Hili ndilo ninaloliona kila kona katika nchi yetu watu wanaukimbia ukweli, wanauogopa, unawasuta, unawachoma miyo yao kwa sababu wameamua kuishi katika uongo. Imeandikwa kuwa kweli itakuweka huru siku zote, lakini sisi tumeamua kujiweka katika uongo. Matokeo ya maisha yetu na hali ilivyo leo ni sababu ya unafiki na uongo, oungo na unafiki ndio imekuwa tabia yetu, watu wazima wanaopaswa kujiheshimu wanatamka uongo hadharani hali wakijua huo ni uongo. Waziri mkuu anasema hivi, Rais anasema hivi, ni wazi mmoja wapo ni muongo na anaongopa bila kujali kitu kwa vile anajua anaishi katika jamii iliyolelewa katika uongo, imefanya uongo sehemu ya maisha yao na kila wanapotaka kufanya lolote lile wanatoa sababu za uongo ambazo hizo ndizo zinazokubalika. Msema kweli anachukiwa na kupingwa, anatukanwa na kusakamwa, watu wanataka uongo tu, uongo ndio unaowapa faraja, ukweli unawanyima usingizi, wengine wanadiriki hata kuwashawishi wengine wasishiriki katika mijadala inayotafuta ukweli kwani hawautaki kuusikia ukweli wala hawataki wengine waujue ukweli. Tusizungumzie udini, tusitaje imani tuseme tu mambo ambayo viongozi wetu wametudanganya, tuyaoredheshe na pia tujiangalie tumefanya nini katika kushughulikia uongo wao halafu pia tujiangalie tumefanya nini katika kumshughulikia Mohamed Said na "uongo" wake halafu tupime tumetumia nguvu nyingi wapi.