Kampuni ya Ujenzi ya China (PowerChina) imejenga mradi wa mfumo wa usambazaji maji katika jiji la Arusha nchini Tanzania, ambao unawasaidia wakazi wa jiji hilo kupata maji safi karibu na makazi yao.
Mmoja wa wakazi wa jiji hilo, Anna Emmanuel, mama wa watoto wanne anayeishi eneo la Njiro, anasema kwa sasa hana tena haja ya kukosa usingizi kwa kufikiria atapata wapi maji kwa ajili ya mtumizi ya familia yake, badala yake, hivi sasa anafurahia kupata maji safi na salama karibu sana na makazi yake.
Mama Anna ni miongoni mwa watu laki 4 wanaofaidika na mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambao ujenzi wake ulioanza mwezi Desemba, 2018, kukamilika Juni 27,2023. Anasena kabla ya mradi huo wa maji kutekelezwa, walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta maji ya mto ambayo si mazuri kwa kunywa, kupikia wala kufua nguo. Hivyo walilazimika kununua maji na mara nyingi watu hawakuwa na uwezo huo kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.
Akiwa na tabasamu kubwa, Anna anasema tangu kukamilika kwa mradi huo, kwa sasa wanaweza kupata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, na pia wanaweza kuweka akiba ya fedha kidogo waliyonayo kwa kuwa hawalazimiki tena kununua maji. Zaidi ya hayo, anasema kwa sasa hawakabiliwi tena na magonjwa ya mlipuko yanayotokana na maji machafu kama ilivyokuwa awali wakati wakitumia maji ya mtoni.
Kwa mujibu wa kampuni ya PowerChina, mradi wa usambazaji maji umejumuisha kulaza mabomba karibu kilomita 620, kujenga mabwawa 11 na kuunganisha mtandao wa mabomba ya maji kwa kaya 48,000.
Meneja mradi huo, Jin Denghui anasema, mradi huo umejumuisha kutafuta maji chini ya ardhi chini ya Mlima Kilimanjaro, ulioko umbali wa kilomita 100 kutoka Arusha, na kuyasambaza kila siku katika kaya zilizolengwa mjini Arusha. Anasema mradi huo umeboresha mazingira ya maisha kwa wakazi na kusaifia kupanua uchumi wa huko, na kuongeza kuwa, wakati wa ujenzi wa mradi huo, walitoa ajira kwa Zaidi ya watu 4,000 wa huko, kutoa mafunzo ya utaalamu wa uchomaji, na kutoa mafunzo kwa kundi la mafundi na watu wenye uwezo wa uongozi.
Katika utekelezaji wa mradi huo, kampuni hiyo ya China pia iliwajibika vema katika masuala ya kijamii kwa kuchangia maabara kwa shule ya huko, kutoa mafunzo mara kadhaa ya uokoaji wakati wa ajali, na kukarabati barabara za huko zilizoharibika kutokana na mmomonyoko wa ardhi, na hivyo kusifiwa sana na sekta mbalimbali za jamii.
Mwezi Januari, 2022, Wizara ya Maji ya nchini Tanzania iliandika barua kwa kampuni ya PowerChina, ikiishukuru kwa mchango wake mkubwa katika kukamilisha mradi huo wa maji mjini Arusha.