RUZUKU, UKABILA WAIGAWA CHADEMA
CHADEMA ndicho chama pekee nchini kilichokuwa kinaonekana kutokuwa na migogoro, lakini hili la ruzuku na mengine yanaelekea kukigawa katika makundi mawili ya CHADEMA MBOWE na CHADEMA WANGWE.
Hali hii imejitokeza baada ya kutokea malalamiko ya wanachama wa CHADEMA kususu masuala kadhaa ya msingi. Masuala hayo yameibua mgawanyo uliozaa makundi hayo mawili na baadaye Mwenyekiti wa chama hicho FREEMAN MBOWE akatangaza kumsimamisha Makamu Mwenyekiti (CHACHA WANGWE).
Kwa tafakuri pana kila Mtanzania alitarajia kwamba kabla ya kumsimamisha Makamu Mwenyekiti, CHACHA WANGWE, Mwenyekiti wa chama hicho alitakiwa kujibu tuhuma moja baada ya ingine ili kujisafisha yeye mwenyewe pamoja na viongozi wengine wa juu wa CHADEMA.
Kimsingi,CHACHA WANGWE anamtuhumu MBOWE katika masuala yafuatavyo:-
Mosi, Kuna matumizi mabaya ya ruzuku (ufisadi wa ruzuku) ndani ya CHADEMA Makao Makuu. Hivyo, CHACHA WANGWE anamtaka Mwenyekiti FREEMON MBOWE atoe maelezo ya matumizi ya Ruzuku, ambayo ni fedha ya walipa kodi inayotolewa na serikali kwa vyama vyenye wabunge. Aidha WANGWE anamtaka MBOWE aonyeshe mapato na matumizi ya Ruzuku hiyo katika vikao vya chama au aunde kamati ya kuchunguza tuhuma hizo. Pia, WANGWE ana mashaka na hesabu zinazoonyesha mgawanyo wa matumizi ya ruzuku yanayopelekwa kwa msajili wa vyama vya siasa kutoka chama cha CHADEMA.
Pili, CHACHA WANGWE hakubaliani na kitendo cha Mwenyekiti na Katibu Mkuu (DR WILBROAD SLAA) kuzuia ruzuku isifike mikoani. Anasema hali hii ina maana matawi ya chama yasifunguliwe na chama kisiwe na ofisi hali ambayo inadhoofisha chama. Vivyo hivyo, WANGWE hakubaliani na kitendo cha MBOWE kufuja fedha za chama kwa ziara za helkopta huku akiwaacha wagombea ubunge na udiwani wa chama chake hawana msaada wowote wa kifedha kutoka katika chama. Katika mazingira haya WANGWE anauliza nani anakihujumu chama kati ya MBOWE na WANGWE? Nani anadhoofisha CHADEMA?
Tatu, CHACHA WANGWE ana hoja kwamba MBOWE, anawajibika kuwaeleza watanzania, ni kwa vipi wabunge watano kati ya sita wa kuteuliwa (viti maalum) wote watoke mkoa wa Kilimanjaro ( MBOWE ni Mchaga wa Kilimanjaro). Ikumbukwe kwamba Tanzania bara ina mikoa 21 na Zanzibar mikoa 5. Kwa kawaida, idadi ya viti maalum inategemea idadi ya wabunge ambao chama kinapata katika uchaguzi mkuu, ambapo asilimia 90 ya viti vya ubunge zilizoleta viti maalum vya CHADEMA zilitoka kanda ya Ziwa. Hivyo, MBOWE kasahau kanda zilizosaidia CHADEMA ikipata viti maalum na kuvipeleka KILIMANJARO.
Nne, CHACHA WANGWE anamtaka MBOWE, aeleleze inakuwaje kati ya wakurugenzi nane wa Idara mbalimbali za CHADEMA wanne ni Wachaga wa Kilimanjaro?
Tano, WANGWE anamtaka MBOWE, aeleze umma wa watanzania inakuwaje Madereva wote wa Makao Makuu ya CHADEMA ni Wachaga kutoka Kilimanjaro?
