Na Ndesanjo Macha
ILIKUWAJE hadi wakatokea watu wakatuibia mamilioni ya fedha kupitia ununuzi wa rada? Wakatuleta mikataba ya kiajabu ajabu kama ya Richmond. Ilikuwaje wakaja jamaa na kampuni yao ya magirini wakituahidi kuwa watatatua tatizo letu la umeme?
Hii sio mara ya kwanza kwa mikataba ya mamilioni kupitia kwenye mikono michafu ya baadhi ya Watanzania wenye dhamana ya kulinda maslahi yetu. Wala haitakuwa mara ya mwisho. Usishangae sana unaposikia habari kama hizi. Tena habari unazozipata ni kama asilimia moja ya ulaji unaoendelea kwa kasi mpya.
Mikataba wanasaini ofisini mwao, wananchi hatuonyeshwi. Hatujui inasema nini. Sijui kwa nini huwa hawatuonyeshi hii mikataba tuisome herufi hata herufi. Mikataba hii sio mikataba yao binafsi, ni mikataba inayohusu mali na maslahi ya umma. Katika kusaini mikataba hiyo ofisini mwao, huko huko ndio asilimia kumi zinaingia matumboni. Vitambi vinazidi kuwa vikubwa. Suti zinanunuliwa. Majumba yanajengwa. Biashara zinaanzishwa. Vitega uchumi vinaongezwa. Wananchi tukilia njaa tunalishwa kauli mbiu.
Kama ambavyo imekuwa miaka na miaka, nchi inaongozwa kwa kauli mbiu na ahadi za mara moja kila baada ya miaka mitano. Ahadi ambazo tunapewa kila miaka mitano ingekuwa zinatimizwa, huenda tungekuwa hivi sasa tunashindana na nchi kama Singapore. Huenda tungekuwa tunatoa misaada kwa nchi majirani zetu.
Nchi ya kauli mbiu na mapambio. Mapambio ya chama twawala. Twawala nanyi mwalala. Mapambio: vyombo vya habari ni sauti ya pili, wananchi sauti ya nne. Wakereketwa sauti ya kwanza. Wakoloni wapya kwa jina la washauri, Benki ya Dunia (eti benki ya dunia), shirika la fedha duniani, n.k., ni wapiga ala. Wanatuambia kwenye ripoti zao kuwa serikali yetu inaendesha uchumi kwa ufanisi na imepiga hatua mbele kwenye vita dhidi ya rushwa.
Eti nini? Rushwa? Niambie, toka uzaliwe, umemsikia nani kati ya akina nani hii amefikishwa mahakamani kwa rushwa kisha akaenda jela? Niambie ni kesi ngapi unazifahamu za rushwa ya mamilioni? Ukisikia mtu kakamatwa kwa rushwa, utasikia elfu 50 au laki moja. Wote hawa ni dagaa tu. Samaki wakubwa mahakamani hawafikishwi, jela hawaioni. Kwanza walioko kwenye tume ya rushwa ni dagaa, watathubutu kuwaendea samaki wakubwa? Wamezwe?
Naomba unipe orodha ya Watanzania waliofikishwa mahakamani au walioko jela kwa kula rushwa ya mamilioni. Ni akina nani hao? Hiyo vita tunayoambiwa ya rushwa inapiganiwa kwenye ripoti zinazotumwa kwa wazungu kuwafurahisha na kwenye hotuba za kutupumbaza. Watupe rekodi, takwimu, majina yao, n.k. Tuachilie mbali watu kufikishwa mahakamani, niambie ni akina nani katika kambi ya samaki wakubwa ambao wameshawahi hata kuchunguzwa tu. Sio kushtakiwa, hapana. Kuchunguzwa. Wapi.
Kuuziana maneno tu na tabasamu. Ndio maana Mwalimu Nyerere akatuambia uongozi sio sura. Kama ni sura, basi mkaribishe huyo mwenye sura nzuri mkanywe naye chai. Tunaongelea maslahi ya nchi na watu wake. Sio utani utani na ushabiki wa mtaani. Eti, aah, fulani ana siha njema na ni mzuri na mtanashati. Wanakuonyesha picha zake akiwa anatabasamu.
Tuache utani na masuala ya kuongoza nchi katika kipindi ambacho tuna mtihani mkubwa wa kuamua mwelekeo wa nchi yetu na jinsi ambavyo utajiri wake wa maliasili na akili na ubunifu wa watu wake vitakavyotumiwa ili kutunufaisha sisi na vizazi vijavyo. Narudia, utani utani na ushabiki wa sijui rangi ya kijani, nyeupe, na nyekundu acha nao kabisa. Unajiumiza mwenyewe na wanao na wajukuu zako.
Wakati shule zilizoko kwenye jiji ambalo ndio kitovu cha nchi, Dasalama, hazionyeshi kuwa tayari kuandaa watoto wetu kwa ajili ya dunia mpya ya ushindani wa sayansi na teknolojia, tunaambiwa kuwa Rais wetu anahitaji ndege mpya ya kifahari kwakuwa ana hadhi kubwa. Eti ndege ya hadhi yake.
Hivi nani kasema kuwa Rais ni mtu mwenye hadhi ya juu kuliko Watanzania wote? Ofisi yake ina majukumu makubwa, ndio. Lakini hii hadhi tunayoambiwa ambayo inahitaji dege la kifahari sijui imetoka wapi. Hivi huyu si mtumishi wetu? Watu tuna mawazo tofauti, achilia mbali suala la ndege. Mimi binafsi sioni sababu yoyote ya Rais eti kufunguliwa mlango wa gari. Kama anaumwa, sawa. Mfungulie mlango, na hata mbebeni kabisa.
Kisha mpelekeni hospitali (tena hospitali ambayo wananchi wengine wanakwenda, sio sijui Ulaya, mara Afrika Kusini). Ila kama ni mzima wa afya hakuna sababu yoyote ya kuwapa binadamu wengine kazi za kitumwa na wengine vyeo vya kimungumungu hapa duniani.
Kumfungulia binadamu mwenzako mlango wakati ana afya njema ni aina ya utumwa unaomfanya yule anayefunguliwa mlango kukwezwa kwenye daraja linalokaribia kuabudiwa. Ndio ibada hizo tulizoambiwa na mchora vikaragosi wa Kenya. Ibada za vyombo vya habari Tanzania kumlamba miguu. Kama anashindwa kufungua mlango wa gari, basi hata kuvaa nguo avalishwe, tuajiri mtu wa kumsaidia kupiga mswaki. Mtu wa kumlisha.
Tusimnunulie ndege tu, bali meli na helikopta pia. Tunaweza pia kumnunulia visiwa vyetu vilivyoko bahari ya hindi iwapo Waarabu na Wahindi hawajavinunua vyote.
Kufungua mlango wa gari ni jambo la kawaida. Hakupunguzi heshima aliyonayo rais, hakumfanyi awe nusu mtu, hakumfanyi ashindwe kutekeleza kazi zake. Kunachofanya ni kuondoa kiwingu cha ibada za miungu watu ambazo zinaelekea kutumika kuwaenzi na kuwapamba marais na viongozi wetu. Vitabu wanavyovitumia kuapa vinatuambia kuwa wanaojikweza watashushwa. Ndio, watashushwa na hizo kashfa wanazoshindwa kulieleza taifa undani wake. Kashfa zinabisha hodi kushoto, kulia, juu, chini, wanabaki kurandaranda dunia nzima kama vile mambo ni shwari.
Ni lini utamaduni wa viongozi kukubali makosa na kueleza ukweli utaanza? Yule wa uwazi na ukweli hakufanya hivyo. Alificha kiasi cha kufanya maneno uwazi na ukweli kutokuwa na maana yoyote. Yule wa fagio la chuma hakufagia chochote. Kila kitu kiliruhusiwa ikiwa ni pamoja na fagio la chuma kuruhusiwa lisifagie chochote.
Sasa watu tunatofautiana. Wako wanaolaumu viongozi kwa ulaghai unaoendelea nchini. Wanalaumu kisha wanaendelea na hamsini zao. Wako wanaotoa lawama kisha wanatafuta njia za kuhakikisha kuwa ulaghai na ufidhuli huu mchafu unamalizika na wanaohusika kujibu mbele ya umma.
