MAPENZI ni hisia. Unapompata mtu anakupenda kwa dhati, ni vigumu sana kuyatambua mateso ya wengine wanayopitia kwenye mahusiano yao. Wapendanao wanajiona wapo kwenye dunia yao, wanapokuwa pamoja wanajihisi matajiri hata kama ni kapuku.
Unapokosea kumchagua mwenzi wa maisha mara nyingi unajikuta kwenye mateso mazito na siku zote kati ya mtihani mgumu kuufaulu katika masuala ya uhusiano wa kimapenzi ni kumpata mwenza sahihi mwenye mapenzi ya dhati.
Wengi wamejikuita wakiingia kwenye uhusiano na watu ambao hawana mapenzi ya dhati. Wanateseka, wanajaribu kuwavumilia wenzi wao ili labda pengine wanaweza kubadilika lakini wapi. Mwisho wa siku wanaishia kuachana.
Ni vizuri sana kwa wale wanaokwenda kuanzisha mahusiano mapya, wakawa makini sana katika kufanya utafiti juu ya wenza wao. Jiulize, unayempenda ana mapenzi ya dhati? Atakujali? Atakuthamini? Atakupa kipaumbele? Atakuheshimu?
Hili linawezekana endapo tu utafanya uchunguzi mapema kwa wakati ule unaonazisha uhusiano. Mwenye upendo wa dhati utamjua tu endapo utakuwa makini.
Penzi la kweli halilazimishwi, linaonekana dhahiri shahiri. Mpenzi wako unamjua kama ana mapenzi ya dhati kwako hata kwa kumuangalia tu machoni, anavyokujali, anavyokuhitaji na hata jinsi anavyokuthamini.