwa Victoria

BigTall

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2022
Posts
525
Reaction score
1,257
Wakazi wa Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa Ziwa Victoria unaouzunguka wilaya hiyo kwa asilimia 77.

Akizundua tawi la Benki ya CRDB eneo la mji mdogo wa Shirati leo Jumatano Aprili 5, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka ametaja fursa za kiuchumi zinazopatikana kutokana na uwepo wa ziwa hilo linalomilikiwa na Tanzania kwa asilimia kwa asilimia 51, kuwa ni ufugaji wa samaki kwenye vizimba, kilimo cha umwagiliaji na biashara ya mazao ya samaki.

Mataifa mengine yanayomiliki Ziwa Victoria ni Kenye yenye asilimia 6 na Uganda inayomiliki asilimia 43.
dc-chikoka.jpg


"Wana Rorya tutumie uwepo wa taasisi za fedha ikiwemo hili tawi jipya la benki ya CRDB kukopa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi mikubwa ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba ndani ya Ziwa Victoria, kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa mifugo kwa tija,” amesema Chikoka.

Mkuu huyo wa wilaya ameahidi kuwa ofisi yake itatoa msaada wa kitaalamu kwa wote wenye nia ya kukopa na kuwekeza kwenye miradi ya aina hiyo ambayo siyo tu itainua uchumi wa mtu mmoja mmoja, bali pia wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.

“Wilaya ya Rorya imejaaliwa ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao yote ya chakula na biashara, inapata mvua misimu miwili kwa mwaka na imepakana na Ziwa Victoria kwa asilimia 77; hatuna sababu ya kuendelea kuwa maskini. Tutumie fursa hizo na uwepo wa taasisi za fedha kujikwamua kiuchumi. Serikali iko tayari kutoa msaada unahitajika kufikia lengo hilo,” amesema na kuahidi Chikoka

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Rabala amewakaribisha wana Rorya kutumia uwepo wa tawi hilo jipya kujiendeleza kiuchumi kupitia huduma za kifedha ikiwemo mikopo nafuu kwa ajili ya mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

"Pamoja na nia ya kusogeza huduma kwa wananchi, tunatarajia uwepo wa tawi hili uwe ni kichocheo cha kukua kwa shughuli za kiuchumi kwa wana Rorya,” amesema Rabala

Irene Mbugi, mkazi wa mji wa Shirati ameushukuru uongozi wa Serikali Wilaya ya Rorya na Benki ya CRDB kwa kufunguliwa kwa tawi hilo akisema siyo tu umewaondolea adha ya kufuata huduma za kibenki eneo la Ingri Juu yaliyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, umbali wa zaidi ya kilometa 20, bali pia umeongeza fursa ya mikopo nafuu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa kati na wakubwa.

Hoja hiyo imeungwa mkono na mkazi mwingine wa mji wa Shirati, Ogutu Juma akisema; “Sasa tuna uwezo wa kuhifadhi fedha zetu benki badala ya vibubu. Hii siyo tu imeongeza usalama, bali pia uwezo wetu wa kukopesheka kwa ajili ya mitaji na shughuli mbalimbali za maendeleo,”


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom