MOI yasogeza huduma za kibingwa na kibobezi kongamano la wanawake TANESCO

MOI yasogeza huduma za kibingwa na kibobezi kongamano la wanawake TANESCO

Taasisi ya Mifupa-MOI

Senior Member
Joined
Apr 15, 2025
Posts
118
Reaction score
214
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imesogeza huduma za kibingwa na kibobezi kwa wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Kongamano la Pili la Wanawake wa shirika hilo lililolenga pia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Huduma zilizotolewa ni pamoja na uchunguzi wa awali wa magonjwa ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, tiba lishe na mazoezi tiba zikilenga kuwasaidia wanawake kupata tathmini ya kina ya afya zao pamoja na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa na wabobezi.

Akizungumza kando ya kongamano hilo leo Jumatano Machi 04, 2026, Dkt. Zehranabu Hussein, Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Mifupa na Mgongo MOI , amesema taasisi hiyo imeamua kusogeza huduma karibu na wanawake hao ili kuwapa fursa ya kupata uchunguzi wa mapema na tiba sahihi.

“Wanawake wengi wanabeba majukumu makubwa kazini na nyumbani, lakini mara nyingi husahau kuweka kipaumbele afya zao. Kupitia kongamano hili, tumewaletea huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ili waweze kuchunguzwa mapema na kupata ushauri sahihi,” amesema Dkt. Zehranabu

Kwa upande wake, Bi. Asha Kalinga, mfanyakazi wa TANESCO aliyepatiwa matibabu, amesema ujio wa wataalamu hao umekuwa msaada mkubwa kwake na wenzake.

“Nimepata fursa ya kuchunguzwa mgongo na kupata ushauri wa kitaalamu ambao usingekuwa rahisi kuupata kwa wakati huu... Huduma hizi zimetupa faraja kubwa sisi wanawake wa TANESCO,” amesema Bi. Kalinga.

Mbali na huduma za afya, kongamano hilo la pili limeendelea kuwa jukwaa la kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, likilenga kulinda afya za wanawake na familia zao dhidi ya madhara ya moshi unaotokana na nishati zisizo safi.
IMG-20260304-WA0210.jpg
IMG-20260304-WA0211.jpg
 
Back
Top Bottom