Maamuzi ya Magufuli yaibua maswali mengi
*Apuuza ushauri wa Makamba, manispaa ya Kinondoni
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, anaelekea kuanzisha mgogoro wa kiutendaji katika utawala wa serikali ya awamu ya nne.
Tayari kuna mvutano baina ya Magufuli na Manispaa ya Kinondoni pamoja na wawekezaji ambao wamemilikishwa viwanja kwa njia halali na za kisheria.
Hali hii mpya imeibuka kutokana na Waziri Magufuli kubariki kubuniwa kwa viwanja kadhaa eneo la Mikocheni, kikiwamo ilipo baa maarufu ya Rose Garden.
Mgogoro huu unahusisha Manispaa ya Kinondoni ambayo imetamka wazi kwamba Waziri huyo amepotoka kwa kubariki viwanja hivyo ambavyo vinaelezwa kubuniwa kinyume cha sheria.
Mbali na mvutano na Manispaa, pia wenye viwanja wengine wamejikuta wakifungiwa njia ya kufika kwenye eneo lao kutokana na kubuniwa kwa viwanja hivyo kwenye eneo la akiba ya barabara.
Mmoja wa watu ambao wamejikuta wakiathirika na uamuzi wa Magufuli wa kubariki viwanja namba 948 hadi 951, ni Kampuni ya ZEK Group ambayo ilinunua viwanja namba 717/5 na 717/4 kutoka Simu 2000 Ltd kwa ajili ya kuwekeza mradi mkubwa wa mabilioni ya shilingi.
Akizungumzia suala hilo jana, Mwenyekiti Mtendaji wa ZEK Group, Zadock Koola, alisema pamoja na kumweleza Waziri Magufuli juu ya mkanganyiko uliokuwako juu ya kubuniwa kwa viwanja hivyo, ameamua kuvitambua bila hata kujibu barua waliyomwandikia mwaka jana, wakimuomba kuingilia kati mgogoro huo.
Hatua ya Magufuli ya kuvitambua viwanja hivyo juzi ni majibu kwa Baraza la Madiwani la Kinondoni chini ya Meya wao, Salum Londa, ambalo lilimtaka awajibike kutokana na kuvamiwa kwa eneo la wazi la barabara ambalo limemegwa na kupimwa viwanja kinyume cha taratibu za sheria ya ardhi.
Madiwani hao wamekwisha kusisitiza mara kadhaa kwamba viwanja hivyo pamoja na ilipo baa ya Rose Garden ni batili na kuna mlolongo wa nyaraka unaoonyesha kwamba eneo hilo ni la barabara lakini liligeuzwa viwanja na watu walioshirikiana na maafisa wa serikali.
Kulingana na mlolongo wa nyaraka zilizoko, mmiliki wa baa ya Rose Garden, Damas Assey, aliomba kibali kutoka Kampuni ya Simu Tanzania, ofisi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Dar es Salaam Kaskazini, kutumia eneo iliko baa hiyo mwaka 1995.
Ofisi hiyo kwa barua ya Novemba 2, 1995 ilimruhusu Assey kuendesha shughuli kwenye eneo hilo likiwa ni mbele ya viwanja namba 717/5 na 717/4 ambako kiwanda cha uchapaji cha TTCL kilikuwako wakati huo, lakini ikamkataza kujenga jengo la kudumu. Wakati huo alikuwa akifanya biashara ya kuuza maua.
Hata hivyo, baada ya Simu 2000 Ltd kutaka kuuza eneo hilo na kuiomba Manispaa ya Kinondoni kuondoa vibanda vyote vilivyokuwa mbele ya viwanja hivyo kwa sababu wawekezaji walikuwa wakisita kuvinunua, Assey alifungua kesi mahakamani kuzuia kuvunjwa kwa baa hiyo.
Wakati kesi ikiendelea mahakamani, kwa nyakati tofauti na baada ya uchunguzi wa kina, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upimaji Ramani Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Julai 12, 2004 ilimwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ikimwagiza kwamba utaratibu wa kubuni na kupima viwanja kikiwamo 951 iliko baa ya Rose Garden haukufuatwa na kwamba kiwanja hicho kifutwe na mawe ya mpaka (beacons) yangolewe.
Nayo Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ikiwa imepokea maelekezo ya Wizara ya Ardhi, Novemba 18, 2004 ilimwandikia Assey ikimtaarifu kwamba kiwanja alichojenga baa ya Rose Garden ni batili kwa sababu kimebuniwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara na kumtaka aondoke kwenye eneo hilo.
Barua hiyo ya Manispaa pia ilihusu viwanja namba 948 951 ambavyo vilikuwa vimepimwa kinyume cha taratibu na kwa maana hiyo hati zake zilikuwa zimefutwa.
Pamoja na barua hizo mbili, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, aliingilia kati mgogoro huo Juni 4, 2004 kwa kumtaarifu aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, E. Berege, kwamba eneo la barabara limevamiwa na kubuniwa viwanja hivyo kinyume cha sheria. Alimtaka kuhakikisha kwamba majengo yote ya kudumu yaliyojengwa kwenye eneo la barabara yanabomolewa na taarifa kuwasilishwa kwake.