Njia hii ya pili ni muhimu sana. Ni jinsi gani wananchi wanaweza kuhakikisha kuwa ulaghai hauendelei kutokea au ukitokea wanaohusika wanapelekwa kula ugali mbichi na maji ya maharagwe yaliyochemshwa?
Hapa ndipo penye mchezo. Hapa ndipo penye fainali. Tunaweza kuorodhesha kila aina ya uchafu, uongo, na utumbo wanaotufanyia watawala wetu. Hiyo ni kazi rahisi sana. Shughuli iko kwenye suala la kuhakikisha kuwa sheria inafuata mkondo wake, taratibu za kuchunguza wanaotumuhiwa kuhujumu uchumi zinafuatwa, wenye hatia kufikishwa mahakamani na wala sio kuambiwe eti warudishe fedha walizoiba, na zaidi kuhakikisha kuwa wizi wa mchana mchana kama huu hautokei tena.
Mjadala huu lazima tuuanze hivi sasa. Ni vipi wananchi, ambao ndio wengi kuliko viongozi walaghai, tutakuwa na uwezo, njia, na mfumo imara wa kuhakikisha kuwa hatuibiwi kama watoto wadogo? Kuna wakati niliandika kuhusu mbinu za kuleta mabadiliko kwenye jamii. Nilisema kuwa iwapo hujaweza kumwajibisha mwenyekiti wa serikali za mtaani kwenu, ni vipi utaweza kumwajibisha raisi, mbunge, au waziri? Kama hujaweza kuunda vuguvugu mtaani kwenu kuhakikisha kuwa mnaondoa wezi, mnajenga utamaduni wa kutupa takataka sehemu zinazohusika, mna utaratibu wa kusafisha mtaa wenu, n.k., ni vipi utaweza kuongelea suala la utunzaji wa mazingira kitaifa au kampeni ya kukamata majambazi kitaifa?
Utakapoweza kuleta mabadiliko mtaani kwenu kwa kushirikiana na wenzako, hapo utakuwa umeanza safari ya kuleta mabadiliko kitaifa. Utajifunza mbinu na kanuni muhimu za harakati za kijamii na kisiasa.
Utakuwa na uzoefu ambao utakusaidia kuweza kuleta mabadiliko makubwa ya kitaifa. Anza mtaani kwenu kisha panda juu. Unaweza hata kuanza kwa balozi. Makundi haya madogo madogo yanaendesha vuguvugu la kuleta mabadiliko katika mitaa na vitongoji, ndio haya haya yanakuja kuungana na kutumia mbinu na mshikamano unaotokana na uzoefu wa kuleta mabadiliko madogo madogo ili kuleta mabadiliko makubwa.
Hii ndio changamoto tuliyonayo. Je tunaweza kuhakikisha kuwa wilaya zetu zinatumia fedha zake sawasawa? Je bajeti ya shule anayokwenda mwanao unaijua? Je inatumiwa ipasavyo? Je unajua manispaa yako ina bajeti gani? Inatumia vipi fedha hizo? Je unajua ripoti ya mkaguzi wa mahesabu wa manispaa yako au wilaya yako inasema nini? Je kituo cha polisi unapoishi kina askari wa kutosha? Je ni waadilifu? Kama jibu ni hapana, unafanya nini? Unamsubiri nani?
Ilikuwaje tukafika hatua hii ya kuingizwa mjini na kila kampuni kubwa inayoingia nchini? Iwe ni umeme, madini, mawasiliano, utaliitumeingizwa mjini. Ilikuwaje? Ulikuwa wapi? Anza sasa kujifunza jinsi ya kuleta mabadiliko ya jamii, jinsi ya kulazimisha viongozi kujali kiapo na majukumu yao. Waonyesha kuwa unajua kuwa kuwa wao ni watumishi wako na una uwezo, mbinu, na hata sababu za kuwaondoa kwenye kiti wanachotaka kukifanya cha enzi. Anza mtaani kwenu. Kisha kesho, tukusanyike twende bungeni Dodoma, keshokutwa twende ikulu.
Mwananchi