Posted Date::3/3/2008
Jengo la ghorofa 12 lanusurika kuteketezwa kwa moto Dar
James Magai na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
MOTO mkubwa uzuka na kuteketeza nusu ya sehemu ya chini jengo la Ushirika lililopo Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Ofisi zilizoteketea ni zile zinazotazamana upande na Benki ya CRDB, ambayo nayo imeponea chupuchupu kuungua.
Jengo hilo lenye gorofa 12 limepana ofisi nyingi zikiweomo za serikalia makampuni na watu binafi na pia ni Makao Makuu ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji nchini.
Hata hivyo, tukio hilo halikusababisha madhara kwa ofisi za kikosi hicho ambacho kipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, baada ya askari wake kuwahi kuudhibiti moto huo usipande ghorofani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Masindoki Masindoki, alithibitisha kutokea kwa moto huo ambao ulianza juzi saa 4.30 usiku na kuteketeza mali zote zilizokuwemo ndani ya ofisi hizo.
Masindoki alisema hadi jana, thamani ya mali ilikuwa imeteketea haikuwa imejulikana na kwamba hakuna athari zozote kwa binadamu.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, Mohamed Kapamba, alilisema moto huo ulianza kuwaka chini kwa chini.
Kapamba alifafanua kwamba, baada ya taarifa hizo kusambaa kuanzia saa nne ilichukua muda wa dakika nne kwa magari ya vikosi mbalimbali ikiwemo ya kikosi hicho na Jiji kufika eneo la tukio.
Alipoulizwa vipi moto huo ulichukua muda mrefu kuzimwa wakati umetokeoa Makao Makuu ya Ofisi za Zimamoto na karibu na Jiji, alijibu: Kilichochelewesha ni mfumo wa umeme, ilibidi tuanze kuwasiliana na wenzetu Tanesco (Shirika la Umeme nchini), ambao walikuja baadaye, alisisitiza Kapamba.
Kapamba aliongeza kwamba, kama kusingekuwa na tatizo la mfumo wa umeme na Tanesco wangewahi, ni dhahiri wangeweza kuudhibiti moto huo mapema.
Alitaja sababu nyingine kubwa ya pili kwamba, ofisi nyingi zilikuwa zimefungwa kwa mageti maalumu hivyo kazi ya kuvunja nayo ilichukua muda.
Ule moto awali uliwaka ndani kwa ndani, sasa hadi kujitokeza nje ulikuwa tayari umekuwa mkubwa, hadi kuvunja mageti ya milango na kuingia nayo ilichukua muda,? alisisitiza Kapamba.
Kuhusu vipi waliweza kuzuia ofisi zao za ghorofa ya nne zisiungue, alisema wakati ukiwaka askari wa kikosi hicho waliokuwa zamu walidhibiti mfumo wa umeme na kujipanga kuhakikisha moto haufiki katika ofisi zao.
Alisema lita za maji zilizotumika ni zaidi ya 30,000 kwa taarifa za awali na kuongeza kwamba bado tathimni inaendelea kufanyika.
Kwa upande wa mmoja wa askari aliyeshudia tukio hilo ambaye ni kutoka kikosi cha jiji Makao Makuu, Sud Alfan, alisema walipata taarifa za kuungua kwa jengo hilo saa 4.00 usiku na kufika eneo hilo saa 4.11 na kukuta moto mkali katika moja ya ofisi hizo.
Shuhuda huyo, alisema chanzo cha moto huo kinawezekana kikawa ni mashine ya kupozea upepo (Air Condition- AC) kwa kuwa ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuungua.
Hatujawa na uhakika, lakini tunahisi chanzo cha moto huo ni AC ambayo iliachwa bila kuzimwa, kwani ndio kifaa cha kwanza kuungua humu. Labda kuna mfanyakazi wa ofisi hiyo ambaye alikuja ofisini jana akawasha mashine hiyo halafu akasahau kuizima na kusababisha hitilafu ya umeme, alisema Alfan.
Alfan alifafanua kwamba, ukali wa moto huo ulichochewa na aina ya malighafi zilizotumika kutengeza dari katika jengo hilo.
Dari za jengo hilo zimetengenezwa kwa majaribosi aina ya takataka za mbao na sehemu kubwa ya kuta za ofisi hizo, zilikuwa ni za mbao jambo ambalo lilisababisha moto huo kuwaka kwa nguvu sana,alisema.
Taarifa zaidi ambazo hazikuthibitishwa, zilisema askari wa wawili, Donald Ndimbo na Mohamed Mtemba, walijeruhiwa baada ya kuangukiwa na vioo wakati wakiwa katika harakati za kuzima moto huo.
Kamanda wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji cha Kampuni ya Nihgt Support, Kevin Lubela naye alisema, inahofiwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika AC ndani ya ofisi moja na kwamba walifika katika eneo latukio saa 6.30 usiku wakati shughuli ya uzimaji moto huo ilikamilika saa 11 alfajiri.
Mwananchi lilifika katika eneo la tukio saa 12.30 asubuhi na kukuta vikosi hivyo vikijaribu kuzima moto huo huku wamiliki wa ofisi na mali zilizoteketea, wakilia wakiwemo mama mmoja ambaye alisema kasha lote la pesa limeteketea, bila kutaja jina lake, ofisi na kiasi hicho cha pesa kilichoteketea.
Baadhi ya wapangaji katika jengo hilo, Agness Mtiganzi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Aglex Company Ltd, na Mama Mohamed Suleiman wa Kampuni ya Uchapaji ya Education Books Publishers, walisema mali zao nyingi ziliteketea.
Hata hivyo, wapangaji hao hawakuwa tayari kueleza thamani na aina ya mali zilizoteketea mbali ya kusisitiza mali nyingi zimeteketea.
Moto huo ulizimwa kwa ushirikiano wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji cha Jiji, Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji cha Bandari, Night Support, Security Group, Ultimate Security na Kikosi cha Zima Moto cha Uwanja wa Ndege.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dares Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana, alifika eneo la tukio na alipohojiwa na Radio Tanzania (RTD) ambayo iko chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alisema inasadikiwa ukali wa moto huo, ulioteketeza ofisi za jengo hilo na ulitokana na makaratasi ambayo ni malighafi, iliyotumika kutengeneza ofisi mbalimbali katika jengo hilo.
Tukio hili ni moja ya janga kubwa kuwahi kulikumba jiji la Dar es Salaam katika siku za karibuni, ambapo la mwisho lilikuwa ni kuungua kwa Hoteli ya Sea Cliff, mwishoni mwaka jana na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.