Sita, WANGWE anataka MBOWE, ajibu tuhuma kwamba yeye mwenyewe, DR WILBROAD SLAA na PHILIMON NDESAMBULO wanajilipa fedha kwa ajili ya kurudisha gharama walizotumia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. WANGWE anauliza mbona wanachama wengine hawarudishiwi gharama hizo akiwemo yeye WANGWE? Je, huu siyo ufisadi? Je huku ni kutenda haki?
Saba, WANGWE anataka kujua ni kwa nini miaka minne iliyopita MBOWE alivunja tawi la CHADEMA mkoa wa DAR ES SALAAM na kubaki na CHADEMA Makao Makuu. Hatua hii imekifanya chama hicho kukosa viongozi na wawakilishi wa chama mkoa wa Dar ES salaam.
Nane, WANGWE anataka kujua kwa nini Wakurugenzi wote wa CHADEMA wameteuliwa na MBOWE badala ya kuteuliwa na Kamati Kuu ya chama kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA. Aidha, Kwa Mujibu wa katiba ya CHADEMA kifungu 7.7.3 (vii), Katibu mkuu anatakiwa kuwajibika kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekti. Hata hivyo, DR SLAA ambaye ni Katibu Mkuu wa CHADEMA hakuwa akitoa ushirikiano kwa WANGWE hadi kufikia kumnyima ofisi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA.
Tisa, Katika moja ya hatua za kumfukuza WANGWE katika Uongozi, Katibu Mkuu aliitisha kikao cha Kamati ya wazee wanne wa CHADEMA lakini kati yao wawili wakiwa wa kabila la Mwenyekiti . Wazee hao wa Kichaga ni EDWIN MTEI ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Wazee wa CHADEMA na PHILIMON NDESAMBULO. Hapo kulikuwa na mgongano wa kimaslahi (conflict of interest). Ikumbukwe kwamba, Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA Bw. EDWIN MTEI ni baba mzazi wa mke wa FREEMON MBOWE kwa maana kwamba MTEI ni mkwe wa MBOWE. Mke wa MBOWE anaitwa DR LILIAN EDWIN MTEI ( Hivi sasa anajulikana kwa jina la DR LILIAN FREEMON MBOWE) ni binti wa EDWIN MTEI.
Kumi, CHACHA WANGWE analalamika kwamba suala la kumfukuza liliibuka ghafla katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA wakati halikuwemo katika agenda. Inadaiwa kwamba MBOWE ndiye aliibua agenda hiyo. Kwa mujibu wa kanuni za CHADEMA, kama suala hilo lilitakiwa kuwa agenda ilitakiwa lijulishwe kwa wajumbe siku 21 kabla ya kikao ili wapate mawazo ya wanachama. Hata hivyo, liliibuka katika kikao bila mtuhumiwa CHACHA WANGWE kujiandaa. Aidha, katika kuhakikisha kuwa WANGWE anavuliwa madaraka yake kwenye kikao, baadhi ya viongozi waliotakiwa kuhudhuria kikao hicho kwa mujibu wa katibu hawakupata mwaliko kwa sababu ilihofiwa kuwa wangekuwa upande wa WANGWE.
Kwa ufupi WANGWE anadai kwamba kuna ufisadi Makao Makuu ya CHADEMA. Kwamba MBOWE hajatoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizo na badala yake anamtuhumu WANGWE kwamba anakigawa chama na kuamua kumsimamisha uongozi.
Katika uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti uliopita, CHACHA WANGWE hakuwa chaguo la Mwenyekiti MBOWE, lakini aliweza kushinda. Kutokana na kitendo cha CHACHA WANGWE kutangaza kwa mara ingine kugombea Uenyekiti wa CHADEMA katika uchaguzi wa Disemba 2008 amezidi kujenga maadui kutoka Makao Makuu ya chama hicho. Hofu ya MBOWE inatokana na ukweli kwamba, hivi sasa WANGWE anaungwa mkono na matawi mengi ya CHADEMA nchini kutokana na msiamamo wake wa kutenda haki na kusimamia ukweli daima.
Hivyo, MBOWE akamjengea zengwe kwamba, WANGWE anavujisha siri za chama lakini katika kikao cha Kamati Kuu hawakuweza kueleza siri ambazo WANGWE anadaiwa kuvujisha. Kwa sababu hiyo, WANGWE anadai kwamba hakuelezwa siri alizovujisha hatua ambayo inakidhi matakwa ya kisheria kwamba MBOWE amemhukumu WANGWE bila hatia. Hatua hii ina lengo la kukwaza ustawi wa demokrasia na utawala bora katika vyama vya siasa.