Hayo yakitokea, Assey alifungua kesi namba 23/2006 Mahakana Kuu kitengo cha ardhi kupinga kuhamishwa eneo hilo, lakini wakati huo huo akisukuma maombi ya kumilikishwa kiwanja hicho kisheria.
Kiwanja hicho namba 951 mwaka jana katikati kilipewa hati miliki wakati huo shauri likiwa bado mahakamani, na Waziri Magufuli akijua kwamba Manispaa ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Upimaji Ramani wa Wizara yake na hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kila mmoja kwa wakati tofauti na kwa uchunguzi unaojitegemea walibainisha kuwako na utata mkubwa wa viwanja hivyo, alibariki miliki hiyo.
Uamuzi wa juzi wa Mafuguli kuhalalisha viwanja hivyo, huku mwenyewe alipokuwa Waziri wa Ujenzi kwenye utawala wa Rais Benjamin Mkapa akiwa amepigania maeneo ya barabara yasivamiwe na kushiriki katika bomoabomoa zilizoaacha maelfu ya watu bila makazi, umemfungua katika sura mpya ambayo haijajulikana.
Alipochaguliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Mandeleo ya Makazi, Magufuli, alitoa ilani kwamba wote waliovamia maeneo ya wazi na kumilikishwa kinyume cha sheria watanyanganywa na kuonya kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kumilikishwa maeneo ya wazi bila ya kibali cha Waziri wa Ardhi.
Kauli hiyo haioani na uamuzi wake wa sasa ambao si tu umemweka kwenye mapambano na mamlaka nyingine za wananchi, Baraza la Madiwani, bali pia na watedaji ndani ya wizara yake mwenyewe.
Wakati huo huo, Andrew Msechu anaripoti kuwa Waziri Magufuli amesema ofisi yake iko tayari kuungana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, kuhakikisha inawashughulikia matajiri walafi wanaodhulumu ardhi ya wanyonge.
Alitoa kauli hiyo wakati wa kuapishwa kwa Baraza la Ardhi la Manispaa tatu za Mkoa wa Dar es Salaam jana, ambapo Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na namna matajiri wanavyotumia uwezo wao kifedha kudhulumu viwanja na ardhi za wanyonge, baadhi wakiwadhulumu hata wajane na yatima.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, ni lazima haki itendeke na kwamba hata kama tajiri au mwenye mamlaka fulani alivamia eneo na kujenga ni lazima aondoke iwapo itathibitika kuwa kwa namna yoyote alihusika kuingilia haki za watu wengine.
"Hawa matajiri jeuri wanaotumia uwezo wao kuvamia hawatakiwi kupewa nafasi, tumieni uwezo wenu kuhakikisha kuwa haki inatendeka, hata kama walishajenga maghorofa katika maeneo hayo waondoke, la waelewane na wale wenye maeneo hayo," alisema.
Aliongeza kuwa katika kutatua migogoro hiyo, hata pale itakapobidi serikali kushtakiwa katika mabaraza ya Ardhi yaliyoundwa nchi nzima na kushindwa basi ishindwe.
Magufuli aliagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinawashughulikia kikamilifu maafisa ardhi ambao kwa namna yoyote walitajwa kuhusika katika kuzalisha migogoro yote iliyowasilishwa katika Tume Mabaraza yaliyoundwa na Rais kufuatilia migogoro ya ardhi ambayo tayari taarifa zake zilishatolewa.
Magufuli alitoa agizo hilo mara baada ya kupokea kilio cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliyelalamikia maafisa ardhi waliopo chini ya Wizara inayoongozwa na Magufuli kwa kuhusika kwao katika kuzalisha migogoro ya ardhi.
Mabaraza hayo ya Wilaya yaliundwa kwa dharura na Rais Jakaya Kikwete mwaka jana, ambayo yalikuwa yakisimamiwa na Halmashauri za Wilaya chini ya uenyekiti wa Mameya nchi nzima.
Alielezea kushangazwa kwake na ukubwa wa tatizo la zaidi ya migogoro 14,500 iliyopo Wilayani Kinondoni ambayo tayari inashughulikiwa na Wizara yake, huku maafisa wa ardhi wakiwa wanahusika zaidi katika ugawaji wa viwanja kwa watu zaidi ya mmoja.
Akitua mzigo wake kwa Waziri Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alielekeza kilio chake kwa kwa maafisa Ardhi waliopo chini ya Waziri Magufuli ambao kwa kiasi kikubwa wameonekana kuwa chanzo cha migogoro mingi ya ardhi iliyopo katika jiji la Dar es Salaam.
Kandoro alisema Manispaa ya Kinondoni pia ndiyo inayoongoza kwa migogoro ya ardhi iliyofikishwa ofisini kwake, ikiwa na migogoro 1,028, ikifuatiwa na Temeke 300 na Ilala 209.
Wajumbe wa mabaraza hayo ni Kenneth Wallace, Salma Dossi na aliyewahi kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa katika baadhi ya mikoa nchini Mary Chipungahelo ambao watakuwa katika Baraza hilo Manispaa ya Ilala.
Katika Manispaa ya Kinondoni yumo aliyewahi kuwa Waziri wa Nyumba, Tabitha Siwale, Heavenlight Bethuel na Ruth Lugarisha, na Temeke wakiwa ni Sautiel Kulaba, Daniel Mtagula, Azid Ulembo, Marina Mlunde na Rhoda Kahatano.
source: Mwananchi