Serikali ya Kaunti ya Nairobi imeondoa Geoffrey Mosiria katika nafasi yake ya Chief Officer anayesimamia Public Participation, Citizen Engagement and Customer Service, katika mabadiliko yanayokuja wakati ambapo tayari ametangaza nia ya kuwania ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kwa mujibu wa tangazo lililosainiwa na Katibu wa Kaunti ya Nairobi, Machel Waikenda, Zipporah Njeri Mwangi ameteuliwa kushikilia kwa muda wadhifa huo. Aidha Zipporah ataendelea pia kusimamia kitengo chake cha awali cha City Culture, Arts and Tourism.
Baada ya kuondolewa kwake, Mosiria ametoa taarifa akimshukuru Gavana Sakaja kwa kufanya rasmi hatua hiyo, huku akidai kuwa kwa muda mrefu alikuwa amepokonywa majukumu yake ya kiutawala. Mosiria amedai kuwa mgogoro wao ulianza Desemba 2023, alipokuwa katika kitengo cha afya, na kwamba baadaye alihamishwa kutoka kitengo kimoja hadi kingine huku akipunguziwa mamlaka ya kutekeleza majukumu yake.
Mosiria pia amedai kuwa bajeti ya kitengo cha afya alichokuwa akisimamia ilipunguzwa kutoka bilioni 1.2 hadi milioni 100 baada ya kutokubaliana kuhusu taratibu za manunuzi.
Je, azma ya kugombea ugavana imechangia mabadiliko hayo?
Mosiria alitangaza nia ya kuwania ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027, akijieleza kama mgombea anayetaka kuleta mabadiliko katika uongozi na utoaji wa huduma jijini. Kuondolewa kwake sasa kunazua maswali kuhusu nafasi yake katika siasa za Nairobi kuelekea uchaguzi huo.
Hata hivyo, ingawa muda wa tukio hilo unavutia kisiasa, hakuna sababu rasmi iliyotajwa katika tangazo la kaunti inayothibitisha kuwa azma yake ya kugombea ugavana ndiyo iliyosababisha kuondolewa kwake.
Kwa wakazi wa Nairobi, suala muhimu litakuwa kuona jinsi mabadiliko haya yatakavyoathiri huduma za umma, ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji katika City Hall.
Je, Mosiria kuondolewa City Hall siku chache baada ya kutangaza kuwania ugavana wa Nairobi ni mabadiliko ya kawaida ya kiutawala, au kuna maswali ya kisiasa ambayo Sakaja anapaswa kujibu?