Mwameja huwezi kumfananisha na Peter Manyika. Mwameja alicheza kipindi ambacho Simba ilitamba pia katika mechi za kimataifa, hasa mwaka 1993. Mwameja aliinyima kwa kiasi kikubwa ushindi timu hatari kutoka Angola iliyokuwa ikijulikana kama ASA, yaani Atletico Sportive Aviacao, ikiwa na winga hatari kabisa Libengue, na wachezaji maarufu kama vile kipa wao Kanka Vemba, Abilio, Arlindo, Kuleka, Lolo, Gito, Gerry na Libengue mwenyewe. Alizuia mabao ya wazi hasa waliporudiana kwao mjini Luanda na mechi iliisha 0-0 na Simba ilisonga hadi fainali ya kombe la CAF kwa jumla ya mabao 3-1 iliyoyapata Dar. Mechi nyingine ya maajabu ni ile ya ya kombe la Challenge kati Simba na El Mereikh ya Sudan ambapo zilikuwa katika kundi moja, Simba ikihitaji ushindi huku wenyeji El Mereikh wakihitaji walau sare. Mwameja aliokoa mabao ya wazi na hadi dakika za mwisho mwisho mambo yalikuwa 1-1, dakika ya 87 hivi Nteze John akaiandikia Simba bao la pili, taa zikazimwa, washabiki wakavamia uwanja na kuwapiga wachezaji na hasa Mwameja ambaye alishangilia bao la pili kwa kuwakatia kiuno washabiki wa Mereikh. Pambano lilivunjika na Simba wakalazimishwa wacheze tena kesho yake, wakajitoa maana walipigwa kweli kweli, na El Mereikh ikaingia kwa ushindi wa mezani na ikatakiwa ikutane na mahasimu wao El Hilal, na El Hilal wakajitoa kuungana na Simba kwa kusema kwamba hawawezi kucheza na timu iliyofungwa, yaani El Mereikh