Katika hili la kuvujisha siri WANGWE anajitetea kwamba kama kuzungumza na wana CCM ni kosa basi mtu aliyetakiwa kuwajibika ni DR SLAA ambaye mke wake ni diwani wa kuchaguliwa wa CCM wakati mkewe CHACHA WANGWE ni mwanachama mwaminifu wa CHADEMA. Kitendo cha DR SLAA kuwa na mke mkereketwa wa CCM yamkini Nyaraka za siri za CHADEMA zinaweza kuangukia kirahisi kwa mkewe na hatimae CCM na pia wageni wa CHADEMA wanaofika nyumbani kwa DR SLAA ambako kuna tawi la CCM kwa maana ya mkewe DR SLAA ambaye anawajibika kuwakirimu wageni na hivyo kusikia mazungumzo yao. WANGWE anataka kujua ni nani kati yake na DR SLAA anaeweza kuvujisha siri za CHADEMA?
Aidha, imeonekana kwamba, kutokana na nafasi yake ya Ubunge WANGWE na wabunge wengine wa upinzani wanaweza kujipatia marafiki kutoka chama tawala CCM kama ambavyo Wabunge wa CCM wanaweza kuwa na marafiki kutoka vyama vya upinzani. Urafiki huu unaweza kuwa wa binafsi/kawaida kuliko mambo ya siasa kwa sababu ya uzalendo, hivyo tofauti ya itikadi siyo uadui bali ni suala la kusimamia ukweli kama ambavyo ZITTO KABWE alivyojumuika na wabunge wa CCM katika kamati ya madini ya Bomani.
Pia WANGWE anadai, kwamba kama kuzungumza na wana CCM ni kosa mbona MBOWE amewahi kuonekana akiwa katika mazungumzo na Rais JAKAYA KIKWETE hata kufikia kumkumbatia mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Halikadhalika MBOWE ameonekana katika mazungumzo na viongozi wengine wa CCM, vivyo hivyo wana CHADEMA wengine?
Kwa ujumla kashfa hizi zinakuja wakati bado baadhi ya Watanzania wanahoji uadilifu wa FREEMAN MBOWE. Kashfa ya kukopa na kushindwa kulipa deni la NSSF kwa muda stahiki ilitia mashaka ya uadilifu wa MBOWE kwa taifa lake. Hakika bila kujibu hoja nzito za WANGWE, Mwenyekiti MBOWE asitarajie kupata kura za Watanzania wenye fikra mbadala katika uchaguzi ujao ndani ya chama chake na asijisumbue kugombea Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Natoa mwito kwa MBOWE kuitisha mkutano wa waandishi wa Habari kujibu tuhuma moja baada ya nyingine. Vinginevyo MBOWE atakuwa ameingia katika kundi la Wenyeviti wa vyama vya siasa wanaoua demokrasia nchini.
Kwa upande mwingine, DR SLAA na KABWE ZITTO wamekuwa watu muhimu kwetu watanzania katika kutoa hoja zinazohusiana na ufisadi bungeni lakini inashangaza wameshindwa kudhibiti ufisadi wa MBOWE ndani ya CHADEMA na badala yake wamemwachia WANGWE pekee. Hakika watu hawa walitusaidia sana katika kuunda tume za kuchunguza Richmond na EPA inakuwaje kwa muda mrefu tangu Desemba 16, 2007 wanakalia ripoti ya Kamati ya Mziray iliyoundwa kuchunguza mambo yanayoweza kusababisha migogoro ndani ya CHADEMA? Kamati hiyo ilibaini ubaguzi wa kikabila na kidini katika CHADEMA lakini haikuwekwa wazi kwa Watanzania na wala haijafanyiwa kazi. Je tuwaelewe vipi viongozi hao wa CHADEMA? Ufisadi ni ule unaofanywa na viongozi wa serikali ya CCM tu? Je sio kweli kwamba Hisani siku zote inapasa kuanzia nyumbani???